TUNATANIWA sana siku hizi. Eti Zinedine Zidane anamchukia Gareth Bale. Huu ni utani wa ngumi. Wapinzani wetu wanaona hali ilivyo kuwa Bale hana morali ya kucheza mpira. Haoneshi kuwa yule aliyewaliza Liverpool au kuwakimbiza Barcelona.
Watani wetu wamekazana kutunanga kuwa Bale tunamchukia mno kiasi kwamba chuki imeoneshwa hadharani. Lakini Bale mwenyewe hasikiki kokote akizungumzia suala hilo. Sisi hao tuanze kumchukia jamani? Tunaanzaje? Aaah!
Huu utani sasa unaudhi mno sisi manazi kindakindaki wa Real Madrid. Lakini chini ya Zinedine Zidane kuna majibu. Majibu hayo yatakuja na swali safi kabisa; nani atapitiwa fagio la Zinedine Zidane?
Hilo ndilo swali linabaki sasa hadi utakapoanza msimu mpya. Na zaidi jina la Gareth Bale ndilo lina habari nyingi kuliko wengine. Wengi wanajua kuwa baada ya kuondoka Cristiano Ronaldo basi nafasi ya kuwa staa wa timu ilikuwa ya Gareth Bale.
Ndiyo, Bale mpenzi wa kucheza mchezo wa gofu, alikuwa ametoka kupachika mabao mawili muhimu katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Liverpool misimu miwili iliyopita. Ronaldo alielekea Juventus Turin.
Hata hivyo haikutokea Bale kuwa mchezaji muhimu zaidi. Karim Benzema na Sergio Ramos wakaimarisha uti wa mgongo wa timu. Mgawanyo wa ushindi ukaenda kwa wengine, wakaibuka Vinicius Junior, Rodrygo Goes, kisha amekuja Eden Hazard na Thibaus Courtois.
Chini ya kocha Julen Lopetegui hakukuwa na kiwango chochote kipya kutoka kwa Bale. Chini ya kocha Santiago Solari tuliona akimpa nafasi zaidi Vinicius Junior ambaye ni kinda kuliko Bale.
Solari aliamua kuwatosa baadhi ya mastaa kwa madai wameshuka viwnago na hawana ubora zaidi. Msimamo wake ulikuwa waondoke tu. Kule beki tatu alimpanga Sergio Reguilon badala ya Marcelo. Upande wa winga wa kushoto alimpanga Vinicius badala ya Bale.
Aliporudishwa Zidane aliamua kumpa nafasi kila mchezaji. Lakini ukweli usemwe kipaji cha Bale hakimvutii Zidane ambaye anaamini jamaa akula mpunga tu, wakati hana cha kitu cha kutisha mguuni, ukiondoa mbio zake.
Hayo yanatafsiriwa kutokana na Zidane kuwa mmoja wa nyota soka duniani, akiwa ametwaa tuzo mbalimbali. Kiburi cha uwezo ndicho kinamfanya aone Bale hana kitu cha kutisha kwenye kandanda licha ya kununuliwa bei kubvwa.
Pengine akilini mwa Zidane anaamini Bale hakustahili hata kuchezea Real Madrid. Pengine anaona Bale amebadilika kimwenendo jambo ambalo mara kadhaa amesema.
Katika mechi 6 za mwishoni mwa msimu huu Bale amewekwa benchi zote. Zidane alitetea uamuzi huo kwama ulikuwa wa kiufundi zaidi. Nimemsikia David Bettoni naye akidai kuwa Zidane hatarajii kuonesha umaalumu wowote kama kocha kwani alichojaliwa ni uhusiano mzuri na wachezaji wake pamoja na uthubutu wa kuchukua maamuzi magumu kwenye timu.
Kwenye hili la maamuzi magumu huenda ndio maana akaamua kuachana kikazi na Antonio Pintus kwa madai hakupswa kuendelea kubaki klabuni wakati yeye alipojiuzulu. Matokeo yake nafasi ya kocha wa viungo ya Antonio Pintus imechukuliwa na mwingine. Zidane akaona Pintus ni msaliti tu, sembuse Bale?
Sasa kwa Bale hali inaonekana hivyo, ikizingatiwa huyu mwarabu, halafu ana tabia za Wafaransa za kiburi zaidi. Kumkobolesha mahindi benchi Bale ni kutuma ujumbe kwa Florentino Perez “huyu simhitaji”.
Bila shaka baada ya kutwaa ubingwa wa La Liga umempa kiburi kingine cha kumwambia Perez afanye tathmini mchango wa Bale hadi kupatikana ubingwa huo. Hapo ndipo mahali ambalo Perez na bodi yake wanatakiwa kuamua nani anabaki kati ya Bale na Zidane.
Taarifa zinasema Zidane atakuwa kocha wa Real Madrid msimu ujao. Wakati anarejea mwaka jana alisaini mkataba wa miaka miatatu, na bila shaka utamalizika mwishoni mwa msimu ujao. Ikiwa Zidane anabaki Real Madrid maana yake Bale lazima aondoke au akibaki akubali kukoboa mahindi benchi.
Kwa vile Real Madrid kwa sasa imeanzisha mkakati wa kukusanya kiasi cha pauni milioni 300 kutoka kwenye mauzo ya wachezaji, bila shaka jina la Bale linaweza kuwa miongoni mwake.
Real Madrid tayari wamemuuza Achraf Hakimi kwenda Inter Milan, na kuna uwezekano baadhi ya makinda wanaorejea kutoka kwa mkopo kwenye timu mbalimbali watauzwa.
Nyota mwingine ambaye anatakiwa kuondoka ni James Rodriguez. Hana uhakika wa namba kikosini, ingawa ana kismati cha magoli. Ana nyota nzuri, ana uwezo wa kufunga, uwezo wa kiufundi na akili yake ni bora. Lakini ndani ya kikosi cha Real Madrid chenye mafundi inamlazimu James kukalia benchi. Pia mbinu za kocha zinachangia James kukaa nje.
Nimesoma mahali Toni Kroos anasema sakata la Bale limewachosha tangu msimu uliopita. Kroos amefichua kuwa msimu uliopita Real Madrid ilishaamua Bale aondoke na yeye alikuwa tayari kufanya hivyo, lakini palitokea mabadiliko kwa uongozi kubadili msimamo.
Tatizo la Gareth Bale haongei mwenyewe. Masuala yake yote yanayohusu anazungumza wakala wake Jonathn Bernett. Kwamba Bale hata kwenye vita ya maneno na Zidane amekuwa akimtumia wakala wake tu.
Kimsingi Zidane anajua njia hiyo, ambayo inaonesha wazi Bale anafanya unafiki mbele yake kiasi kwamba anaweza kukana maneno ya wakala wake kuwa yeye hajazungumza.
Ndani ya uwanja kuna wachezaji wanne wanaomfukuza Bale Real Madrid. Ujio wa Rodrygo Goes Silva na Vinicius Junior, Eden Hazard na Lucas Vazquez.
Hazard na Vazquez ni ‘askari’ watiifu wa Zidane wasio na maneno wala kuonesha tabia za unyangumi ndani ya kikosi. Hii ni tofauti kwa James na Bale ambao daima ni manyangumi kikosini hali ambayo inakosesha utulivu. Angalau James aliporejea kutoka Bayern Munich amebadilika, hali ambayo imemfanya apunguze unyangumi kikosini.
Zidane amemaliza msimu 2019-2020 kwa kuwajenga zaidi Rodrygo na Vinicius kuliko kumpa nafasi Bale. Katika mechi 6 alizomweka benchi Bale, tumewaona Rodrygo na Vinicius wakipewa dakika nyingi.
Katika mazingira hayo Bale anafukuzwa ndani ya uwanja kwa ‘maamuzi ya mbinu za mchezo’. Hii ndiyo staili anayotumia Zidane kumweleza Perez, katika mbinu zake kikosini hamhitaji Gareth Bale. Ndio maana hakuna picha ya Bale akiwa ameshika kombe la La Liga.
“Kama Gareth Bale akiamua kuhama hata kesho, kwa hakika litakuwa ni jambo bora zaidi kwa kila upande.’ Maneno ya Zidane Julai 21 mwaka 2019 jijini Houston, Marekani. Na sasa Zidane tena ametumia maneno mawili tu, “Tactical decision” kumweka benchi Bale.