Katibu mkuu mpya wa TFF, Angetile Osiah, anatarajiwa kuripoti leo katika ofisi za shirikisho hilo la soka Tanzania kwa ajili ya kuanza kibarua chake kipya alichokiomba hivi karibuni.
Osiah aliteuliwa na Kamati ya Utendaji ya TFF kushika nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Fredrick Mwakalebela, baada ya kuonekana kuwa na uwezo zaidi ya waombaji wengine wanne waliofika hatua ya fainali ya mchujo.
Hata hivyo, TFF kupitia kwa Rais wake, Leodegar Tenga haikuwa tayari kuwataja waombaji wengine waliojitokeza na kufika hatua hiyo ya tano bora.
Akizungumza na gazeti hili, Osiah alisema kuwa kabla ya kuanza kazi anatarajia kukutana na watendaji wengine wa shirikisho hilo kwa ajili ya kufahamiana na baada ya hapo atakutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kueleza mikakati yake.
Osiah alisema kuwa mara baada ya kuripoti atasaini mkataba wa ajira wa miaka miwili na ana anaamini atakapopata ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka hapa nchini, malengo yaliyopo yatafikiwa.
Siku chache baada ya kutangazwa kuwa katibu mkuu mpya, gazeti hili lilifanya mahojiano na Osiah ambapo alisema kuwa msingi wa kazi zake utakuwa ni kutekeleza kanuni, sheria na maagizo ya mkutano mkuu ambao ndio unaotoa dira na muelekeo sahihi.
Osiah alisema pia atahakikisha katika uongozi wake hapendelei klabu yoyote na zote atazipa haki sawa kama katiba na kanuni husika za mashindano zinavyoeleza.
Aliongeza kuwa katika uongozi wake atafanya kazi bila ya kuyumbishwa na atakuwa na msimamo, jambo analoamini litasaidia kuinua soka la nchini kuanzia klabu hadi taifa.
Mbali na Osiah, Boniface Wambura aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Jambo Leo, naye anatarajiwa kuanza kibarua chake cha Afisa Habari wa shirikisho hilo pamoja na Jimmy Kabwe ambaye ni Mkurugenzi wa Kwanza wa Masoko na Matukio.
Comments
Loading…