Usiku wa jana kulikuwa na hafla ya utoaji tunzo za soka ambazo
ziliandaliwa na shirikisho la soka duniani FIFA.
Hafla ambayo iliwakutanisha watu mbalimbali, tena miamba migumu
iliyotengeneza historia iliyotukuka katika ulimwengu wa soka.
Historia ambayo haiwezi kufutika zaidi ya kutumika kama kumbukumbu kwa
vizazi na vizazi.
Historia ambayo inawapa heshima wao kwa sababu wao walianza kuupa
heshima mpira wa mguu.
Waliuheshimu, wakautukuza na wakaishi ndani ya mpira na kuota
mafanikio yao makubwa yatakuwa ndani ya mpira.
Ndiyo maana historia itamkumbuka Pele ambaye jana ilikuwa siku yake ya
kuzaliwa kama moja ya wachezaji bora kuwahi kutokea dunia.
Hii yote ni kwa sababu Pele alipigana vya kutosha miaka ya 1960
kuhakikisha dunia itakuja kumkumbuka kama mmoja wa wachezaji bora
katika dunia.
Alitumia muda wake kuhakikisha kuwa ipo siku moja dunia itamwandika
kwa wino wenye bashasha la tabasamu, na siyo wenu wenye bashasha la
huzuni.
Hakutaka kuruhusu neno kushindwa liwe katika mwisho wa kitabu chake
cha historia, alihakikisha kuwa ushindi ndiyo neno pekee linalotakiwa
lionekane kwenye kurasa ya mwisho ya kitabu chake.
Hiki ndicho ambacho alitaka kukiacha kwenye kizazi cha milele, milele
atakumbukwa.
Nilitabasamu sana na kufurahia baada ya kuwaona Maradona na Ronaldo De
Lima wakienda kutoa tunzo ya mchezaji bora dunia wa kiume.
Macho yangu yalifurahia kuwaona kwa sababu akili yangu iliruhusu
kumbukumbu zangu zirudi nyuma.
Kumbukumbu ambazo kwa asilimia kubwa zilikuwa zinaelezea mafanikio
makubwa ya kukumbukwa ya hawa magwiji wawili.
Mafanikio ambayo waliyapata na kuyaacha kama kumbukumbu kwa kila kizazi.
Historia inamtambua Maradona kama mchezaji bora wa dunia kuwahi
kutokea baada ya Pele, historia hiyo hiyo inasema Ronaldo De Lima ni
mshambuliaji bora wa kati kuwahi kutokea.
Historia imewafanya kuwa nguzo imara kwa sababu wao walijenga msingi
mzuri wa historia yao wakati wanacheza.
Wachezaji wawili wenye medali ya kombe la dunia walikuwa wanamkabidhi
mchezaji bora wa dunia wa mwaka 2017 ambaye hana medali ya kombe la
dunia.
Mchezaji ambaye ana mafanikio makubwa uwanjani kwa sababu ya jitihada zake.
Jitihada zake zimemfanya awe na mafaniko makubwa na jitihada zake pia
zinamtengenezea mazingira mazuri ya yeye kuandikwa kwenye vitabu vya
historia kwa wino wa tabasamu.
Ni mchezaji ambaye amezaliwa katika mazingira magumu, lakini alikuwa na maono.
Maono yake makubwa yalikuwa kuja kuwa mtu mwenye mafanikio makubwa
duniani kwa kutumia kipaji chake.
Alikiamini kipaji chake na kuamini ipo siku moja dunia itamkunbuka kwa
mazuri kwa sababu ya kipaji chake
Wakati akiwa mtoto mdogo, Cristiano Ronaldo aliwahi kumuonesha baba
yake hotel kubwa nchini Ureno nakumwahidi kuwa ipo siku angemjenge a
Hotel kubwa kama hiyo.
Miaka mingi imepita leo hii Cristiano Ronaldo ana hotel zake kubwa
Ureno na Marekani.
Ndoto yake kaipita kwa sababu aliishi ndani ya maono yake.
Alikiamini kipaji chake na kuamini ipo siku moja atapata mafanikio
makubwa kupitia kipaji chake.
Jana wakati anaulizwa siri ya mafanikio yake alisema kitu kimoja ”
Talent without working is nothing”.
Kipaji bila kukifanyia kazi ni kazi bure, unatakiwa uhakikishe
unakifanyia kazi kipaji chako kwa manufaa yako binafsi.
Unapokuwa na kipaji unatakiwa utamani uwe mkubwa kila siku.
Jua la leo likitoka, unatakiwa litoke katika hali ya utofauti na wa jua la jana.
Kila siku unatakiwa uwe mkubwa kuliko jana.
Usiendelee kuishi katika mfumo wa jana ambao umekufanya udumae kila uchwao.
Inauma unapoona kipaji hakipigi hatua ya mafanikio na muda unaenda.
Haina ubishi Ajib ana kipaji kikubwa sana, kipaji ambacho hakistahili
kuendelea kuvaa jezi ya Yanga.
Ni dhambi kubwa kwa Ajib kuendelea kuwepo katika ardhi ya Tanzania.
Historia ya mpira itamwandika kama Ngassa .
Mwisho wa kitabu chake kutakuwa na maneno ya huzuni kama kitabu cha Ngasa.
Kuna haja ya Ajib kutamani kitabu chake kiwe na kurasa ya mwisho
chenye maneno ya ushindi.
Naamini anaweza akabadilisha historia, na kizazi kijacho kikamsoma
kama mchezaji bora kuwahi kutokea nchini kutokana na mafanikio yake
ambayo anatakiwa kuyapata nje ya ardhi ya Tanzania.