*Sare zaendelea, Gabon wachapwa
WAKATI sare zikitawala mechi tatu za katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), washabiki wamekabiliana na polisi kabla ya mechi baina ya wenyeji Guinea ya Ikweta na Burkina Faso.
Wakitaka kushabikia timu yao ya nyumbani, mamia ya washabiki walitaka kulazimisha kuingia uwanjani, huku wengine wakiwa hawana tiketi, baada ya kuzuiwa baadhi wakaanza kurusha mawe na polisi wakajibu kwa kufyatua mabomu ya kutoza machozi kwenye Uwanja wa Bata.
Polisi wamekuwa wakimiminika kwenye viwanja kwa ajili ya kuhakikisha usalama kwenye michuano hii, ambapo washabiki wamekuwa wakicheleweshwa kuingia uwanjani, ambapo hutokea kiwanja kimoja kikawa na mechi mbili zinazofuatana.
Polisi wa kutuliza ghasia pia walilazimika kutumia ngumu kudhibiti wafuasi kwenye jiji la Ebebiyin katika mechi za kwanza. Guinea wanaandaa michuano hii kwa notisi ya dharura baada ya Morocco kuchelea kuandaa kwa hofu ya maradhi ya Ebola yaliyozikumba nchi za Liberia na Sierra Leone na kuua maelfu ya watu.
Katika mechi za Jumatano hii, Guinea ya Ikweta walikwenda suluhu na Burkina Faso, ikiwa ni sare ya pili kwa wenyeji huku Wabukinabe wakiwa wameambulia pointi moja katika mechi mbili.
Kwenye mechi nyingine Kongo Brazzaville waliwafunga Gabon bao 1-0, Ivory Coast wakatoshana nguvu 1-1 na Guinea Bissau huku Mali nao wakitoka nguvu sawa na Cameroon kwenye mechi za Jumanne.
Alhamisi hii Zambia wanacheza na Tunisia huku Visiwa vya Cape Verde wakicheza na Kongo Kinshasa.