NGUMI zinashika kasi na sasa washabiki wanataka kuona wakali wawili katika Anthony Joshua na Tyson Fury wakipambana.
Mmoja wa mapromota wakubwa wa ngumi wa hapa Uingereza, Eddie Hearn, anasema kwamba angependa kuona wawili hao wakipanda jukwaani kuzichapa, akisema kwamba Joshua, au AJ kama anavyojulikana, ataingia ulingoni akipewa nafasi ndogo ya kushinda.
Hearn anasema wataonekana kituko iwapo watashindwa kusuka dili la mpambano huo na kwamba kambi yake inafurahi kuona jinsi watu wanavyomchukulia poa AJ, lakini siku ikifika ndipo mbivu na mbichi zitajulikana.
Tangu Fury amchape na kummaliza Deontay Wilder kwenye raundi ya saba huko Las Vegas, Marekani Jumamosi iliyopita, washabiki wamekuwa wakitaka Waingereza hawa wawili sasa wapambane.
Wilder alikuwa anashikilia mkanda wa WBC wa uzani wa juu, lakini mambo yalipomuwia magumu ulingoni, kambi yake ilisalimu amri. Joshua anashikilia mikanda ya WBO, IBO, WBA na IBF na hapana wasiwasi kwamba Fury atataka kumnyang’anya.
Shearn anasema kwamba hana nia ya kujaribu kuzuia pambano baina ya mabondia hao wawili. “Nilimwambia AJ usiku uliopita; ‘jambo kubwa juu ya hili ni kwamba unakwenda kwenye pambano ukipewa nafasi ndogo.
“Ni mara chache sana utamwona AJ akiingia ulingoni huku akipewa nafasi ndogo lakini wakati huu, unaangalia watu wanavyoweka madai yao, AJ anapewa nafasi ndogo dhidi ya Tyson Fury. Sawa kabisa – na ndivyo tunavyotaka iwe.
“Tunaamini tunaye mtu anayeweza kutokea na kuwa bingwa anayeshikilia mikanda yote ya uzani wa juu pasipo utata duniani. Tyson Fury anaamini kwamba anaweza kumpiga Anthony Joshua. Ni namna moja tu tunaweza kujua ukweli wa hili – kuhakikisha pambano linafanyika,” anasema Hearn.
Joshua aliupata tenda mikanda yake baada ya kurekebisha makosa yake ya Juni mwaka jana, ambapo Desemba alimpiga Andy Ruiz Jr kwa pointi katika pambano la marudiano. Alionesha ujuzi mkubwa na mbinu za kuvutia badala ya kutumia nguvu tu muda wote. Ameshachakaza mabondia kwa Knock-Out (KO) mara 21.
Akimzungumzia Furry, promota huyo alisema; “bondia maarufu … mpiganaji mjanja sana na sasa ameonesha kidogo kwenda mbele zaidi na kuonesha makabiliano ya nguvu. Je, atafanya hivyo kwa Anthoy Joshua? Mtu tofauti kabisa …Joshua si Deontay Wilder anayeweza kutupa konde kidogo lakini anaonekana si mzuri kwneye kurudi nyuma, anaweza kumalizwa baada ya kushambuliwa. Joshua ni bondia mkubwa wa uzani wa juu – kama walivyo wote. Watakapokutana litakuwa jambo moja la aina yake sana.”
Fury alisema kwamba alikuwa na uhakika wa kukabiliana na Wilder tena ili kukamilisha utatu anaoutaka dhidi ya bondia huyo wa Alabama. Desemba 2018 walikwenda sare. Makubaliano ya kurudiana yalikuwa na kifungu kinachoipa kambi ya Wilder siku 30 za kutafakari uwezekano wa pamban la tatu ambapo pochi itagawanywa kwa 60-40, Fury akichukua kilicho kimono zaidi.
Mapema, promota Hearn alisema; “sidhani kwamba kuna mtu anataka kuona pambano la tatu, hitimisho lilifanywa, lakini tutaona iwapo atataka kufanya hivyo. Ninavyoona, labda Wilder angependa kurudiana. Sioni kwingine anakoweza kwenda.”
Joshua amekuwa akipangwa kwa ajili ya kutetea mikanda yake jijini London dhidi ya Kubrat Pulev wa Bulgaria anayetakiwa kupigania mkanda wa IBF, huku mwezi Juni ukidhaniwa kwamba ndio wakati wa kupigana iwapo kambi yake itashindwa kupanga mpambano dhidi ya Fury.
Promota Hearn anasema kwamba kila mmoja anataka kuona mpambano wa Joshua na Fury, akiahidi kwamba atafanya kila awezalo ili lifanyike. “Ikiwa itabidi kupigana na Pulev itabidi tumshinde na ikiwa Fury atatakiwa kupigana na Wilder basi anatakiwa kumshinda tena. Hayo yote yatatokea – Fury atampiga Wilder tena na AJ atampiga Pulev kirahisi kabisa, kisha tutalipata pambano kati ya Fury na AJ,” anasema.
Anasema kwamba Waingereza ni wafalme wa ndondi duniani kwa sasa, kwa hiyo hawana muda wa kupoteza.