Ndiyo maana amekuwa lulu barani Ulaya. Andre Onana Anawashinda Kepa na Mendy kwa uwezo wa kucheza na miguu, kupanga safu…
WAACHENI Chelsea wahangaike kutafuta saini ya golikipa namba moja wa Inter Milan. Wana kila sababu ya kutaka huduma yake. Andre Onana anajiamini. Msimu wa 2022/23 haukuwa mzuri kwa Chelsea. Makocha waliopita wamchemsha, na sasa wamemwajiri Mauricio Pochettino kuwa kocha wao mpya.
Msimu ujao Chelsea itakuwa chini ya kocha aliyewahi kuzinoa Tottenham Hotspurs na PSG. Kikosi cha cha sasa Chelsea kina makipa wawili; Kepa na Mendy. Tatizo la makipa hawa uwezo wao wa kucheza eneo la ulinzi ni mdogo mbele ya Andre Onana.
Nyota huyo wa Kameruni hawanazidi kwa mengi makipa waliopo Chelsea kwa sasa. Tukianza kwa Mendy, ana urefu unatakiwa, anapangua mashuti kadiri anavyojisikia na hakika awapo langoni anatisha. Lakini Mendy hana ubora katika matumizi ya miguu katika mfumo.
Mendy si kipa wa kisasa ambaye anaweza kucheza kwa kutumikia mfumo hasa kwa miguu na kusogea eneo la ulinzi linalokaliwa na beki namba tano. Tatizo la Mendy ndilo analokabiliwa nalo Kepa. Wote wawili hawana uwezo mkubwa wa kulinda lango katika mfumo wa mabeki watatu nyuma.
Katika kikosi cha Simone Inzaghi, mabeki watatu nyuma mbele yao wanakuwa na wachezaji watano huku safu ya ushambuliaji ikiwa na wachezaji watatu. Hii ina maana mfumo wa ulinzi wa Inter Milan unamhitaji golikipa ambaye anasogea eneo la beki wa kati na kuwasaidia walinzi hivyo kuwa mtu wa nne nyuma.
Mfumo huo (3-5-3) unawawezesha wachezaji watano wanaokuwa eneo la kiungo kushambulia na kujilinda katika uwiano mzuri. Wakati wa kushambulia Inter Milan wanatumia 3-5-3, lakini wanapojilinda wanatumia 3-5-2-1, ndiyo maana wakati mwingine Lautaro Martinez alikuwa akionekana eneo la ulinzi la timu yake akitekeleza majukumu ya kuilinda.
Hii ina maana wakati wanapojilinda kwa mfumo wa 3-5-2-1, katika nafasi ya mabeki watatu anaongezeka golikipa wao ambaye anasimama kama ‘Sentafu’ huku akiwa na ujuzi mkubwa wa kucheza kwa miguu. Inasemekana mfumo huo ili kuifunga timu inabidi wapinzani waanze kukabia juu (eneo la hatari la wapinzani wao) kwa nia ya kumsukuma golikipa katika eneo lake ili asiweze kuwasaidia walinzi wa kati kusogea mbele.
Njia hii ndiyo ilimpa umaarufu Manuel Neuer golikipa wa Kijerumani. Ni mifumo ambayo imeondoa mtindo wa zamani wa golikipa kukaa langoni muda wote na kutohusika kwenye maandalizi au mpango wa kusaka magoli.
Kwa mtindo huo pia umewaondoa makipa wengi wa asili ambao wanasubiri kuondoa michomo ya wachezaji wa timu pinzani. Kwa Andre Onana anakupa vitu vingi kwa wakati mmoja. Anao mpira miguu, kwa maana ya anajua kuucheza. Anapanga mashambulizi kwa kutengeneza pasi kuanzia eneo la beki wa kati. Anaweza kupiga pasi ndefu kwenda kwa washambuliaji na kuwafikia walengwa.
Huyu ni kipa ambaye anatoa somo muhimu kwa makipa wa kisasa barani Afrika. Andre Onana ni kipa ambaye anacheza vema eneo la nambari tano. Katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Man City aliongoza safu ya ulinzi kwa utulivu na umahiri mkubwa.
Ndiyo maana amekuwa lulu barani Ulaya. Andre Onana Anawashinda Kepa na Mendy kwa uwezo wa kucheza na miguu, kupanga safu. Kiwango kikubwa alichokionesha kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa ni punje tu ya kile anachokifanya kwenye Ligi Kuu Italia. Anatumikia mifumo kwa uwezo mkubwa. Langoni ametulia, anamudu kupangua krosi na kona. Lakini kubwa zaidi ni mwanzilishi mzuri wa ashambulizi mengi ya Inter Milan.
Hizi taarifa za klabu ya Chelsea kumtaka golikipa huyu ni njema kwao. Andre Onana ataimarisha idara ya makipa kwani kumekuwa na changamoto kadhaa msimu uliomalizika. Pengine ni miongoni mwa makipa weusi ambao wamefanikiwa kuchezea timu kubwa barani Ulaya.
Onana na Mendy ndiyo waliofanikiwa zaidi kuliko makipa wote wa kutoka bara la Afrika kucheza vilabu vikubwa. Lakini tofauti yao ya uchezaji ipo wazi kabisa. Kilichobaki ni wao Chelsea kutimiza nia yao ya dhati ikiwa wanataka kumsajili nyota huyo. Kwa sasa kipa huyu apewe maua yake licha ya Inter Milan kutoshinda taji la Ulaya. Vilevile kocha wa Kameruni Rigobert Song bila shaka amejionea umahiri wake na hivyo atakuwa radhi kusuluhisha mgogoro wao na kumtaka kijana wao arudi nyumbani kutumikia timu ya Taifa. Apewe tu maua yake.
Comments
Loading…