HAKUNA lugha nzuri unayoweza kusema wakati bao la pili lilipofungwa na winga hatari wa Simba, Kibu Dennis zaidi ya kusema βheshima kwa nchiβ. Simba waliingia katika uwanja wa Taifa wakiwa na jambo moja tu la kutafuta pointi tatu. Hata hivyo SC Sfaxien wameadhibiwa kutokana na nidhamu mbovu ya kuchelewesha mpira. Katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam kulikuwa na matukio kadha andani na nje ya kiwanja.Β
Tathmini ya TANZANIASPORTS inaonesha kuwa kucheza dhidi ya timu kongwe na yenye mafanikio kama SC Sfaxien unahitaji mbinu nyingi kuishinda kuanzia uzoefu wa mashindano, historia na mifumo ya soka. Unapozungumzia timu mahiri na zenye historia barani Afrika basi moja kwa moja unaitaja SC Sfaxien sambamba na ndugu zao Esperance na Club Africain za Tunisia. Uzito wa timu hiyo ndiyo uliwapa nafasi Simba kujaribu kile walichokiweza na kufanikiwa kuibuka na ushindi.
Refa amewaadhibu Sfacien
Kuchelewesha mpira, kupoteza muda, kuanguka anguka na kusingizia kuumia, kulalamikia maamuzi au faulo ni miongoni mwa sababu ambazo zilimfanya refa kuongeza dakika 7 za mchezo. Katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2022 nchini Qatar, pamoja na mambo mengine Kamati ya waamuzi ilifika hatua yakuongeza dakika 10 kwa kila mchezo ili kufidia muda wa kushangilia mabao,matibabu na wachezaji kupoteza muda. Kwenye jopo lile liliongozwa na mwamuzi mahiri na maarufu duniani, Piereluigi Collina raia wa Italia, kwamba muda wa nyongeza ni adhabu kwa timu zinazopoteza muda hivyo kila mwamuzi alitakiwa kufidia dakika 10.
Kimahesabu timu nyingi hucheza mechi kwa dakika 70 za mchezo huku 20 zinazosalia zinaambatana na matatizo mengi ikiwemo kupoteza muda,kushangilia,ugomvi,mpira wa kurusha au kona. Kwhaiyo mwamuzi wa mchezo kati ya Simba na Sfaxien ametumia muda wa nyongeza kama adhabu kwa wageni ambao walipoteza muda mwingi. Hata pale alipooneshwa ishara na wachezaji wa Sfaxien kuwa muda umekwisha, lakini mwamuzi aliashiria kukataa na kuagiza mpira wa βgolikikiβ utengwe na kupigwa kueleka langoni mwa Simba.
Katika fursa hiyo Simba walipanga shambulizi lao vizuri kutoka kiungo wa kati kwenda kulia, kisha wakasogea eneo la 18 na kuachia krosi maridadi iliyokwenda kutua kichwani mwa Kibu Dennis na kutinga kimyani. Kiufundi kulikuwa na wachezaji wanne wa Simba waliojipanga kwenye mstari wa 18 wakisubiri pasi. Lilikuwa shambulizi ambalo Sfaxien walitaka kuokoa bila kuangalia jinsi Simba walivyojipanga. Kisha mpira ukatinga wavuni na mwamuzi sekunde chache baadaye akaashiria mpira umemalizika. Tabia za kupoteza muda,kulalamikia waamuzi,kuanguka kudai matibabu na udanganyifu mwingine ni miongoni mwa mienendo ya timu za Kiarabu. Kwa matendo yao mwamuzi kwa kutumia kanuni ya Collina amewaadhibu kwa dakika 3 za ziada hivyo wakaishia kulalamika.
Bao la mapema
Lilikuwa bao lenye kila dalilia kushtua mashabiki na wadau wa soka kwnai lilitokana na makosa binafsi ya beki imara wa kati Che Malone. Beki huyo alikuwa kwenye jitihada za kutoa pasi kwenda kwa golikipa wake Mousa Camara lakini alitumia nguvu kidogo hivyo mpira ukawahiwa na mshambuliaji wa Sfaxien. Bao la kwanza lwa Sfaxien linaonesha namna timu hiyo ilivyo na uzoefu wa mashindano kama haya. Kuhitimisha ni kwamba lilikuwa kushtukiza ambalo lilifungwa na mshambuliaji aliyekuwa akichezeshwa peke yake eneo la ushambuliaji kutokana na timu yake kucheza kwa kujihami kwa muda wote wa dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Karata ya Fadlu Davids
Kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, lazima pongezi ziende kwa kocha wa Simba, Fadlu David. Kwanini? Katika eneo la kiungo aliwapanga wachezaji wawili kucheza jukumu moja; Kibu Deenis na Awesu Awesu. Wachezaji wawili hawa walikuwa na kazi ya kusaidia ulinzi na kushambuliaji. Walicheza kwa kubadilishana mara kwa mara, na walisogea eneo la nambari 8 kwa ustadi. Kibu Dennjis alikuwa katika mfumo wa βfree roleβ, mara nyingi alirudi kama kiungo kufuata mipira kwa mabeki, kisha alipandisha nao kwa kushirikiana na Awesu.
Wakati Awesu alikuwa na jukumu la kukaba na kushambuliaji kutoka nyuma-katikati kwenda kushoto wake, kwa upande wake Kibu Deenis alikuwa anashambuliaji kupitia katikati au kuelekea kushoto. Katika mfumo huu Fadlu Davids alihitaji wachezaji wenye ubunifu na kuapngua ngome ya walinzi wa SC Sfaxien. Hakukuwa na namna nyingine zaidi ya kuwapangua kwani waliwafahamu watacheza mchezo wa kujihami. Kwa mpango huo Fadlu Davids alipewa matunda kwa Kibu Dennis kusawazisha bao muda mfupi tangu walipotanguliwa kufungwa. Kwa kumpanga βfree roleβ inaonesha kwa mara nyingine Fadlu Davids anakua kimbinu, anajiendeleza na kuonesha umahiri wake kama walivyokuwa wazawa wenzake wa Afrika kusini akina Trott Moloto na Rulani Mokwena. Eneo la katikati ya dimba wachezaji wanne walikuwa na kazi ya kuhakikisha Sfaxien wanarudishwa nyuma na kumpa nafasi kiungo mkabaji Fabrice Ngoma.
Maamuzi magumu
Kila kocha ana mambo ya kushangaza. Fadlu Davids amekuja na uamuzi mgumu kwanza kwa kuhakikisha Kibu Dennis hachezi nafasi iliyozoeleka siku zote; ushambuliaji na winga. Katika mchezo dhidi ya Sfaxien, Kibu Dennis alichezeshwa kwa kiungo mchezeshaji akishirikiana na Awesu ambaye hajapata nafasi ya kucheza michezo ya Kimataifa.
Kumpanga Awesu, Fabrice Ngoma na Fernandez ulikuwa uamuzi mgumu ambao ulimweka benchi Yusuf Kagoma katika eneo la kiungo wa ulinzi. Eneo la kiungo lilikuwa na wachezaji wanne huku mbele yao kukiwa na Leonel Ateba na Jean Ahoua. Uamuzi mgumu ni kumwanzisha Awesu na kumwondoa Joshu Mutale katika kikosi cha kwanza. Kipindi cha pili kocha alionesha tofauti nyingine ya aina yake baada ya kubadilisha mfumo na kumpeleka Kibu Dennis katika nafasi yake ya winga wa kulia, kisha akamtoa Leonel Ateba na kumpa nafasi Steven Mukwala. Mabadiliko hayo yalionesha Fadlu anahitaji huduma za washambuliuaji wake katika mechi moja na katika mifumo tofauti. Mfumo awali ulimpa uhuru Kibu Dennis lakini kipindi cha pili ukapelekwa kwa eneo la kiungo wa ushambuliaji.
Uzoefu wa mashindano
Fadlu Davids amewahi kuwa kocha msaidizi katika klabu ya Raja Casablanca, kwhaiyo anafahamu uchezaji w atimu nyingi za kutoka afrika kaskazini. Simba hawakuwa wakipaniki kila walipoteza mpira lakini walionesha kutokimbizana na kwa kasi. Mechi za awali kocha huyo alipendelea soka la kasi, lakini kwenye mechi mbili za makundi amecheza soka la kutuliza timu na kupiga pasi kuanzia nyuma kwenda mbele. Kipindi cha pili aliwapa majukumu yao mabeki wake wa pembeni na kuisaidia z aidi timu. Uzoefu wake kukabiliana na utamaduni wa timu za kirabau ulimsaidia kwani wachezaji wa Simba hawakutaka kupoteza muda kila walipoipata pigo la adhabu ndogo au mpira kutoka nje ya uwanja.
Sfaxien na darasa la kifundi kwa Simba
Kipindi cha kwanza walicheza kama vile hawataki bao. Walijihamia kuanzia dakika ya kwanza, wakitumia mfumo wa 5-4-1 ambao mabeki watano nyuma, viungo wanne na mshambuliaji mmoja. βWakapaki Bus laoβ kwa muda wote wa dakika 45 licha ya kutangulia kufunga. Kipindi cha pilikuanzia dakika 60 wakafanya mabadiliko ya kusogeza wachezaji wanne kwenye mstari wa katikati ya dimba ili kuwazuia viungo wa Simba, kisha eneo la kushambulia wakaweka wachezaji watatu; mmoja kati na wawili pembeni. Uchezaji huo uliwasaidia kupokonya mipira mara nyingi na kuongeza tishio langoni mwa Simba. Shinikizo la mbinu hizo liliwafanya Simba wawe wanashindwa kupanda mbele zaidi, hivyo mabeki wao wakabaki nyuma zaidi hadi pale kocha wao alipofanya mabadiliko. Kimsingi mbinu hiyo imeonesha kwamba Simba wana tatizo la kupoteza pasi kirahisi sana, jambo ambalo linaweza kuleta madhara langoni mwao.
Changamoto ya Simba
Katika mfumo wowote wa kuwatumia mawinga wake, kocha Fadlu Davids anakabiliwa na kibarua kigumu kuthibitisha uamuzi wake wa kumchagua Joshua Mutale kama winga namba mbili baada ya Kibu Dennis. Pale benchi alikuwa na Valentin Nouma. Ladaki Chasambi na Joshua Mutale. Badala yake akawaingiza Mutale na Nouma huku Chasambi akisugua benchi.
Tatizo ni kwamba Joshua Mutale bado hajachangamka kuonesha umahiri uliosababisha Simba wahitaji huduma yake. Pengine mbinu za mwalimu zinambana lakini hata katika uhuru wa kucheza soka bado amekuwa si tishio dhidi ya wapinzani. Kuingia Joshua Mutale maana yake kocha alikuwa amebadili mbinu kuondoa kutegemea viungo na kuhamishia mpira pembeni. Kama kuna jambo wanatakiwa kulifanya ni hili la kumsaidia Joshua Mutale ili kuwa mchezaji hatari. Changamoto ya pili ni kocha kuchelewa kufanya uamuzi dhidi ya Che Malone, beki huyo tayari alishakosea hivyo hakuwa timamu mchezoni na hivyo wapinzani wao waligundua mwanya wa kutumia ni kupitia kwake.
Comments
Loading…