*Wawafyatua Ruvu Shooting 7-0
*Mbeya City hoi, Azam kazi ipo
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania, Yanga ya Dar es Salaam wamefanya mauaji ya sharubela baada ya kuwapiga wanajeshi wa Ruvu Shooting mabao 7-0 katika Uwanja wa Taifa.
Ruvu ndio walikuwa wenyeji wa mechi hiyo na walikuwa wamejigamba kwamba wangeshinda, na kuwataka Yanga watie maji mapema, lakini mambo yaliageukia.
Kocha wao, Tom Olaba alishindwa kukaa kitini na kusimama pia ilikuwa tabu wakati upande mwingine kipa wa Yanga, Deogratius Munisi ‘Dida’ alionesha umahiri wa aina yake langoni.
Yanga ndio kwanza wametoka kuwacharaza Wacomoro jumla ya mabao 12-2 katika mechi zao mbili na wakisubiri Al Ahly ya Misri Machi mosi jijini Dar es Salaam.
Bao saba hazikutarajiwa kutoka kwao kwenye ligi ngumu kama hii, lakini wachezaji wake walijituma na kuirejesha timu kileleni baada ya kufikisha pointi 38.
Yanga wamewapita ‘Wana Lambalamba’ lakini Azam wana mchezo mmoja mkononi Jumapili hii watakapoumana na Prisons walioamka kwenye usingizi wa pono tangu mechi mbili zilizopita wakipata ushindi muhimu.
Yanga walimtumia kwa mara ya kwanza kwenye ligi hii mshambuliaji wao matata kutoka Uganda, Emmanuel Okwi ambaye alicheka na nyavu kama ilivyokuwa kwa Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa na Simon Msuva, hivyo timu kwenda mapumziko zikiwa 4-0.
Yanga walifungua kitabu cha mabao dakika ya kwanza tu na kuwa ishara njema kwa washabiki waliofurika, Kavumbagu akifunga baada ya kupikiwa na Okwi.
Msuva alifunga mpishi wa bao akiwa Ngasa wakati Okwi kufunga kake kulitokana na upishi wa Hamisi Kiiza huku Ngassa akifunga kwa juhudi binafsi.
Yanga walikuwa bado na mabao matatu kipindi cha pili, kupitia kwa Kavumbangu akipikiwa na Msuva.
Kiiza kwa pasi ya Msuva na Msuva mwenyewe akifunga la mwisho
Katika mechi nyingine, wapinzani wakubwa wa Yanga na Azam, ambao ni Mbeya City wamepoteza mechi ya pili msimu huu kwa kukubali kichapo cha 2-0 kutoka kwa Coastal Union ya Tanga, hivyo kuwapa ahueni wababe hao walio kileleni.