*Wafuatiwa na Azam, Mbeya City
*Simba waambulia nafasi ya nne
Ligi Kuu ya Tanzania imetimiza nusu msimu jioni ya Alhamisi hii, kwa Yanga kutwaa uongozi wake.
Macho na masikio ya washabiki wengi yalielekezwa katika Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Chamazi, ambako miamba walikuwa wakitafuta kupata nafasi ya kwanza.
Yanga waliendeleza kasi yao ya hivi karibuni ya kutupia mabao matatu karibu kila mechi, baada ya kuwafunga JKT Oljoro mabao 3-0.
Kwa ushindi huo baada ya mechi 13, Yanga wamejikusanyia pointi 28 na kushika usukani.
Katika mechi zote tangu walipokwaana na Simba na kwenda sare ya 3-3 baada ya kuwa wameongoza 3-0 hadi mapumziko, Yanga wamefunga ama mabao matatu au zaidi, wakiwa chini ya kocha Mholanzi Ernie Brandts.
Azam Complex ndiko timu mbili zilizokuwa juu – Azam na Mbeya City zilipelekeshana na matokeo ya mwisho yalikuwa sare ya mabao 3-3.
Kwa hali hiyo, Yanga wamechupa kutoka nafasi ya tatu hadi ya kwanza, wakifuatiwa na Azam.
Mbeya City wanashika nafasi ya tatu licha ya kutoshana pointi na Azam kwa pointi 27 lakini City wana upungufu wa mabao manne ya kufunga kuliko wana ‘Lambalamba’.
Mbeya City waliungwa mkono na washabiki wengi waliokodi mabasi kutoka Mbeya siku moja kabla kwa ajili ya kushangilia timu ambayo imekuwa mwiba mkali msimu huu ambao ndio kwanza imepanda daraja.
Simba waliocheza Jumatano jioni Dar es Salaam dhidi ya Wauza Mitumba wa Ilala – Ashanti United na kupata ushindi wa mabao 4-2 wanashika nafasi ya nne kwa pointi zao 24.
Washabiki wa Simba walikuwa na homa kabla ya mechi hiyo, huku kukiwa na habari kwamba uongozi wa klabu ulilenga kuwafukuza Kocha Mkuu King Abdallah Kibaden na Msaidizi Jamhuri Kiwelu ‘Julio’ kutokana na mwenendo mbaya wa timu.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alinukuliwa Jumanne ya wiki hii akisema akili yao wote ilikuwa kwenye mechi hiyo na kwamba mambo mengine yoyote yangekuwapo yangefanyika baada ya hapo.
Baadhi ya washabiki wa Simba walikuwa wakilalamikia timu yao kupoteza uongozi wa ligi na kutoka sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa.
Hata hivyo, kocha Kibaden ameeleza kuwashangaa wote wanaolalamika kwa sababu kazi aliyopewa ni kusuka kikosi cha msimu ujao na kwamba hadi alipocheza dhidi ya Yanga hakuwa amepata kikosi cha kwanza.
Washabiki wa Simba walifanya vurugu baada ya mechi dhidi ya Kagera Sugar na kung’oa viti, hivyo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwapiga faini ya Sh milioni 25.
Ligi Kuu iliyo chini ya udhamini wa Vodacom itakuwa katika mapumziko hadi Januari mwakani, kwani ndiyo kawaida ya ratiba ambapo pamoja na mambo mengine hupisha michuano ya kimataifa.
Msimamo wa ligi hiyo kuanzia nafasi ya tano ni Kagera Sugar wenye pointi 20 sawa na ndugu zao Mtibwa Sugar, wakifuatiwa na Ruvu Shooting wenye pointi 17.
Coastal Union wanafuatia nafasi ya nane kwa pointi 16, JKT Ruvu 15, JKT Oljoro 10 sawa na Rhino Rangers na Ashanti lakini hiyo ni kabla ya mechi ya 13 kwa Rhino Rangers.
Ashanti walikuwa wametuama nafasi ya 12 baada ya mechi 13 huku Prisons na wakiwa nafasi ya 13 baada ta mechi 12 na mburuza mkia wakiwa ni Mgambo wenye pointi sita baada ya kukamilisha mzunguko wa kwanza wa msimu huu wa ligi.