Nyota 25 kutoka timu mbalimbali wameitwa katika timu ya taifa ya soka ya Tanzania ya wanawake ‘Twiga Stars’ kwa ajili ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na mechi ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake dhidi ya wenzao wa Namibia itakayochezwa Januari 15 jijini Windhoek.
Akitangaza majina ya wachezaji hao, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), Boniface Wambura alisema kuwa kikosi hicho kitaanza mazoezi rasmi Jumatatu chini ya kocha wake Boniface Mkwasa anayesaidiana na Nasra Juma kutoka Zanzibar.
Wambura aliwataja wachezaji walioitwa kuwa ni pamoja na nahodha Sophia Mwasikili (Sayari Women), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma Omari (Sayari Women), Mwajuma Abdallah (JKT), Asha Rashid (Mburahati Queens), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens), Ettoe Mlenzi (JKT), Zena Khamis (Mburahati Queens), Fatuma Khatib (Mburahati Queens), Maimuna Said (JKT), Fadhila Hamad (Uzuri Queens), Fatuma Mustapha (Sayari Women) na Evelyn Senkubo (Mburahati Queens).
Wachezaji wengine waliotwa ni Rukia Hamisi (Sayari Women), Mwapewa Mtumwa (Evergreen), Judith Hassan (TMK), Aziza Mwadini (Zanzibar), Sabai Yusuf (Zanzibar), Semeni Abeid (Tanzanite Queens), Zena Said (Uzuri Queens), Pulkaria Charaji (Sayari Women), Tatu Said (Makongo Sekondari), Mwanaidi Hamisi (Uzuri Queens), Hanifa Idd (Uzuri Queens) na Fatuma Gotagota (Mburahati Queens).
Alisema kuwa baada ya kuanza mazoezi timu hiyo itatafutiwa mechi za kirafiki kabla ya kuelekea Namibia ili wachezaji waende huko wakiwa wameimarika zaidi na kukabiliana na ushindani.
Aliongeza kwamba mechi ya marudiano kati ya timu hizo mbili itachezwa Januari 29 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na mshindi kati ya Twiga Stars na Namibia atakutana kati ya Ethiopia au Misri.
Fainali hizo zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake zimepangwa kufanyika Oktoba mwakani huko Zimbabwe.
Mwaka jana wawakilishi hao wa Tanzania walifuzu kushiriki fainali hizo zilizofanyika nchini Afrika Kusini lakini walifungwa mechi zote tatu za hatua ya makundi na kutolewa mapema.
Comments
Loading…