England kigugumizi Kombe la Dunia
*Wang’ang’aniwa Montenegro kwa sare
*Ujerumani ina kiwango kikubwa kufuzu
Matarajio ya Zimbabwe kucheza fainali za Kombe la Dunia yalifishwa, baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri jijini Alexandria.
Mabingwa hao wa soka mara saba wa Afrika, wanaongoza katika kundi G, na wanataka kurejea fainali hizo za FIFA, baada ya kushindwa kufuzu kwa miaka 24.
Zimbabwe hawakukubali kichapo kwa urahisi, na hadi nusu ya kwanza inamalizika walikuwa wametoshana nguvu wakiwa suluhu.
Hata hivyo, katika dakika ya 64, Hosni Abd-Rabou aliondoa udhia kwa timu yake kwa kutumbukiza mpira wa adhabu ndogo katikati ya ukuta wa Zimbabwe na kuandika bao safi.
Wageni hao hawakukubali kudhalilika kirahisi, kwani katika dakika ya 75, Knowledge Musona anayechezea Ujerumani alipachika bao kwa fataki ya uhakika, licha ya kuchezewa vibaya na mlinzi Mohamed Naguib na kufanya ubao usomeke 1-1.
Zimbabwe walikaribia kuondoka na pointi moja muhimu, lakini dakika tatu kabla ya mechi kumalizika, Mohamed Salah akienda kumwona golikipa aliangushwa na Augustine Mbara, iliyobaki ilikuwa Mohamed Abou-Treika kuweka mpira kimiani kwa mkwaju wa penati na mechi kumalizika kwa ushindi wa 2-1.
Kwa matokeo hayo, Misri wanaendelea kuongoza wakiwa na pointi tisa, wakifuatiwa na Guinea wenye pointi nne, kisha Msumbiji pointi mbili na Zimbabwe wamebaki na pointi moja tu. Timu zote zimecheza mechi tatu, hivyo bado nyingine tatu za marudio.
Timu ya taifa ya soka ya England imeshindwa kujiweka pazuri kujihakikishia kwenda fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani.
Sare yao ya bao 1-1 na taifa dogo la Montenegro inamfanya kocha Roy Hodgson kunoa bongo zaidi kuhakikisha wanashinda mechi nne zilizobaki.
England walianza kwa kasi, Wayne Rooney akafunga bao kwa kichwa dakika ya sita tu, lakini walipokwenda mapumziko, walirudi kama walioloa na Montenegro wangeweza kuibuka na ushindi mkubwa tu, lakini wakapata bao moja.
Kwa sare hiyo, Montenegro wanaongoza kundi ‘H’ kwa pointi 14, England wana pointi 12, Poland na Ukraine pointi nane kila moja, Moldova pointi nne na San Marino hawana kitu.
Hata hivyo, Poland na Ukraine wana mchezo mmoja pungufu ya timu nyingine, hivyo kuwaacha England katika sintofahamu kubwa.
Katika matokeo mengine, Uholanzi waliwatandika Romania mabao 4-0, Ukraine wakawachapa Moldova 2-1 na Serbia wakawaondosha kabisa Scotland katika kampeni ya kwenda Brazil kwa kuwafunga mabao 2-0.
Israel walitoa onyo jingine baada ya kuwapa Ireland Kaskazini kichapo cha mabao 2-0 wakati Jamhuri ya Ireland walitoka sare ya mabao 2-2 na Austria.
Wales walianza vyema mechi yao dhidi ya Croatia na kupata bao kupitia kwa Gareth Bale, lakini walitota baadaye kwa mabao 2-1.
Jamhuri ya Czech waliwapelekesha Armenia kwa kuwachabanga mabao 3-0, Ureno wakapata ahueni kwa kuwafunga Azerbaijan kwa mabao 2-0.
Estonia waliwazidi nguvu Andora kwa kuwafunga mabao 2-0, Uturuki na Hungaria wakitoshana nguvu kwa bao 1-1 kama ilivyokuwa kwa Denmark na Bulgaria.
Katika kundi A Ubelgiji na Croatia wanaongoza kwa pointi 16 kila moja; kundi B Italia ipo mbele ikifuatiwa na Bulgaria.
Ujerumani wanaongoza kundi C kwa tofauti ya pointi nane, wakifuatiwa na Austria, Sweden na Jamhuri ya Ireland wote wakiwa na pointi nane.
Uholanzi wanachekea nafasi ya kwanza kundi D kwa pointi 18 wakifuatiwa na Hungaria wenye pointi 11 na Romania pointi 10.
Uswisi wana pointi 11, Iceland tisa sawa na Albania katika kundi E wakati Norway ni wa nne kwa pointi saba.
Urusi wanaongoza kundi F kwa pointi 12 wakifuatiwa na Israel na Ureno zenye pointi 11 kila moja na katika kundi G Bosnia Herzegovina wanaongoza kwa pointi 13, Ugiriki wakiwafuata kwa pointi 10 na Slovakia pointi nane.
Kundi I lina Hispania juu yake wenye pointi 11 wakizengewa kwa karibu na Ufaransa wenye pointi 10.
Ulaya ina nafasi 13 kwenye Kombe la Dunia, ambapo mfumo wa kufuzu kucheza fainali hizo uliowekwa na UEFA ni timu moja kutoka kila kundi, ikimaanisha jumla ya timu tisa.
Timu nne zilizobaki zitapatikana kwa kucheza mechi mbili, nyumbani na ugenini kwa timu zinazoshika nafasi ya pili katika kila kundi, washindi wakipata tiketi moja kwa moja. Hata mabingwa watetezi – Hispania lazima wapite mchujo huo.
Comments
Loading…