YANGA imewapa raha Watanzania baada ya kuiadhibu Vital’O ya Burundi kwa mabao 2-0 na kufuzu kuingia nusu fainali ya Kombe la Kagame ambako sasa itakutana na Tusker ya Kenya, kesho.
Tusker, ilifuzu kwa mbinde katika mchezo wa awali ilifuzu kwa hatua hiyo baada ya kuilaza kwa penalti 7-6 Rayon Sports ya Rwanda.
Wakenya hao walifunga penalti zao kupitia Ibrahim Shikanda, Osborne Monday, Edward Kauka, Humprey Okoth, John Shikokoti, John Njoroge, Aden Hassan huku Oscar Kadenge akikosa.
Katika mchezo wa Yanga na Vital’O, vijana wa kocha Dusan Kondic walianza kuhesabu bao, dakika ya 11 kupitia kwa kiungo Kigi Makassi baada ya kuunganisha kwa kichwa, mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na Nurdin Bakari aliyeng’ara jana.
Nurdin alipiga faulo hiyo baada ya kiungo Abdi Kassim kufanyiwa madhambi na beki wa Vital’O wakati akielekea langoni.
Dakika ya 20, mshambuliaji Boniface Ambani aliipatia timu yake bao la pili kwa shuti baada ya kupata pasi ya beki Nurdin Bakari.
Lakini, kama ilivyokuwa katika mechi za awali, Yanga walikosa nafasi kadhaa za kupachika mabao kupitia kwao, Shamte Ally, Ambani, dakika za 33 na 40 kwa mshangao wa wengi.
Chipukizi Mrisho Ngassa, ataijutia nafasi ya wazi, dakika ya 75 alipobaki na kipa wa Vital’O, Mubirigi Suleiman, lakini akapaisha na dakika mbili baadaye, kipa Juma Kaseja alifanya kazi ya ziada kuokoa shuti kali la Mbazimutima Henry wa Vital’O na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Baada ya mchezo, Kondic alieleza kuwa amefurahishwa na ushindi kutokana na vijana wake kucheza vizuri na kutengeneza nafasi nyingi, lakini kwa bahati mbaya walizikosa.
Lakini, kocha huyo alishindwa kuzungumzia mechi ya kesho, dhidi ya Tusker kwa maelezo kuwa anaisubiri mechi ya leo.
Naye Younde Kanyankole wa Vital’O aliisifu Yanga kwa kucheza vizuri na kuwazidi vijana wake, lakini alieleza kuwa kukosekana kwa nyota wake wawili kuliidhoofisha timu yake.
Katika mchezo wa awali, hatua ya kocha wa Vital’O, Younde Kanyankole kumwacha benchi beki Erasto Nyoni, kisha wawili walioanza kuwatoa nje kumepokewa na mashabiki kuwa ni kutokana na hasira.
“Huyu amewatoa hao kwa sababu za ‘kiunazi’,” alisikika akieleza shabiki mmoja na kuongeza kuwa ni kutokana na uraia wao, chuki ya kufungwa na Yanga.
Baada ya kutolewa kwao mashabiki waliofurika uwanjani hapo kusikika wakizomea na kupiga miluzi.
Kivutio kikubwa katika mchezo huo kilikiwa ni mashabiki kwa maelfu ambao kwa muda wote wa dakika 90 walionekana wakiishangilia timu yao kwa nguvu wakisaidiwa na matarumbeta.
Hata hivyo, baadhi yao walisikika wakiizungumzia mechi ya leo, kati ya Simba na URA ya Uganda ambayo itafanyika katika Uwanja Mkuu wa Taifa.
Mchezo huo wa kwanza wa nusu fainali unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa na wa aina yake, kutokana na timu hizo mbili kucheza mchezo tofauti.
URA, washindi wa kwanza wa kundi la Morogoro ambao walianza kwa kuichakaza Rayon Sports ya Rwanda kwa mabao 4-1 na kuonyesha safu kali ya ushambuliaji.
Juzi, waliweza kuitimua nje Miembeni ya Zanzibar kwa mabao mawili, huku kocha wao, Mosses Basena akieleza kuwa vijana wake wenye damu changa wataingia uwanjani kusaka ushindi dhidi ya Simba na si kitu kingine.
Basena alieleza kuwa licha ya Simba kuwa na wachezaji wengi wazuri na walioonyesha mchezo wa kasi, lakini vijana wake ambao watamkosa Tonny Mawejje aliyetolewa kwa kadi nyekundu juzi, wamejizatiti hata hivyo kutoa ushindani mkali.
Kutoka kambi ya Simba, hali hadi jana ilikuwa shwari huku kukiwa na kila dalili kuwa makocha, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na bosi wake, raia wa Bulgaria wakiwa makini na kuusubiri mchezo huo kwa hadhari kubwa.
Kuingia kwa Jerry Tegete badala ya Ambani na Athuman Idd badala ya Abdi Kassim kuliongeza uhai kwa Yanga, hata hivyo kosa kosa ziliendelea kama ilivyokuwa awali.
Tatizo hilo, linalipa jukumu benchi la ufundi la mabingwa hao wa Tanzania Bara kujiwekwa vizuri kwa ajili ya mchezo wa nusu fainali dhidi ya Wakenya, Tusker, hasa ikiwa wana ndoto ya kutaka kulitwaa taji hilo.