Menu
in , , ,

ZANZIBAR WALIPATA FURAHA CECAFA, AIBU WAMEIPATA CAF

Tanzania Sports

Tulishuhudia CECAFA, macho yetu yalipendezwa na vingi vilivyotokea
Kenya kwenye michuano ya CECAFA.

Furaha ambayo ilipitiliza kiasi kwamba tulitumia kubeza sehemu moja na
kusifia sehemu nyingine bila kutuliza akili zetu kwa umakini.

Zanzibar ilisifiwa sana, Tanzania bara ilizodolewa sana, cha ajabu
tulifika sehemu ambayo ilitulazimu kusema Zanzibar wana misingi imara
ya soka na kama wakipewa uanachama wa FIFA watafuzu kombe la dunia.

Nilishtuka baada ya kusikia maneno hayo, nafsi yangu iliniambia
usiingie kwenye mkumbo huo wa kusifia wakati nikiwa na furaha.

Akili yangu ilitulia nikaamua kuandika makala ambayo niliwaambia
Zanzibar maeneo wanayotakiwa kuyapitia ili na mimi niwasifie.

Sikutaka kuwasifia Zanzibar na kuwaweka daraja la juu kwa sababu ya
kufika kwao fainali ya kombe la CECAFA.

Michuano ambayo haina ushindani na mvuto ndani na nje ya uwanja,
michuano ambayo timu za taifa hupeleka vikosi vya vijana kushiriki
michuano hiyo.

Michuano ambayo Zanzibar ilitegemea wachezaji wengi wanaocheza ligi
ambayo siyo ya Zanzibar, ndiyo maana nikaona hakuna mipango dhabiti
katika soka la Zanzibar.

Mipango ambayo inawezesha kutoa timu yenye ushindani wa hali ya juu na
kushindana na timu zilizo bora.

Ligi yao imekuwa dhaifu miaka nenda rudi, hata baada ya michuano ya
CECAFA mwaka huu kulifanyika michuano ya kombe la mapinduzi ambayo
vilabu vya Zanzibar vilifanya vibaya.

Hiki ndicho kilichoonesha hali halisi ƴya ligi ya Zanzibar ilivyo.

Ligi imara siku zote hutoa vilabu ambavyo ni imara, vilabu ambavyo
vinaweza vikashindana katika ngazi kubwa na kufanya vizuri.

Kushindwa kwao kufanya vizuri katika michuano ya Zanzibar mbele ya
timu tano kutoka nje ya Zanzibar ilikuwa ni kielelezo tosha ƙligi kuu
yao ni dhaifu.

Udhaifu ambao unatokana na kuendeshwa vibaya kwa ligi hii, hakuna
mipango dhabiti ya kuifanya ƙligi hii iwe imara.

Timu yenye timu zaidi ya 20 lakini haina mdhamini, timu zinashiriki
katika mazingira magumu, mazingira ambayo hayatoi motisha kwa
wachezaji kupigana kwa nguvu zote.

Viongozi wa ZFA wamekaa maofisini bila kufanyia ufumbuzi wa hili jambo.

Hakuna kitu kipya wanachokiwaza ili kuimarisha ligi hii zaidi ya wao
kukaa na kuimarisha migogoro kati yao.

Viongozi wa Unguja na Pemba hawana maelewano mazuri kati yao, kuna
migogoro kila uchwao.

Migogoro ambayo inadumaza maendeleo ya mpira Zanzibar, badala ya
kufikiria namna sahihi ya kuchochoe kuni za maendeleo wao wanawaza
namna gani wataongeza majiko ya kupikia migogoro yao.

Kitu kinachopelekea mpaka baadhi ya timu kugoma kushiriki ligi kuu Zanzibar.

Hakuna anayeshtuka kuhusiana na hiki kitu, kitu pekee kitakachowashtua
ni wao kuamka siku moja mifuko yao haina pesa.

Watakuna kichwa kuangalia njia sahihi ya wao kushibisha tumbo lao na
kusahau kuwa wapo pale kwa ajili ya kushibisha njaa ya wapenda mpira
Zanzibar.

Mwisho wa siku ligi inatosha timu dhaifu, timu ambazo haziwezi
kushindana ipasavyo kwenye michuano ya vilabu Afrika.

Ndiyo maana haikuwa ajabu Zesco kuwaadabisha JKU magoli saba (7), na
hakuna aliyeshtuka kuhusiana na hiki ƙkipigo.

Tunasubiri timu ya taifa iende kushiriki CECAFA ifike fainali
ipokelewe kwa shangwe na kuvishwa taji la ushujaa.

Taji ambalo litaenda sambamba na mbwembwe za kuwapa wachezaji viwanja
kila mmoja kisa tu wamefika fainali ya kombe la CECAFA.

Kuna wakati bora kipofu anayeona kuliko mtu asiyekipofu na haoni.
Inauma sana viongozi wanaposhindwa kuona njia za misingi ya kukuza
mpira.

Hakuna anayeona namna ya kukaa kwenye njia ya maendeleo ya mpira.

Vile viwanja waliopewa wachezaji wa timu ya taifa haikuwa njia sahihi
ya kutengeneza mkondo wa maendeleo ya soka Zanzibar.

Nilidhani viwanja vile wangepanga kujenga kituo cha kulelea vipaji ili
wanufaike kwa baadaye.

Lakini kutokana na furaha kuwazidi walishindwa kuona mbele, macho yao
yakabaki kutazama walipokuwa wamesimama.

Ikawa ngumu kufanya hatua moja ya kwenda mbele, kwa sababu walishindwa
kutambua njia ya kupitia kwa sababu ya furaha

Mapinduzi na mashindano ya vilabu Afrika yameshatoa funzo tosha kwa
mpira wa Zanzibar, wanatakiwa wakae wamalize migogoro waliyonayo,
baada ya hapo waangalie namna sahihi ya kujenga ligi yenye ushindani.

Ligi ambayo itatoa washindani kama ilivyokuwa kwa Malindi waliofika
nusu fainali katika mashindano ya vilabu Afrika.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version