Mchezaji bora wa Afrika na kiungo mahiri wa Manchester City, Yaya Toure amedai kuwa kwake mweusi kunamfanya asipewe heshima anayostahili duniani.
Raia huyu wa Ivory Coast anasema kwamba kimsingi anatakiwa kupewa sifa na heshima zaidi, lakini watu wangefanya hivyo angekuwa Mzungu.
Toure (30) ameshafunga mabao 22 msimu huu licha ya kucheza sehemu ya kiungo na uwapo wake kwenye kikosi cha Kocha Manuel Pellegrini huchangia matokeo mazuri sana.
“Kusema ukweli ni kwamba nimekuwa nikitambuliwa, kupewa sifa na heshima na washabiki tu, sitaki kuwa na msimamo mkali wala kuwa hasi, bali nasimamia ukweli tu,” alisema mchezaji huyo aliyepata kukipiga Barcelona kwa mafanikio makubwa.
Hivi karibuni mchezaji mwenzake, Samir Nasri aliyewahi kuchezea Arsenal, alisema kwamba Toure angekuwa ameshatajwa kuwa kiungo bora wa dunia kama hangekuwa anatoka Afrika.
Toure anaamini alichosema Nasri ni sahihi kabisa na kwamba ndiyo hali ya soka iliyopo duniani, ambapo Waafrika wanadharauliwa. Amepata kulalamikia kubaguliwa kwake, ambapo alipata fursa ya kukutana na Rais wa Fifa, Sepp Blatter.
Amefanikiwa kutwaa ubingwa akiwa na timu tofauti katika mataifa manne ya Ivory Coast, Ugiriki, Hispania na England. Alikuwa Barca kwenye kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 2009.
Toure anaamini pia kwamba raia mwenzake wa Ivory Coast, Didier Drogba na Mcameroon, Samuel Eto’o wanashushwa thamani kwa sababu ni Waafrika.