in

Adele alikuwa sahihi kuwapuuza Bob Geldof na Band Aid

HUWA nashangazwa yanapokuja masuala ya taasisi au wakfu zinazotoa misaada, ambapo imekuwa kawaida kwa matajiri na watu mashuhuri kujitolea muda wao lakini sisi wengine tunashinikizwa kutoa fedha.

Kuna kundi linalojumuisha wanamuziki na wasanii wa Uingereza na Ireland linalokwenda kwa jina la Band Aid, wenyewe wakiliita super group, lililoanzishwa na Bob Geldof na Midge Ure kwa ajili ya kukusanya fedha za kupambana na umasikini. Lilitoa wimbo uitwao ‘ Do They Know It’s Christmas?’ kwa ajili ya soko la Noeli nchini Ethiopia.

Natatizwa sana na ‘single’ ya Band Aid na sijui nianzie wapi, lakini lazima tuanze ili tuendelee. Kwanza theluthi ya wahusika kwenye kundi hilo hawajulikani kwa yeyote mwenye umri wa miaka zaidi ya 30.

Niliona kwenye picha alikuwapo msanii Bono ambaye ni kana kwamba angefurahi zaidi kuwa sehemu nyingine kuliko pale chini ya Vloga wa mtandao wa You Tube, Zoella na kushoto kidogo mwa Olly Murs aliyepata kushindwa kwenye mashindano ya vipaji ya The X Factor.

Hiyo si shida sana, pengine ni ishara ya jinsi nilivyo mbali na utamaduni husika, maana hata nilipoangalia kwenye picha hiyo nikajisemea, ‘ala, hii picha ni kana kwamba ni ya watoto wa shule ya siku wasiyovaa sare!’, kisha nikahisi unafuu kwa jinsi One Direction walivyojaribu kuwafanya bibi vizee vionekane vidogo tangu 2010.

Ukweli ni kwamba tatizo langu ni kwa Geldof kumshutumu msanii na mwanamuziki wa Uingereza, Adele Laurie Blue Adkins, maarufu zaidi kwa jina la Adele kwa kutoshiriki kwenye traki waliyotoa karibuni.
adele

Eti anasema; “Hakuna kitu Adele anachofanya, hapokei simu…haandiki. Hajihusishi katika kurekodi, hataki kusikiliza yeyote, hata kwa meneja wake hapokei simu. Analea familia yake naona.”

Naona kwamba Geldof anaonesha kiburi na kujisifu kama wimbo wenyewe ulivyo – je, Waafrika wanajua kwamba Krismasi imewadia? Ukweli kwamba zaidi ya watu milioni 500 wanaoishi pale ni Wakristu, lazima tuchukulie kwamba jibu la swali hilo ni ‘ndio’. Mbaya zaidi ni aina ya uonevu au vitisho wanavyotoa huku wakijifunika kwa joho la wasamaria wema.

Ujumbe uliopo ni wazi na kwa sauti kubwa, hata kama muziki hautoi maana hiyo; kwamba eti Geldof yupo kwa ajili ya kuwaokoa watu wa Afrika Magharibi dhidi ya Ebola, huku Adele, mwenye mtoto mdogo, asiyependa umaarufu hataki kuiteka hadhira, anaoneshwa kwamba ni mwanamke mdogo na mbinafsi ambaye lazima afedheheshwe hadharani.

Licha ya majigambo yote hayo ya Geldof, tumekuja kupata habari kwamba Adele alitoa mchango wake kuwasaidia Afrika Magharibi kupitia Oxfam, kimya kimya bila kujidai wala kujitangaza. Kwa kuangalia juu juu sisi watu wa kawaida na wale fukara wanadhani kwamba watu hawa maarufu wametoa fedha kumbe wapi, na wengine wengi watatekwa na maneno ya Geldof, kwamba eti Adele aliyetoa kimya kimya, hajafanya kitu.

Ukweli ni kwamba matajiri na watu maarufu wanachofanya ni kutoa muda wao ili watukuzwe na kusherehekewa na watu wa kawaida, kupongezwa kana kwamba kabla ya kuandaa video ya wimbo husika huku wakicheka, hatukufahamu juu ya tatizo la Ebola au kwamba maelfu ya watu wa Afrika Magharibi walikuwa katika siku zao za mwisho kwa mateso makubwa kutokana na ugonjwa huo, wakitokwa damu bila kupata fursa ya kufarijiwa na wanafamilia na marafiki.

“Tupeni fedha zenu hizo …” ndiyo maana ya ujumbe wa Geldof tangu mwnazo, na sasa anasisitiza kwamba mtatakiwa kukwangua zaidi fedha mlizopata kwa shida, kwa sababu watu maarufu hutengeneza mamilioni ya fedha kwa kuimba na kutoa saa chache wikiendi kwa ajili ya kuburudisha kwa jina la ‘matatizo’ nasi tutoe viingilio.

“Kwa hakika hatuwezi kusitisha hili…majanga haya yanatisha,” nilimsikia Geldof akisema kwenye kipindi cha ‘BBC Breakfast’ majuzi, lakini ajabu ni kwamba hakuzungumzia kamati ya dharura ya maafa, ambayo imeshakusanya pauni milioni 20 kwa ajili ya eneo husika. Hakuzungumzia hata matabibu wasio na mipaka ambao wapo huko Afrika Magharibi tangu Machi.

Kwa hali ilivyo hata wanajeshi waliopelekwa Sierra Leone kusaidia zahma hii ya Ebola wanaonekana kama hawafanyi kitu bali sifa na heshima vinakwenda kwa Geldof na ‘jeshi’ lake la watu maarufu kwa sababu ya kuimba tu. Hawa na wenzake wanaweza kuwa na fikara kwamba nguo maalumu wanazovaa madaktari na wahudumu kule Afrika Magharibi ni mtindo mpya tu katika ulimwengu wa sanaa na muziki.

Hali hii inaniumiza kwa sababu ukweli unapotoshwa, na inanikumbusha kile Noel Gallagher alichosema miaka tisa iliyopita:
“Nisahihisheni ikiwa nimekosea, lakini wanadhani kwamba mmoja wa jamaa hawa kutoka G8 aliye kwenye mapumziko ya haraka ya chai kwa robo saa hapo Gleneagles (hoteli ya kifahari iliyoko Uskochi) anayemwona Annie Lennox (mwanamuziki na manaharakati wa kisiasa wa Uskochi) akiimba wimbo wake ‘Sweet Dreams’, kisha atafakari na kusema; ‘ha, nadhani ana ujumbe murua hapo,…kwa kweli tunatakiwa tuwapunguzie deni hili’. Hakuna kitu kama hicho kitatokea, au siyo?”

Ya G8 ndiyo hayo hayo ya Geldof, ambapo anayekataa kuandamana nao anatukanwa na kufedheheshwa. Hata mmoja  wa watangazaji wa televisheni ya Sky News alipomuuliza swali muhimu juu ya mwenendo wa ulipaji kodi wa baadhi ya wasanii walioshiriki kwenye wimbo huo hakutoa jibu zuri zaidi ya aina ya matusi.

Kwa hakika, hili lingekuwa jibu la kutarajia kutoka kwa mtu mwenye umri wa miaka 21 kwenye mtandao wa YouTube,  lakini kutoka kwa mtu mwenye umri wa miaka 63 anayejidai kujitolea kupambana na Ebola tuseme ni nini zaidi ya ufedhuli? Anatarajia vipi sisi tumchukulie kwa umakini iwapo hawezi kuwa na tabia njema?

Hakuna mtu anayetaka Ebola kusambaa duniani, lakini pia sipendi dunia iwe na wagonjwa wengi wa Malaria au VVU/Ukimwi na Kifua Kikuu pamoja na magonjwa mengine mengi – achilia mbali majanga ya njaa na umasikini – yanayoharibu maisha ya mamilioni ya Waafrika kila siku.

Sipendi kuelezwa jinsi ya kukuza hali yangu ya maisha na mtu mwenye utajiri unaokadiriwa kuwa pauni milioni 32, lakini anayedaiwa kushiriki katika miradi ya kukwepa kodi. Alipoulizwa na mwanahabari miaka miwili iliyopita analipa kodi kiasi gani alimlipukia mwanadada Yule akisema: “Muda wangu je? Hiyo si kodi? Sawa, hapana, Bob, sio.

Sitaki kutoa kwa upendo eti baada ya kuombwa na bendi ambayo wanamuziki wake wanasafiri kwa ndege tofauti, tena ya binafsi kwa sababu hawaelewani na wale wa One Direction au na Bono (msanii) anayekwepa kodi kwa Serikali ya Ireland lakini hapo hapo wanatumia muda mwingi kuiambia Serikali ya Ireland isaidie nchi zinazoendelea.

“Kwa kweli haijalishi ikiwa hupendi wimbo huu. Unachotakiwa kufanya ni kununua kitu hiki,” ndivyo alivyosema Geldof wakati akizindua single hiyo.

Lakini kweli tufanye hivyo? Tunawiwa? Tusipotekeleza yaweza kutufanya sisi tuwe watu tusiojali au kuhisi uchungu kwa wanaoumia? Vipi kama tumeshatoa fedha kwa ajili hiyo au kwa wenye matatizo mengine? Lazima tununue single yao?

Nihitimishe kwa kusema kwamba huu ndio msingi wa pingamizi langu dhidi ya Band Aid. Wanataka kujenga hisia kwamba watu wa Uingereza hawana moyo wa kusaidia wala si wakarimu wakati wametoa sana. Ni wakati mwafaka kwa watu wa aina ya Geldof kuacha kutuomba fedha. Waige mfano wa Adele kwa wao wenyewe kutoa fedha zao, kwanza wema huanzia nyumbani.  

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Man United: Hakuna kusajili Januari

Nigeria nje AFCON