*Wana kila kitu lakini wanashindwa uwanjani
Wiki hii tulishuhudia maajabu ya soka na jinsi Arsenal wanavyoweza kuwatesa wanachama, washabiki na hata wadau wake, ambapo walipoteza uongozi wa mabao 3-0 waliokuwa nao nusu saa kabla ya mechi dhidi ya Anderlecht kumalizika, wakatoka 3-3.
Hii ilinifanya niweke bayana kwamba inahitaji moyo sana kujitangaza waziwazi kwamba wewe ni shabiki wake au hata kubaki na imani nao, kwa sababu ya jinsi wanavyochanganya watu na kupata matokeo yasiyotarajiwa kabisa wakati ushindi ukiwa mikononi mwao.
Mjadala mkubwa umeibuka juu ya hilo, baadhi wakikubali kwamba Arsenal wanakatisha tama, lakini baadhi ya washabiki wa Tottenham na Newcastle wanaelekea kutofautiana na nadharia hiyo, pamoja na wengine wa klabu ndogo zenye matatizo makubwa kuliko Arsenal.
Ukweli ni kwamba unaweza kuwa shabiki wa timu fulani ndogo, kwa mfano Southend, mwingine akawa Manchester (iwe City au United) na mwingine Arsenal. Wale wa klabu ndogo zinazofungwa hawatachanganyikiwa kama inavyotokea kwa wa Arsenal kwa sababu ya mazingira.
Wanaounga mkono klabu nyingine ndogo wanakuwa tayari na wazo kwamba bado wanajijenga, wanatarajia kufungwa japo hawapendi lakini wa Arsenal wanajua uwekezaji mkubwa umefanywa, wapo wachezaji wazuri japokuwa bado fursa za kuchukua wazuri zaidi, hasa walinzi, hazikutumiwa ipasavyo.
Newcastle wanaweza kuwa wanaudhi kwa jinsi wanavyokuwa kama wameganda kwa muda mrefu, wakishindwa kusonga mbele, kufunga mabao na kupata ushindi lakini hufika mahali washabiki hawatarajii kubwa zaidi, lakini majuzi hapa wameibuka na kuwakandika Man City na hata Liverpool.
Spurs wanajulikana kwa tabia yao ya kuwekeza sana kwenye itikadi moja, kisha wakasonga mbele na kuvuruga kila kitu. Inaumiza, lakini miongoni mwa washabiki wao, ni yupo alipata ndoto kwamba wangefikia kutwaa ubingwa wa England? Hasa baada ya Mwenyekiti Daniel Levy kumuuza Gareth Bale.
Arsenal wapo kwenye aina tofauti ya mkato wa tamaa, kwa sababu, tofauti na klabu hizo nyingine, wana uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kisoka. Hakika, mafanikio makubwa kwao, kwa kuzingatia rasilimali walizo nazo, ni jambo lililo wazi kabisa, tatizo utekelezaji, na hapo ndipo wanapoumiza watu.
Wamezoea mno kuvuruga mipangilio na matarajio; ambapo mechi ya majuzi kila mmoja alijua wangeshinda kirahisi wka sababu walikuwa wakubwa zaidi, wenye nguvu zaidi na uzoefu kuliko vijana wa, Anderlecht kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL). Ndiyo maana wtau walitikisa vichwa kuona mwelekeo mzuri walipokuwa 3-0 mbele, lakini wakavishika na kugeuka wekundu baada ya mabao yote kurudi, akiwamo kocha Arsene Wenger.
Kinachowatofautisha Arsenal na timu nyingine kama Spurs, Newcastle na southend ni kwamba hawana kisingizio katika upupu waliofanya; wana kila rasilimali ya kuwafanya wawe klabu iliyofanikiwa zaidi, yenye vikombe vingi duniani lakini wanaposhindwa kutumia fursa si jambo la kawaida.
Newcastle wako vizuri kwa maana ya uungwaji mkono wa washabiki na uwanja mzuri, lakini zama hizi za uungwana katika matumizi ya fedha, klabu zinatakiwa kutumia tu kile wanazopata kujiweka vyema. Wanaweza kupata washabiki zaidi ya 50,000 uwanjani kwao, lakini hawawezi kutoza viingilio wanavyotoaz Arsenal.
Kadhalika hawana ubavu wa kuvutia matajiri wa dunia, mashirika na kampuni kubwa kwa ajili ya kuwadhamini, jambo ambalo kwa Arsenal ni kawaida na wanaingia mamilioni ya pauni kila mara.
Spurs wangeweza kwenda sambamba na Arsenal katika mapato ya mechi, lakini hawana uwanja wa kuwaweka watu wengi kiasi hicho, dimba la White Hart Lane linalochukua watu 36,000 linawakwamisha wakati Arsenal wana dimba la pili kwa ukubwa hapa baada ya Man United pale Old Trafford.
Arsenal wamekaa sehemu nzuri hapa London kimkakati, kibiashara na kisoka, kana kwamba kusema uwanja huo umelipiwa tayari. Kadhalika wana eneo bora la kisasa kwa mazoezi, akademia nzuri kabisa na mtandao mpana wa wang’amua vipaji, wafanyakazi wenye viwango na uzeofu na falsafa ambayo daima itavutia washabiki wapya.
Kuendelea kwao kwa msimu wa 17 mfululizo kufuzu kwa UCL kunawapa nafasi, wakipenda, kuvutia wachezaji nyota zaidi duniani na wana uwezo wa kuwalipa mishahara mikubwa bila kuhatarisha hatima ya klabu. Yote haya yanachangia katika washabiki wake kukatishwa tama na mwenendo wa watu wenye kila kitu na uwezo wa kupata makombe yote.
Comments
Loading…