Shirikisho la Kimataifa la Soka, FIFA, jana limekata kidomodomo cha ZFA, Chama cha Soka cha Zanzibar, kwa kusema kuwa Zanzibar sio nchi, ila ni sawa na mkoa wa Arusha hivyo haustahili kupata mgao wa fedha zinazotolewa na shirikisho hilo kila mwaka kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
FIFA kila mwaka hutoa dola za Marekani 250,000 na ZFA imekuwa ikilalamikia Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, kuwa hailipwi sehemu ya pesa hizo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo wa FIFA katika nchi za ukanda wa Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi alisema kuwa fedha hizo zinatolewa kwa mipango maalum na utekelezaji wake unakuwa chini ya usimamizi wa TFF ambao ndio wanachama wanaotambuliwa na shirikisho hilo na sio ZFA.
Mamelodi alisema kuwa fedha hizo hazitolewi kwa vyama kwa ajili ya kugawana na hutolewa kwa malengo maalumu ya kuendeleza soka ambayo yanakuwa yameanishwa na baada ya utekelezaji wake FIFA huhitaji maelezo.
“FIFA inafanya kazi na TFF na Zanzibar ni kama Arusha au Kigoma ambayo ni sehemu ya Tanzania hivyo tutaendelea kuipatia fedha TFF na kupata maelezo ya matumizi kutoka kwao na si vinginevyo,“ alisema Mamelodi.
Aliongeza kuwa FIFA inaridhishwa na utekelezaji wa programu za maendeleo zinazofanyika hapa nchini na kusema kuwa hali ilivyokuwa mwaka 2004 kurudi nyuma sasa imebadilika.
Pia kiongozi huyo ambaye alikutana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF aliwataka kuangalia upya mipango yake ya muda mrefu na kuiboresha ili kupata mafanikio.
Aliwataka viongozi wa TFF kuendeleza walipofikia na kuwa mfano wa mabadiliko katika nchi za Afrika na kuongeza kuwa ndio nchi pekee ambayo inatolewa mfano kwa kubadilika na kuwa nchi ya kwanza kuanza kutekeleza maelekezo ya FIFA katika bara la Afrika.
- SOURCE: Nipashe