Wapenzi wa timu ya Young Africans (Yanga) ya Dar es Salaam wameitaka timu hiyo kuacha maringo katika kushiriki michuano ya kuwania Kombe la Mapinduzi Zanzibar ambalo ni kumbukumbu ya siku ya kupata Uhuru wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia uongozi wa timu kupeleka kikosi kisichasikika kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi inayoendelea Uwanja wa Amani Zanzibar.
Yanga inadaiwa kupelekea kikosi cha pili ambacho usiku wa kuamkia Januari 3 , 2012 kilichapwa goli 1-0 na timu dhaifu ya Kikwajuni Zanzibar. Kufungwa huko kumewashtua wapenzi na wanachama wa timu hiyo kwani ni cha dalili mbaya kwa mwaka mpya ikizingatiwa pia kwamba iliaga mwaka 2011 kwa kipigo cha magoli 2-0 kutoka kwa Azam wakati wa mchezo wa kirafiki ambayo kwa sasa iko kundi moja.
Sababu za kupeleka kikosi hicho hazikuwa wazi, lakini ilielezwa kwamba uongozi umeamua kupeleka kikosi hicho ili kuwapa nafasi wachezaji wa kikosi cha kwanza kujiimarisha zaidi kwa michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambapo inatarajiwa kukutana na mafarao wa Misri klabu ya Zamalek.
”Uamuzi huo hauna busara kabisa kwani, timu ingeyatumia mashindano hayo kujipanga vizuri kimataifa na kwa ajili ya ligi kuu inayotarajiwa kuanza mwezi huu”, alisema Hamis Mkude ambaye ni shabiki wa timu hiyo kutoka eneo la Kimanga Dar es Salaam.
”Mazoezi ya timu za Simba na Yanga ni ya kitoto kwani wanafanyia kwenye viwanja vidogo, mashindano kama ya Kombe la Mapinduzi ni mazoezi tosha ambayo yanatakiwa kuzingatia kuliko kudharau”, alisema Zawadi- Jesta Kipiti wa Bima jijini hapa.
Kauli za wapenzi hao wa soka zinatolewa wakati nayo timu ya Simba ikiwaacha wachezaji wake saba kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kuwa majeruhi wengine kuuguliwa.
Hata hivyo simba ambayo ndiyo bingwa mtetezi wa kombe hilo ilitamka awali kwamba itayatumia mashindano hayo kikamilifu ili kulinda heshma yake huku ikijinasibu pia kwamba itajiandaa vizuri kupambana na klabu ya Kinyovu ya Rwanda itakayopambana nayo Februari kuwania kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).
Simba ambayo ipo kundi A linaloshirikisha timu za Miembeni United, KMKM za Zanzibar panoja na Jamhuri ya Pemba ilitarajiwa kutetea ubingwa wake usiku wa kuamkia Januari 4 wakati Yanga ipo Kundi B ikiwa pamoja na Azam ya Tanzania Bara, Kikwajuni na Mafunzo ambayo ilitandikwa magoli 3-1 na Azam.