in ,

Ambokile na Kiyombo walifanya vyema kutokwenda Simba na Yanga

Ambokile

Hapana shaka mmepata sifa nyingi, kila mtu anafurahia kutaja uwezo wanu mahiri. Kuna wengine waliwahi kusema kuwa mnajua kutumia miili yenu vizuri, miili mikubwa yenye sifa zote za mwili wa washambuliaji.

Kuna wengine waliwahi kuja na jambo lao wakisema kuwa nyie mna uwezo mkubwa wa kufunga magoli ya mbali kwa mashuti makali. Tena walisindikiza hayo maneno kwa kusema mnafunga magoli ya kiume.
Kipindi mko Tanzania kuna wengi walisema hamstahili kucheza Mbao FC na Mbeya City. Wengi waliwaona mbali, hawakutaka kuwaona katika nchi hii ya Tanzania, macho yao yaliwaona nyie kwenye ligi kubwa nje ya nchi.

Wengi wetu hutazama kufanya vibaya sehemu fulani katika maisha matokeo yake ya kesho yatakuwa mabaya. Ni wachache wanaoamini kuwa afanyae vibaya leo, kesho anaweza akafanya vizuri. Ndiyo maana hata mtu anayefanya vizuri leo hii wengi wetu huiona kesho yake katika sehemu nzuri.

Huwa tunasahu misukosuko kama iliwahi kuletwa duniani. Akili yetu hutiwa upofu na uzuri wa kitu fulani kwa wakati ule na kushindwa kukumbuka kuwa kuna kushuka kwenye maisha.Siyo kila siku waweza kusimama pale pale ulipo kwenye maisha, kuna mabadiliko hutokea iwe hasi au chanya.

Na hii inategemea na wewe unaangalia mbele au unatazama mbele. Hapo ndipo utakuta wengi huachana, mwingine ataenda kulia na mwingine ataenda kushoto. Ndiyo maana kuna wachezaji wengi sana ambao waliwahi kutamba kwa muda mfupi na wakashindwa kuendelezea tambo zao.

Kelele za kuwasifia ziliwadidimiza na wakasahau ni kipi wanachotakiwa kufanya. Usishangae kuona mfungaji mahiri Salim Aiyee kwenye ligi kuu Tanzania bara msimu uliopita wa mwaka 2018/2019 leo hii hana hata goli tano.

Na hii yote ilitokana na yeye kuchanganywa na zile kelele za kumshangalia.Kelele ambazo hakutakiwa kuziamini na kuzipa nafasi kubwa zipite kwenye ngoma ya sikio lake. Maana kelele hizi zilimwaminisha kuwa amefika , na akasahau kuwa ana safari ndefu ya kufika kwenye mafanikio halisi. Mafanikio ambayo hata Said Bahanuzi alipishana nayo.

Mafanikio ya Adidas/Nike kugombania miguu yake ili wauvishe kiatu bora. Mafanikio ya kulipwa kwa wiki pesa ndefu ambayo kwa hapa Tanzania waweza kutumia miaka mingi kuipata. Mafanikio ya kucheza ligi ambazo sisi huziangalia kwenye Televisheni, ligi ambazo zinawachezaji ambao Said Bahanuzi alikuwa anawahusudu kwa kipindi kile.

Wengi wa wachezaji hawakuwahi kufikia mafanikio hayo kwa sababu waliruhusu sifa ziwapeleke kushoto na kuipoteza njia ya kwenda mbele. Kwao ikawa kila walipokuwa wanageuka na kutazama ndiko mbele yao ilipo. Ikawafanya wakose uelekeo sahihi wa kwenda kwa sababu ya kelele za majukwaani. Mwanzoni Habib Kiyombo na Ambokile mliamniwa muende Kariakoo, Ilemela na Mbeya palionekana siyo sehemu yenu . Lengo lao la kuwaomba muende Kariakoo kwa kipindi hicho walitaka kuwafanya muamini kuwa kariakoo inafanana na mji wa Catalunya.

Kariakoo huwaaminisha wachezaji kuwa hawana haja ya kwenda popote pale kwa sababu hujifanya waone wapo kwenye mji bora kisoka kuliko miji yote.Watu wa Kariakoo akili huzifumba na kuona ndiyo sehemu sahihi kuna wakati huzifumba kwa kukuletea wale wasichana wanaotumia dawa za kina Jack Ma kukuza makalio ili mradi uone tofauti ya Ilemela na Kariakoo. Na zile Ofa za bia zitakufanya ulale usiku wa manane na kukusahaurisha kilichokufanya uende Kariakoo. Wengi wakifika Kariakoo huwa wanaona ndiyo wamefika mwisho wa safari yao ya maisha ya kisoka. Hakuna anayetumia Kariakoo kama daraja la kwenda Catalunya.

Ndiyo maana huridhika, hata mazoezi hupungua, kujituma uwanjani huondoka na akili ya mpira hufifia kabisa. Ndoto zile za kucheza Ulaya hupotea ghafla. Hakuna anayewaza kuwa na wasimamizi wao binafsi ambao watawaongoza kukilea na kukikuza kipaji chao.

Hata suala la kuwa na wakala nalo hupotea kwa sababu wengi wao hawaoni haja ya kusogea hatua moja mbele kutoka pale waliposimamia. Umri utazidi kwenda, nguvu za mpira huisha mwilini mwao na uwezo wa kucheza mpira hupungua. Na mwisho wa siku watatupwa kama kopo la chooni na vilabu vya kariakoo bila msaada wowote.

Sisi tutabaki na historia tu ambayo tutatumia kuvielezea vizazi kuwa alikuwepo fulani aliyeng’aa msimu fulani, akaenda timu fulani kwa sababu ya sifa kumlevya kwa sasa hana hata timu fulani.
Kama ambavyo ilivyohadithi ya Bahanuzi na michuano ya Kagame ilivyobadiLisha maisha yake, kutoka mchezaji mwenye njaa kuwa mchezaji aliyeridhika ghafla, ndivyo hivo hofu yangu ilivyokuwa kwa Habib Kiyombo na Eliud Kiyombo kabla hawajaamua kuondoka Mbeya City na Mbao FC.

Leo hii wapo sehemu ambayo kama wakiongeza jitihada zao kwa dhati wanaweza wakafika mbali . Sehemu walizopo ni sehemu ambazo ziko karibu sana na neno mafanikio kwenye mpira wa miguu . Mamelodi Sundowns na TP Mazembe ni sehemu nzuri sana kwa mchezaji kwenda sehemu kubwa na bora kama akiongeza jitihada .

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Kuna haja ya Fei Toto kutopitia njia za Said Ndemla

Tanzania Sports

Wanasoka EPL kukatwa 30%?