Mikel amefanya jambo lililowaacha hoi mashabiki wake.
KAMA kuna kocha aliyekuwa anacheza mwishoni mwa wiki iliyopita basi ni Pep Guardiola wa Manchester City. Akilini mwa Guardiola zipo timu kubwa mbili anazozifuatilia katika Ligi Kuu England. Ni Liverpool na Arsenal. Guardiola anakumbuka alivyohenyeshwa msimu uliopita na Arsenal hadi akatakiwa kusubiri dakika za majeruhi kujihakikishia ubingwa wa EPL.
Bila shaka yoyote msimu huu anawatazama Arsenal kwa faida kubwa mbili; kwanza wanacheza Ligi ya Mabingwa ambako wametoka kuinyuka PSV ya Uholanzi. Pili anawatazama kwa mechi zao za EPL. Kifupi anawasoma, halafu anawasoma tena. Mwishoni mwa wiki timu zote tatu zilikuwa dimbani. Liverpool na Manchester City zote zimeshinda mechi zao.
Guardiola anafahamu kuwa Jurgen Klopp ni kama mbogo aliyejeruhiwa na hivyo anautaka ubingwa wa England kwa usongo mkubwa. Hali kadhalika Mikel Arteta naye ana ghadhabu za kukosa ubingwa msimu uliopita katika mechi za mwisho. Unaweza kusema mchawi wa Arsenal alikuwa William Saliba, maana tangu alipoumia beki huyo kikosi cha Mikel Arteta kilianza kuyumba.
Msimu huu Mikel ameanza kwa kuwaimarisha nyota wake. Anatafuta kiwango bora katika vipaji vya wachezaji wake karibu wote, Gabriel, Kiwior, Nketiah,Nelson, Jesus na wengineo. Langoni ameongeza nyanda mwingine David Raya kusaidiana na Aaron Ramsdale.
Hata hivyo katika mechi ya wikiendi iliyopita Mikel Arteta ameshangaza. Alikuwa kwenye dimba la nyumbani dhidi ya Tottenham Hotspurs. Msimu huu Spurs wamempoteza nyota wao Harry Kane aliyetimkia Bayern Munich, lakini safu yao ya ushambuliaji bado imechangamka ikiongozwa na Hueng Son, Sarr na Richarlson. Kwenye mechi hiyo Mikel amefanya jambo lililowaacha hoi mashabiki wake.
TANZANIASPORTS imchunguza uchezaji wa timu hiyo katika mchezo dhidi ya Spurs na kubaini kuwa palikuwa na makosa katika kubadilisha wachezaji, nafasi ya winga wa kulia bado inahitaji msaidizi,beki wa kulia ina kigugumizi kingi,timu yake ilikatikatika mno katika mchezo mchezo,ari ya wachezaji wake ingalipo,vipaji vya Arsenal ni vizuri na shauku ya ubingwa kwa benchi ya ufundi bado iko imara, licha ya changamoto.
KIUNGO
Kipindi cha pili kocha Mikel alimtoa Declan Rice na nafasi yake ilichukuliwa na Jorginho. Ni kiungo huyo ndiye aliyesababisha Spurs wakasawazisha bao la pili kwa sababu alitaka kuwapiga chenga wachezaji wawili mita chache kutoka eneo la katikati ya dimba. Ufanisi wa Jorginho haukuwa wenye kuridhisha hivyo huenda Mikel alitakiwa kuongeza kiungo mwingine ili kumsaidia Declan Rice kuliko kumtoa. Ikiwa angeongezewa kiungo wa ulinzi maana yake angemsaidia kusogea mbele zaidi kuliko kuirudisha timu nyuma na kumfanya Martin Odegaard arudi zaidi nyuma kusaka mipira. Hilo la kwanza.
Jambo la pili, katika mabadilishano hayo Mikel alimwingiza Kai Harvetz. Huenda kocha alitaka ubunifu zaidi pamoja na kusaidia ulinzi. Lakini chaguo lake halikuwa sahihi. Kai hawezi kutoa mchango unaotarajiwa kwa mechi ngumu kama dhidi ya Spurs.
Katika mahojiano mara kadhaa Mikel amepata kuviambia vyombo vya habari, “Kai anafanya kazi nzuri, ingawa hajafikia kile tunachotaka lakini angalau anaweza kukifanya. Alichokosa sasa hivi kufunga mabao, akishafunga atajiamini tena na kucheza vizuri zaidi,” alisema Mikel alipozungumza na Skysports mwezi uliopita katika utetezi wake wa usajili wa Kai Harvertz. Bado nyota huyo haridhishi wala kuwashinda wachezaji wenye mtiririko na mfumo wa timu hiyo. Hajafikia uhodari wa Trossand ambaye alitumia muda mwingi akiwa benchi. Katika eneo la kiungo ndilo injini ya timu, na Spurs inayo majembe yenye nguvu na kutisha zaidi. Timu yao imeimarika na bila kocha Ange anastahili pongezi. Pengine mechi dhidi ya Arsenal lilikuwa jaribio lao la kwanza lakini wakiwa ugenini walipata pointi moja.
UKAME WA MABAO
Je upo uwezekano washambuliaji wa Arsenal wakafunga mabao 40 msimu huu? Nazungumzia washambuliaji Eddie Nketiah,Gabriel Jesus, Kai Harvetz pamoja na mawinga wao Martinelli, Bukayo Saka, Nelson, na Trossand. Mabao 40 kwa maana angalau mshambuliaji mmoja afikishe mabao 20, kisha 20 mengine wanaweza kugawana nyota wengine. Ikiwa timu inaruhusu mabao ya kufungwa namna ile dhidi ya Spurs, je itakuwa na nafasi gani msimu huu?
Unaweza kusema Ligi bado mbichi, lakini magonjwa yaliyoko lazima yafanyiwe kazi mapema. Ingawa mfumo ndiyo unaobeba nyota wa kisasa lakini wanahitaji mfungaji wa mabao mwenye uwezo wa kufikisha angalau 20 kwa msimu. Ukame wa mabao ukizidi utawarudisha nyuma zaidi katika mbio za ubingwa.
Ukifika hapo ndipo unagundua kuwa Pep Guardiola anazitazama timu hizo kwa makini na anapoona makosa ya kizembe yanafanywa lazima awe anacheka huko aliko. Na pengine atawageukia Liverpool lakini nao wakifanya makosa itakuwa yaleyale.
GOLIKIPA
Hakuna mjadala mkubwa isipokuwa hisia za mashabiki,wachambuzi na wanamichezo. Makipa wote wa Arsenal wana viwango vizuri na wanastahili kukaa langoni kulinda lango la timu hiyo. Raya amemmzidi Ramsdale eneo dogo tu la kucheza kwa miguu. Lakini Ramsdale alikotoka kulikuwa kugumu sana, hata hivyo ameimarisha uwezo wa kucheza kwa miguu.
Isipokuwa Ramsdale huwa hachezi kwa namna ya golikipa-namba tano (huyu ni kipa anayetakiwa kushiriki kuandaa mashambuliaji, ndiyo maana Andre Onana anaweza kupanda hadi Yadi 26 toka langoni. Kwenye mchezo dhidi ya Spurs, Raya naye anafanya majaribio hayo. Golikipa wa Spurs naye anafanya majaribio hayo.
Makipa wote si wale wa zama za akina Nelson Dida, Fabian Barthez, Tony Sylva, Hans Vonk, au David De Gea. Wengi wanabadilika kutokana na mapokeo ya sasa. Kinachotokea Arsenal ni kwamba kocha anahitaji timu imara na yenye ushindani. Eneo la golikipa nalo lilihitaji ushindani. Amefanikiwa. Labda arekebishe kwingine kwenye uamuzi wa kufanya mabadiliko wakati mchezo unapoendelea.
Comments
Loading…