Zimesalia siku mbili pekee kuelekea kuanza kwa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017) itakayoanza kutimua vumbi Jumamosi hii ya Januari 14. Wenyeji Gabon walio kwenye Kundi A watafungua michuano hiyo dhidi ya Guinea-Bissau ndani ya dimba la Stade d’Angondje siku hiyo Jumamosi. Timu nyingine za kundi hilo ni Burkina Faso na Cameroon.
Algeria wenye kikosi kinachojumuisha nyota kadhaa wakubwa akiwemo mwanasoka bora wa Afrika, Riyad Mahrez wamo kwenye Kundi B pamoja na Tunisia, Zimbabwe na Senegal wanaokamata nafasi ya kwanza kwa timu za Afrika kwenye viwango vya FIFA vya hivi karibuni.
Kundi C linaundwa na mabingwa watetezi Ivory Coast wakihitaji kucheza michezo mitatu migumu dhidi ya Togo, Congo DRC na Moroco kutafuta nafasi ya kutinga robo fainali kwa mara ya saba mfululizo.
Misri ambao ni vinara wa mataji ya michuano hii wakiwa wamenyakua jumla ya mataji 7 wamo kwenye Kundi D pamoja na Ghana, Mali na Uganda ambao ni wawakilishi pekee wa ukanda wa Afrika ya Mashariki.
Mabingwa watetezi Ivory Coast ndio wanaopewa nafasi zaidi ya kuibuka washindi wa michuano hii. Kikosi chao kinamjumuisha Wilfried Zaha aliyeamua kuiacha England na kuichagua Ivory Coast.
Nyota wengine tishio waliomo kwenye kikosi hicho cha mwalimu Michel Dussuyer ni pamoja walinzi Serge Aurier anayekipiga kwenye kikosi cha mabingwa wa Ufaransa, PSG na Eric Bailly wa Manchester United ya England pamoja na mshambuliaji Wilfried Bony wa Stoke City ya England pia.
Ushindi walioupata kwenye mchezo wa kirafiki Jumapili iliyopita dhidi ya Sweden umewafanya waonekane imara zaidi. Kutokuwepo kwa nahodha wao wa zamani Yaya Toure aliyestaafu hakuonekani kupunguza makali ya mabingwa hao watetezi.
Hata hivyo vipo vikosi vingine imara vinavyotarajiwa kuleta upinzani mkali dhidi ya Ivory Coast kuelekea dhamira yao ya kutetea ubingwa wa Afrika. Senegal, Algeria na Ghana ni baadhi ya vikosi hivyo.
Senegal ndio wanaoonekana kuwa imara zaidi. Upo uwezekano mkubwa wa wao pia kunyakua taji hilo. Timu hii inayonolewa na mwalimu Aliou Cisse inashikilia nafasi ya 33 kwenye viwango vya FIFA na namba moja kwa Afrika ikiwaburuza Ivory Coast na wengine.
Wao ndio timu pekee iliyoshinda michezo yake yote kwenye michuano ya kufuzu. Uwepo mshambuliaji hatari, Sadio Mane wa Liverpool ni faida kubwa mno kwa Simba hao wa Teranga. Viungo wawili mahiri, Cheikhou Kouyate na Idrissa Gueye wanaweza kukamata vichwa vya habari baada ya kila mchezo.
Senegal watatupa karata yao ya kwanza kwenye mchezo dhidi ya Tunisia wanaoshikilia nafasi ya 3 kwa ubora Afrika. Mchezo huo unaotazamiwa kuwa mgumu utapigwa ndani ya uwanja wa Franceville Jumapili, January 15.
Ingawa Senegal hawakuwahi kutwaa taji la michuano hii na wamo kwenye kundi gumu, lakini huenda sasa zamu yao imefika. Wao ndio tishio kubwa zaidi kwa mabingwa watetezi Ivory Coast. Huenda ni wao watakaowavua taji.