Yanga jana ilianza ligi kuu ya Bara kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Dodoma katika mchezo mgumu kwenye Uwanja wa Jamhuri ambapo Jerson Tegete alifunga, na kisha kuadhibiwa kwa kutaka kufunga kwa mkono.
Tegete ambaye alionekana kuendeleza makali ya ufungaji aliyomaliza nayo msimu uliopita, aliifungia Yanga goli pekee katika mchezo huo dakika moja kabla ya mapumziko.
Tegete ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa alifunga goli kwa shuti kali baada ya beki wa Polisi Noel Msakwa kuzembea katika kumkaba.
Baada ya kucheza kwa karibu kipindi kizima cha pili bila kuona nyavu kwa mara nyingine, Tegete alikumbuka ‘Mkono wa Mungu’ wa Maradona na kujaribu kuusindikiza mpira wavuni kwa mbinu hiyo katika dakika ya 89, lakini akaishia kuonyeshwa kadi ya njano na muamuzi wa mchezo huo.
Yanga ambayo inawani kuivua Simba ubingwa wa ligi kuu ya Bara baada ya kupokonywa msimu uliopita ingeweza kwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao zaidi kama Athumani Iddi Chuji angetulia katika dakika ya 25 ya mchezo alipobaki na mlinda mlango wa Polisi Salum Kondo.
Sihaba Mathias naye aliikosesha Polisi angalau goli la kufutia machozi baada ya shuti lake kuishia mikononi mwa mlinda mlango wa Yanga Yaw Berko katika dakika ya 39. Kocha wa Yanga Kostadin Papic alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kwa timu yake kutokana na Polisi kucheza vizuri lakini ameridhika na ushindi kwasababu lengo halikuwa kupata mabao mengi.
John Simkoko, mwalimu wa zamani wa timu ya taifa na klabu za Morogoro ambaye amekabidhiwa jahazi la Polisi Dodoma alisifu goli la Tegete na kusema ameridhika na matokeo kwasababu Yanga ilitumia makosa ya vijana wake kuibuka na ushindi.
Timu zilikuwa:
Polisi Dodoma: Kondo Salum, Christian Semsuu, Nahoda Bakari, Noel Mswakwa, Ismail Nkulo, Salmin Kissi, Admin Bantu, Ally Kharid (Mohammed Neto dk.59), Sihaba Mathias (Aman Mbarouk dk.74), Mohammed Seifu, Delta Thomas (John Kanakamfumu dk.49).
Yanga: Yew Berko, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir Haroub, Isaack Boakye, Ernest Boakye, Nurdin Bakari (Godfrey Bonny dk.83), Athumani Iddi, Yahya Tumbo, Jerry Tegete (Iddi Mbaga dk.89), Nsa Job.
Kutoka Arusha, Jimmy Charles anaripoti kuwa Azam nayo ilianza kwa kujikusanyia pointi tatu baada ya kuilaza AFC kwa mabao 2-0. Mabao yote ya Azam yalifungwa na John Boko ‘Adebayor’, katika dakika ya 35 baada ya mlinda mlango wa AFC Aly Mhando kutema mpira wa kona wa Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na katika dakika ya 47 kwa shuti la mbali.
Agrey Moris wa Azam alionyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa mchezo huo.