Ligi Kuu ya England ipo kwenye mapumziko kwa ajili ya mechi za kimataifa, huku Arsenal wakiongoza kwa tofauti ya pointi mbili.
Baada ya kupoteza mechi dhidi ya Manchester United katika dimba la Old Trafford Jumapili iliyopita, Arsenal wameahidi kurejea kwa nguvu zaidi.
Kadhalika, wameona kwamba mshambuliaji wao wa kati Olivier Giroud hawezi kuachwa mwenyewe, hivyo wanataka Januari waendelee kumsaka mshambuliaji wa Real Madrid, Karim Benzema.
Wenger alimtafuta Mfaransa mwenzake Benzema majira ya kiangazi lakini hakuweza kufikia makubaliano na Madrid, ila sasa inaelezwa kwamba Arsenal wapo tayari kutoa kitita kinachotakiwa na Real, pauni milioni 43 takriban.
Msimu wa kiangazi, Wenger alikuwa anataka amchukue Benzema (25), Angel Di Maria na Mesut Ozil, lakini alifanikiwa kumpata Ozil pekee.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Arsenal, Ivan Gazidis amesema kwamba wataangalia hali itakavyokuwa Januari, lakini akasema si sahihi kumwacha Giroud peke yake.
Mbadala wake kwa namba yake hasa ni Nicklas Bendtner lakini ameshaonesha nia ya kuondoka, huku akilalamika kwa nini hakuuzwa msimu wa kiangazi wakati klabu nyingi zilikuwa zikimtaka.
Bendtner katika hali ya kushangaza aliingizwa dakika ya 78 Jumapili kucheza dhidi ya Manchester United wakati katika mechi nyingine zilizopita alifanya hovyo.
Kutokana na mfumo wa Wenger anaoupendelea wa
4-2-3-1 kwa sasa Giroud anaonekana kuwa mshambuliaji pekee wa kati anayeaminiwa, huku wengine wenye uwezo wa kucheza hapo, Lukas Podolski na Theo Walcott ambao kwa sasa ni majeruhi
wakitakiwa zaidi kucheza kwenye wingi.
Benzema amefunga mabao sita na kutoa pasi zilizozaa mabao moja kwa moja 12 katika Ligi ya Hispania, washabiki wa Real hawampendi, na wamekuwa wakionesha hivyo wazi, kwa hiyo anaweza kupata kimbilio Arsenal atakakokuwa na uhakika wa kucheza vizuri zaidi.
Bendtner (25) ni raia wa Denmark na anachezea timu ya taifa ya nchi hiyo na amekuwa na Arsenal tangu akiwa na umri wa miaka 16 na alipewa nafasi walipopambana na Chelsea kwenye Kombe la Ligi lakini hakuisaidia ipasavyo timu yake zaidi ya kukimbia hapa na pale na mitindo yake mipya ya nywele.
Comments
Loading…