Hivi karibuni kumesambaa taarifa za klabu kongwe na yenye mafanikio makubwa katika soka la Sudan ya Al Hilal Omdurman kwamba itahamia kwa mda nchini Tanzania na itashiriki ligi kuu ya soka ya tanzania bara. Taarifa hiyo ilitolewa rasmi kwa umma mnamo tarehe 18 mwezi 3 mwaka 2024 na afisa habari wa shirikisho la soka nchini Tanzania bwana Clifford Ndimbo. Alitoa taarifa kwama klabu hiyo imetuma maombi na maombi yao yamekubaliwa na shirikisho la soka nchini Tanzania. Maamuzi hayo ya kuhamia katika ligi kuu Tanzania yamekuja bila ya shaka baada ya machafuko ya vita kuzidi kushika hatamu na hayaonekani kama yataisha haraka katika kipindi cha hivi karibuni.
Taarifa hii iliibua hisia za mashabiki wengi wa soka kwani waliona kama ni jambo la ajabu na wengui walistaajabu Zaidi pale waliposikia kwamba mechi zao hazitakuwa zinahesabiwa poitni yaani hata kama ukiifunga klabu hiyo hakuna pointi ambazo utakuwa unaongeza na kama wakikifunga nako hakuna utakachokuwa unachokipoteza. Taarifa hizi ziliwashitua wadau wengi wa michezo hususani soka na wengi wakashangaa klabu itashiriki vipi ligi bila ya kuchukuliwa pointi. Lakini kwa wenye kufahamu ukubwa wa klabu hiyo na matatizo ya kisiasa ambayo yapo katika taifa lao hawakushangaa sana na wamefahamu kwamba kutakuwa na faida zifuatazo:
Mosi Klabu hiyo ni mojawapo ya vilabu vikongwe barani Afrika na yenye mashabiki wengi sana. Ni klabu yenye mafanikio makubwa katika soka la nchi ya Sudan. Ni mojawapo ya vilabu vikongwe vya soka barani Afrika. Ilianzishwa mnamo februari 13 mwaka 1930. Al Hilal ndio bingwa wa kihistoria katika mashindano ya ligi ya nchini kwao. Amewahi kushinda mara 29 na amebeba mara 8 kombe la Sudan Cup na amewahi kuwa mshindi namba mbili wa mashindano ya klabu bingwa wa afrika na hiyo ilikuwa kwenye miaka ya 1987 na 1992 na amewaahi kuwa mshindi wa pili kwenye mashindano ya mabingwa wa ligi za waarabu mnamo mwaka 2002. Ligi kuu Tanzania bara itapata fursa ya kushirikisha klabu kongwe na itaweza kuchangamsha vilabu ambavyo vitapata fursa ya kucheza pamoja naye.
Pili klabu hiyo ina mashabiki na wafuatiliaji wengi barani afrika. Hili litasaidia kuendelea kutangaza ligi yetu kwani mashabiki hao wa Al Hilal wataifuatilia ligi ya Tanzania kuona maendeleo ya timu yao na hivyo hata kuifanya nchi pia kuwa inafuatiliwa kutokana na mechi ambazo Al Hilal itakazokuwa inazicheza.
Tatu klabu hiyo iko chini ya meneja ama kocha mashuhuri barani Afrika ambaye ni Florent Ibenge. Wasifu wa Ibenge ni mkubwa sana barani Afrika kwani ni mojawapo ya makocha wa daraja la juu ambao wapo barani Afrika. Kocha huyo ni mzoefu na ameshahiriki mashindano yote makubwa katika bara la afrika na kufika mbali. Amewahi pia kuwa kwenye benchi la ufundi la timu ya taifa la jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ambapo aliisaidia taifa hilo kuweza kufuzu kwenye mashindano ya mataifa huru ya Afrika katika mwaka 2016 kwa wachezaji wa ndani. Alisaidia kushika nafasi ya tatu kwenye mashindano ya Afrika mnamo katika mashindano kama hayo. Mafanikio yake makubwa kimataifa katika ngazi ya klabu yanajulikana Zaidi kuanzia wakati alipokuwa anafundisha klabu ya AS VITA ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo ambapo aliisaidia kushika nafasi ya pili katika kombe la klabu bingwa Afrika mnamo mwaka 2014 aidha alisaidia klabu hiyo kubeba kombe la Congo super cup mnamo mwaka 2015, nafasi ya pili katika kombe la shirikisho Afrika mnamo mwaka 2018. Baada ya kutoka klabu hiyo alihamia klabu ya Rs Berkane ya nchini Moroko ambako nako aliisaidia klabu hiyo kubeba kombe la shirikisho barani Afrika mnamo mwaka 2021 na amewahi kubeba kombe la mfalme wa Moroko mnamo mwaka 2020. Uwepo wa kocha huyo hapa nchini utaongezea uzoefu makocha wazawa ambao wako hapa Tanzania na pia inawezekana ukawapa uwezo wa kujiamini makocha wetu kwamba hata wao wanaweza kwenda nje ya mipaka yao na kufundisha vilabu vikubwa barani Afrika.
Nne klabu hiyo mwaka jana ilishiriki katika mashindano ya African Super League na mwaka huu wanatarajiwa kushiriki mashindano hayo. Kushiriki kwao kwenye mashindano hayo kwa namna moja ama nyingine inawezekana wakachezea mechi zao katika viwanja vya nchini Tanzania kwa hiyo hilo nalo litakuwa ni fursa kwa ligi yetu kuendelea kutangazika katika Nyanja za kimataifa. Kwani mashindano hayo yanafuatiliwa na wadau wengi sana wa michezo duniani na kwa kuwa mashindano hayo yaliletwa barani Afrika ili kuangalia uwezekano wa kuweza kuchezwa katika mabara tofauti hususani barani ulaya basi yamekuwa yana msisimko mkubwa sana ambao umepelekea kuwa na wafuatiliaji wengi sana.
Tano vilabu vyetu vitapata uzoefu wa kucheza mechi na klabu kongwe barani Afrika. Vilabu vyetu vya ligi kuu hususani vile vidogo vimekuwa vina kawaida ya kucheza na timu kubwa barani Afrika ambavyo ni Simba na Yanga peke yake tu kwa kuwa vingi katika vilabu hivyo hushindwa kufuzu kushiriki mashindano ya kimataifa katika ngazi ya vilabu. Hali hii imevipelekea kuwa ni vinyonge na hata baadhi ya vilabu hivyo pindi vikiomba vilabu vikubwa mechi za kirafiki huwa havikubaliwi na hata wakikubaliwa hushindwa kumudu gharama za kukaribisha vilabu hivyo na kuvihudumia pindi wakikubali kuja hapa Tanzania.