Huwaelezi chochote washabiki wa soka barani Afrika juu ya Ligi Kuu ya England (EPL) kwa jinsi wanavyoipenda na kujifungamanisha nayo.
Utawasikia katika pande mbalimbali za bara hilo wakisema; “leo tutawamaliza…leo tunapumzika tutacheza kesho…poleni, jana mlikwisha mapema.” Hapo unaweza kufikiria wanazungumzia Gor Mahia na AFC Leopards au Simba na Yanga.
Kumbe wanazungumzia klabu ‘zao’ kwa maana ya Chelsea au Manchester City; Arsenal au Manchester United, na pia wapo pia washabiki wa klabu ambazo huwa katikati ya jedwali la msimamo wa ligi kama Stoke, Tottenham au Everton.
Wakati ligi hii iliyoanza msimu mpya Jumamosi iliyopita inafuatiliwa kwa karibu na watu zaidi ya bilioni moja duniani, kutoka Afrika ni watu zaidi ya milioni 260, bila kujali hali zao za uchumi, ambapo kama hawana viunganishi, basi watakwenda kwenye mabanda yanayoonesha, ambako hulipa kiingilio au walau kupata kinywaji kama kiingilio kisicho rasmi.
Katika msimu huu, tayari tambo zimeanza, baadhi wakiwazodoa wenzao kwamba walipata bao la ‘mkono’, kwamba wengine pre-season ya kuzoa mataji matatu ilikuwa ‘cha mtoto’ na wengine wakijisifu kwa ushindi mkubwa kwenye mechi ya kwanza.
Kuanzia Cairo, kule kaskazini mwa Afrika hadi Cape Town, Afrika Kusini, washabiki wanafuatilia kwa karibu, ambapo Ijumaa hii mzunguko wa pili unaanza. Si rahisi kusema moja kwa moja ni timu gani ya England inapendwa zaidi, kwa sababu ya ugumu wa kujumlisha wote kwa kutumia akaunti zao wanapotuma salamu za kutakia klabu heri na pia huwezi kuwahesabu kwa vichwa vyao huko waliko.
Afrika Mashariki wengi ni Arsenal, na chaguo la rangi zao ni nyekundu, wakikumbuka zaidi Arsenal ile iliyoitwa ‘Invincibles’ iliyomaliza msimu wa 2003/4 pasipo kupoteza hata mechi moja na walikuwa chini ya Mfaransa huyu huyu, Arsene Wenger.
Arsenal wamekuwa na wachezaji wazuri kutoka Afrika, hata kama si Mashariki, wakiwamo Nwankwo Kanu, Emmanuel Adebayor, Kolo Toure na Lauren ambapo washabiki walipoangalia rangi zao wakaona ni wao. Kanu pia aliwafanya Wanigeria wengi kuipenda Arsenal.
Inashangaza jinsi watu wa Afrika Mashariki walivyoipenda klabu hii au kuwa na mvuto mkubwa na EPL kwa ujumla, wakati mchezaji pekee anayecheza humo ni yule wa Southampton, Victor Wanyama.
Ni rahisi kuona kwamba kwa Afrika Magharibi, watu wengi wanashabikia Chelsea, mabingwa watetezi. Haijulikani kianuai sababu yake, lakini najua kwamba huko wametoka wachezaji muhimu wa Chelsea.
Huwezi kuizungumzia EPL, na kwa namna ya pekee, Chelsea, bila kuwataja akina Didier Drogba, Solomon Kalou, Samuel Eto’o, Victor Moses, Michael Essien na John Mikel Obi, wote wakitoka Afrika Magharibi na walipata au wanachezea Chelsea.
Drogba yupo juu zaidi, licha ya kwamba alishaondoka Chelsea, kwa sababu ya mafanikio aliyowaletea timu; ni Mwafrika wa kwanza kufunga mabao 100 EPL, lakini ndiye aliyetia bao lililowapa Chelsea ubingwa wa kwanza wa Ulaya, nayo ilikuwa 2012.
Anaheshimika sana nyumbani kwake, Ivory Coast, akiwa ni balozi wa amani na alishiriki kwa kiasi kikubw akuirejesha nchi ilivyo, baada ya machafuko ya 2010/11 yaliyotokana na wizi wa kura. Ameanzisha wakfu ya kusaidia watu katika elimu na afya nchini mwake.
Upande wa kusini mwa Afrika kuna washabiki wengi wa Manchester United, klabu yenye mafanikio makubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa EPL, wakiwa wametwaa ubingwa mara 13 kwa ujumla wake tangu 1992.
Walimsajili mmoja wa wachezaji wazuri zaidi wa Afrika Kusini, Quinton Fortune aliyewachezea kwa miaka saba. Kadhalika huyu ni mmoja wa wachezaji wa zamani wa Man U wanaosafiri kurudi Kusini mwa Afrika kama mabalozi wa chapa za United kila mwaka. Afrika Kusini ni nchi ya kwanza kuwa na Klabu ya Washabiki wa Manchester United iliyosajiliwa rasmi.
Kaskazini mwa Afrika nako wanawapenda Arsenal na The Gunners wana uwakilishi mkubwa kwenye mataifa ya Morocco, Algeria na Tunisia.kuna klabu zenye nguvu sana za washabiki wa Arsenal huko zinazosaidia kuikuza Arsenal kwa kila hali, kupitia matukio mbalimbali, kama lile la kila mwaka linaloitwa ‘Be a Gunner. Be a Runner’.
Hata hivyo, nchini Misri Chelsea wana mizizi huko na labda kama shukurani kwao ndiyo maana wakamchukua Mohamed Salah Januari mwaka jana, japokuwa amekuwa akicheza kwa mkopo kwingineko.