Wakati msimu ukielekea kumalizika na huku wakijua kuwa wameshavuliwa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uongozi wa Yanga umeanza kumeguka ambapo juzi jioni, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Seif Ahmed ‘Magari’ alitangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo.
Kutokana na kuwa mjumbe, Seif ndiye aliyekuwa akiiwakilisha Yanga katika Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Akizungumzia maamuzi yake ya kujizulu, Seif alisema kuwa ameamua kuachana na kuiongoza Yanga kutokana na kubanwa na shughuli za kifamilia na hivyo, anaona kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuwapisha wengine kuongoza kwa ufanisi.
Seif alisema anaamini kwamba kuendelea kuwa mtendaji kwa wakati huu hakutasaidia kwani hataweza kuitumikia ipasavyo klabu yake, lakini ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wengine waliopo kwani yeye bado ni mwanachama wa Yanga.
“Nimejiuzulu kwa sababu nimebanwa na mambo ya kifamilia, na wala si kwa sababu tumeshindwa kutwaa ubingwa,” alisema Seif, ambaye anatajwa kuwa ni mmoja kati ya vigogo ambao hufanikisha usajili wa wachezaji mbalimbali wa ‘Wanajangwani’.
Jana mchana, mjumbe mwingine pia wa Kamati ya Ufundi, Mashindano na Usajili ya klabu hiyo, Abdalah Bin Kleb, aliwasilisha barua ya kujiuzulu nafasi aliyokuwa akiishikilia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana na kusainiwa na Bin Kleb, imeelezwa kwamba mjumbe huyo amefikia maamuzi hayo kutokana na kukosa ushirikiano na uwajibikaji mbovu wa baadhi ya viongozi wa klabu yake.
Alisema kutokana na hali hiyo, ameona si vyema kuendelea kuwa mjumbe wa kamati hiyo baada ya kutafakari na kuona kuwa uwajibikaji wa wajumbe katika majukumu waliyopewa haukuwa wa kuridhisha; hivyo amemfuata mwenyekiti wake, Seif, katika kujiweka pembeni.
Alisema shughuli za utekelezaji wa majukumu katika klabu hiyo ni mzigo kwa baadhi ya wajumbe huku baadhi ya viongozi wakishindwa kuendesha klabu hiyo na kuiacha ikipoteza dira na mwelekeo wake.
Bin Kleb alisema vilevile kuwa licha ya kujiuzulu kwake, ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu na mkereketwa wa klabu hiyo.
Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga, alisema kuwa hajapokea barua yoyote ya kujiuzulu kwa viongozi hao kwa sababu yuko nje ya nchi kwa shughuli zake binafsi.
Nchunga alisema kuwa mara baada ya kurejea nchini, atakuwa tayari kuelezea kitakachofuata kwa kuitisha kikao cha Kamati ya Utendaji.