Menu
in , , ,

Zidane anapenda masika sana kuliko kiangazi

Tanzania Sports

Moja ya kosa kubwa ambalo wengi huwa tunalifanya ni pale tunapojisahau na kuamini kuwa furaha zetu hutegemea kitu/mtu.

Yani bila mtu/kitu fulani ni ngumu kwetu sisi kupata furaha. Hapo ndipo hatua ya kwanza ya maumivu inapoanzia.

Hapo ndipo palipo na chimbuko la maumivu ndani yake. Maisha ni furaha, hiki ndicho tunachotakiwa kukijua.

Tunatakiwa kuishi maisha yenye furaha ndani yetu. Na furaha siku zote hutengenezwa na mtu mwenyewe. Hakuna furaha ambayo mwanadamu yeyote hutengeneza kwa ajili ya mwanadamu mwingine.

Na kama ipo hiyo itakuwa furaha ya muda mfupi na siyo furaha ya muda mrefu. Kipi unakitafuta katika maisha yako ?, furaha inayoyeyuka au furaha inayosimama kama mwamba?

Hili ni swali muhimu sana. Swali ambalo huja na mwongozo sahihi wa kupata furaha. Furaha ya dhati hupatikana kwenye mikono ya mhusika mwenyewe.

Ndiyo maana tunashauriwa sana kujifunza kutafuta furaha. Hapa ndipo ambapo tunapokuja kuona ambavyo Zinedine Zidane alivyo na uwezo mkubwa wa kujitafutia furaha.

Anapenda kuishi kwenye furaha, anapenda kuishi kwenye sehemu ambayo kuna masika. Masika ambayo yanaweza kumsaidia kwenye kilimo chake.

Anajua kabisa jinsi ya kujitengenezea mazingira ya masika, anajua kabisa kujitengenezea mazingira ya kumpa furaha.

Yani kwa kifupi anajua kutengeneza furaha kwa mikono yake mwenyewe. Wakati anachaguliwa kuwa kocha wa Realmadrid alifanikiwa sana na timu hii.

Alibeba ligi ya mabingwa barani ulaya mara tatu mfululizo. Alikuwa na kikosi imara sana. Kikosi ambacho kilikuwa na Cristiano Ronaldo.

Mwanadamu ambaye alikuwa anafunga magoli kuanzia 50 ndani ya msimu mmoja. Kwa hiyo wakati yupo Realmadrid alikuwa na uhakika wa timu yake kupata magoli 50 kupitia mtu mmoja tu!.

Alikuwa na wapishi mahiri wa magoli, Toni Kroos alikuwa mpishi bora sana. Luka Modric alikuwa mhimili mkubwa sana ndani ya kikosi cha Realmadrid.

Akamtengeneza Casemiro kuwa kiungo bora wa eneo la kuzuia. Sergio Ramos alikuwa beki imara.

Beki ambaye alikuwa anauwezo mkubwa wa kuyalinda magoli na alikuwa na uwezo wa kuyafunga pia hayo magoli.

Unamkimbuka Marcelo?, beki ambaye alikuwa na sifa nyingi sana za kuwa mshambuliaji?

Huyu alikuwepo kwenye kikosi chake na akamfanya kuwa beki ambaye alikuwa anatengeneza nafasi nyingi za magoli yeye pamoja na Dani Carvajal.

Lakini taratibu hali ya dalili ya kiangazi ilianza kuonekana katika klabu ya Realmadrid, Cristiano Ronaldo aliondoka Realmadrid.

Toni Kroos na Luka Modric wakawa wameshuka kiwango. Vivo hivo kwa Dani Carvajal na Marcelo.

Dalili za kupata Realmadrid ambayo ni dhaifu zilianza kuonekana. Ndipo hapo Zinedine Zidane alipoamua kujitoa taratibu na kupumzika kwa muda.

Akaiacha Realmadrid dhaifu, Realmadrid ambaye kwa hivi karibuni imefungwa mechi 5 mfululizo katika uwanja wao wa nyumbani zikiwemo mechi mbili dhidi ya Barcelona.

Realmadrid ambayo imetolewa kwenye ligi ya mabingwa barani ulaya na Ajax kwa kufungwa katika uwanja wao nyumbani.

Realmadrid ambayo iko nafasi ya tatu katika ligi kuu ya Hispania (La Liga) ikiwa nyuma kwa alama 12 na mtu anayeongoza ligi.

Msimu umekaribia kuisha, Zinedine Zidane anarudi tena Realmadrid. Anarudi kipindi ambacho watu wengi hawata mhukumu kwa matokeo haya ya mwishoni.

Kitu kizuri kuwa tunaenda kuingia katika dirisha kubwa la usajili, dirisha ambalo litampa nafasi yeye kusajili wachezaji nyota ambao atatembea nao.

Tayari amekuja kipindi ambacho anauwezo wa kujitengenezea masika yake. Kipindi ambacho anauwezo wa kujitengenezea furaha yake mwenyewe.

Kipindi ambacho ana uhakika wa kuingia sokoni kumchukua Mbappe, Neymar , Hazard kwa ajili ya kuendelea kutengeneza Ufalme wake pale Santiago Berbaeu.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version