Habari kwamba bingwa wa uzito wa juu, mwanamasumbwi, Tyson Fury hatapigana kwa miezi sita akipumzika na kutibiwa matatizo ya akili zimepokewa kwa heshima Uingereza. Ni mara chache sana wanamichezo wakubwa wakubwa maarufu hukubali kunawa mikono wakionesha ukweli wa maisha yao. Mwanasoka Gazza- kiungo maarufu wa timu ya England aliyewika miaka 90 amehangaika muda mrefu sana na maradhi ya akili na ulevi. Gazza alikuwa mwanamichezo mzuri sana enzi zake kwenye kiwango cha mwanasoka David Beckham na bondia Lennox Lewis.
Tyson Fury alizaliwa mwaka 1988 na kuutwaa ubingwa mwaka jana. Licha ya urefu wa juu sana – sentimeta 206 (futi 6 na inchi 9) – Tyson ni maarufu kwa mbwembwe na domo kaya. Mwaka 2015 alipopewa taji la mwanamichezo bora wa mwaka, kelele nyingi zilisikika kwa msimamo uliowakera Wazungu wenzake kukashifu ushoga wazi wazi. Baada ya mida taji liliondolewa.
Karibuni Tyson aliamua kujitoa nafasi ya uzito wa juu WBO, WBA na IBO, taasisi muhimu za ngumi duniani. Alisema ameamua kuachana na kuzingatia matibabu ya akili na matumizi ya dawa za kulevya. Mambo haya yamemletea maradhi yaitwayo “manic depression” kushindwa kupambana na Wladimir Klitschko kutoka Ukraine. Klitschko alitolewa na Tyson Fury mwaka jana na pambano lao lililotarajiwa mwisho wa mwezi huu lilikuwa kuuteteta ushindi huo.
Klitschko ambaye pia ni mrefu sentimeta 1.98 yaani futi 6 kwa inchi 6, ana umri wa miaka 40 na ilitegemewa hili liwe pambano lake la mwisho.
Maradhi ya Tyson Fury yameenea sana dunia hii na mpiganaji ngumi mwingine maarufu David Haye mara moja alimsifia : “Mimi pia nilikuwa na tatizo hilo. Kimwili nilikuwa safi kabisa lakini nilijikuta na tabia ya kujifungia ndani, nikazima simu na taa. Nikakaa siku kadhaa bila kuongea na mtu.”
Haye mwenye umri wa miaka 36, ambaye hakuwahi kupambana na Tyson Fury kutokana na majeraha alisisitiza tatizo hilo wanalo wengi, ila hawalisemi wazi wazi au kusaka tiba.
Matatizo ya “manic depression” hutokana na kuzaliwa nayo katika familia au vurugu tu za kimaisha. Dalili za maradhi haya ni mtu kuwa na mabadiliko mabadiliko ya kihisia. Mara moja hujisikia vibaya halafu ghafla akaona raha au kutotaka kutulia, na kuhangaika hangaika. Huanzia miaka 15-19 na ni nadra sana kutokea baada ya miaka 40.
Matokeo ya hisia hizi ni mtu kuwa na fikra za kutokuwa na matumaini, kushindwa kuamua mambo haraka, kuchanganyikiwa changanyikiwa na kukosa raha kiasi cha kuamua kujiua.
Kihisia unapokosa raha au matumaini, tabia huathirika na matokeo mtu hutaki kufanya mapenzi, kazi, kula, kulala au hata kuzungumza.
Tatizo hili linalowafanya wahusika kutokuwa na mawasiliano mazuri na wanadamu wenzao hutibiwa kwa vidonge na waganga wa kisaikolojia. Mabondia wengine maashuhuri wenye maradhi ya akili ni Rick Hutton na Frank Bruno. Bruno aliyewahi kupambana na mtemi Mike Tyson akapigwa amekuwa pia muwazi kuhusu tatizo hili.
Vyombo mbalimbali vya afya, michezo na jamii vimeanza kupiga kelele kuitaka serikali iwe makini zaidi kutathmini na kuwatibu walemavu wa akili katika tasnia ya michezo. Tyson Fury ni mfano mzuri wa uamuzi usio na aibu