Menu
in

Yanga ya ushindi, Simba ya burudani 

Ngao ya Jamii

Ngao ya Jamii

Ni timu mbili zenye miundo tofauti. Ni timu mbili zinazocheza kwa staili ya aina yake. Ni timu  mbili zenye presha kubwa katika soka la Bongo. Ni timu mbili ambazo zinajaribu kuondokana  na ufukara wa kiuchumi kwa kukaribisha wawekezaji na kuunda taasisi imara. Ni timu mbili  zenye mastaa kibao kutoka nje ya nchi. Ni timu mbili ambazo ni kioo cha soka la Bongo. Hizo  ndizo sifa za Simba na Yanga zilizokutana katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambao unafungua  pazia la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa bao pekee la Fiston Mayele aliyepokea pasi kutoka kwa  Farid Mussa. 

Katika mchezo huo Simba walikuwa walewale, wakicheza pasi fupi fupi, kuandaa mashambulizi  kutoka nyuma, kwenda langoni mwa Yanga. Kwa Yanga walikuwa mahiri katika maeneo ya  winga na mabeki wa pembeni. Beki wa kulia Djuma Shaban na winga wa kulia Jesus Moloko  walimsumbua kiasi cha kutosha beki wa kushoto wa Simba Mohammed Hussein, huku SHomari  Kapombe akikumbana na shughuli pevu ya kumzuia winga wa kushoto Farid Mussa na beki  wake Kibwana Shomari. 

Tofauti za timu hizo ni kwamba Simba wanaendeleza falsafa yao ya kuonesha wanachokicheza,  lakini Yanga bado hawaonekani kucheza kitimu kama walivyo wapinzani wao. Yanga waliweka  ukuta mgumu kuanzia safu ya kiungo ambako walikuwepo Khalid Aucho na Yannick Bangala,  kisha kiungo mshambuliaji akakaa Feisal Salum.  

YANGA YA USHINDI 

Wakati pekee ambao Yanga ilikuwa imecheza kwa utulivu ni kipindi cha pili baada ya kuingia  Yacouba Sogne. Kuna pasi 12 mfululizo zilipigwa bila Simba kugusa. Lakini wakati huo tayari  Yanga walikuwa wameshapata bao.  

Yacoube ni mchezaji mzuri kwa vile anaweza kukaa na mpira, kusaidia ulinzi na anapenda  kushambulia akitokea pembeni kushoto. Ujuzi wake katika kushambulia na kuweka mpira katika  himaya yake ni sawa na kile anachokifanya Farid Mussa au Jesus Moloko.  

Uwezo wa Yanga kucheza kwa utulivu kama Simba bado haujafika. Wachezaji wake  wanaonekana wanatafuta namna ya kufahamiana vizuri. Lakini wana silaha kali mno za kuifunga  timu yoyote. Silaha yao ya kwanza ni Feisal Salum, hapo ndipo Yanga ya ushindi inaposukwa. 

Kama sio umahiri wa Taddeo Lwanga kutumwa kazi ya kumdhibiti Fei Toto nadhani Simba  wangepata shida kubwa mno katika mchezo huo. Matokeo ya kazi aliyotumwa Lwanga  yalionekana kwa faulo alizochezewa Fei Toto tangu mwanzo hadi pale mwamuzi Ramadhani  Kayoko alipomlima kadi nyekundu Lwanga ikiwa ni hitimisho lake la kazi chafu alizopewa na  Didie Gomes. 

Silaha ya pili ya Yanga ya ushindi ni mawinga wake wa kulia na kushoto. Nafasi hizo ndizo  zilikuwa zikisisimua kuona shughuli ilivyokuwa ikifanyika kiasi kwmaba benchi la ufundi la  Simba likamtoa Mohammed Hussein. Mo Hussein ni bonge la beki, ameimarisha uwezo na  uzoefu wake una pa faida kubwa.  

Silaha ya tatu ni uwezo wa golikipa Djigui Diarra ambaye anacheza kama makipa wa kisasa.  Djigui anaweza mkubwa kupiga pasi kuwafikia walengwa ili kuanzisha mashambulizi, anacheza  kama sentahafu ikiwemo kuosha hatari langoni mwake. 

Silaha ya nne ni eneo la kiugo wakabaji; Yannick Bangala na Khalid Aucho. Wakati Bangala  anao uwezo wa kupanda mbele kupiga mashuti lango la adui, Aucho anabaki nyuma kulinda  ukuta wake. Mgawanyo wa majukumu hayo unawapa nafasi nzuri Yanga ya kujigawa  kimajukumu. Na endapo timu hii ikicheza kwa utulivu na mwelekeo wa uhakika basi itakuwa  moto wa kuotea mbali.  

Eneo la mwisho ni safu ya ushambuliaji, ambako Fiston Mayele hakuhitaji nafasi nyingi ili  kufunga mabao. Nafasi aliyopata na uamuzi wa haraka aliofanya ulimpatia bao lililowapa  uongozi Yanga. Hii ni aina ya washambuliaji wanaohitaji nafasi chache sana, kisha wanatimiza  majukumu yao. lakini mabailiko yao ya kumwingiza Herieter Makambo ni ujumbe kuwa wanayo  machaguo mazuri katika eneo hilo. 

Udhaifu pekee uliojitokeza ni eneo la ulinzi wa kati, ambalo walimu wana kazi ya kufanya  kuwaambia namna ya kuwazuia wapinzani mapema kabla hawajafika langoni mwao. Kazi ya  namna hiyo pale Yanga hufanywa na Abdalah Shaibu, lakini kutokana na ushindani uliopo  Dickson Job na Bakari Mwamnyeto wanatakiwa kukumbusha kuzuia hatari mapema kabla  haiatokea.  

Vilevile Yanga wanaonekana kukosa beki wa kushoto hali ambayo walimu wanamtumia  Kibwana Shomari ambaye kimsingi ni beki wa kulia. Kwa msimu mzima sio rahisi kutegemea  beki wa bandia ingawa anacheza vizuri, hivyo wanapaswa kuepuka hatari hiyo. Pia wanapaswa  kumwandaa Ramadhan Kabwili na Eric Johora wakati wowote kwa kuwapanga baadhi ya mechi  ili kumpumzisha Djigui na kuimarisha viwango vya eneo hilo. 

SIMBA YA BURUDANI 

Simba wanacheza kwa kujiamini. Wanacheza kama mabingwa. Wanacheza kwa uzoefu.  Maingizo mapya yanaonesha kuwa yanafaa kuziba mapengo ya Luis Miquissone na Cletous  Chama. Ni Simba ileile inayocheza soka la burudani kuanzia kwa golikipa wake anayejiamini  mno Aishi Manula hadi safu ya ushambuliaji.  

Ni kweli Chris Mugalu alikosa nafasi kadhaa, lakini huyu ni mshambuliajihatari ambaye  anaweza kuimaliza timu pinzani wakati wowote. Simba wanapanga mashambulizi kutokea 

nyuma, wanajikusanya, wanawajibika pamoja kuanzia katikati kwenda kushoto,kulia,pembeni na  safu ya ushambuliaji.  

Uzuri ni kwamba Sadio Kanoute ameonesha thamani yake angalau kwa muda mfupi. Kanoute  anajua namna ya kusukuma timu iende mbele,anailinda sambamba na Taddeo Lwanga. Kimsingi  Taddeo Lwanga alifanya kazi chafu zote muhimu na kumfanya Kanoute awe anaelekea lango la adui zaidi kuliko kubaki pembeni yake.  

Kanoute ni mwepesi,ana mshuti,ana muono mzuri, lakini anahitaji muda tu kuchezeshwa kwenye  mfumo wa Simba iwe 4-2-3-1 au 3-2-4-1 na mwingine achaguao mwalimu wao. Hii ni Simba  ileile ya burudani,haijapoteza mwelekeo wake bali wanaonekana kujua wanafanya nini.  Kilichobaki ni mwalimu kuwafanya watekeleze majukumu yao kwa ufasaha. Kinachoweza  kuaangusha ni pale watakaposhindwa kupachika mabao. Timu isipopachika mabao inajiweka  katika shinikizo kutokana na kosa kosa hizo ikiwemo kupungua kujiamini mchezoni. 

MBABE WA NGAO YA JAMII 

Simba imeshindwa kuweka rekodi mpya ya kutwaa taji hilo mara tano mfululizo, baada ya  kulichukua tangu mwaka 2017 hadi 2020. Rekodi zinaonesha kuwa sasa Yanga wameshinda Ngao ya Jamii mara sita. Mwaka 2001 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2002 na 2003 mshindi  alikuwa Simba. Mwaka 2004 mechi hiyo haikuchezwa. Mwaka 2005 mshindi alikuwa Simba.  Mwaka 2006-2008 mechi hiyo haikuchezwa. 

Mwaka 2009 mshindi alikuwa Mtibwa Sugar. Mwaka 2010 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka  2011 na 2012 mshindi alikuwa Simba. Mwaka 2013 na 2014 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka  2015 mshindi alikuwa Yanga. Mwaka 2016 mshindi alikuwa Azam FC. 

Takwimu zinaonesha kuwa Simba na Yanga zimewahi kuchukua kombe hilo mara tatu  mfululizo. Yanga walifanya hivyo mwaka 2013, 2014 na 2015. Nao Simba wakajibu mapigo  kwa kuchukua mara nne mfululizo mwaka 2017, 2018, 2019,2020. Na sasa Yanga wamechukua  taji hilo mara ya sita mwaka 2021.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version