HAKUNA ubishi kwamba mashabiki wa Yanga wana hamu ya kuona timu yao ikipepetana na miamba ya Afrika kusini, Mamelodi Sundowns katika mashindano ya CAF. Lakini kiu ya mashabiki wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga watashuhudia kwneye runinga tu timu ya Mamelodi Sundowns ikishiriki mashindano hayo katika hatua ya makundi bila kucheza kwenye dimba mashuhuri la Benjamin Mkapa jijini Dar Es Salaam.
Mashabiki wa Yanga wanaamini kuwa bado hawajamalizana na klabu ya Mamelodi Sundows na hivyo wana kila sababu ya kutamani mtanange wao. Mchuano kati ya Yanga na Mamelodi umekuwa ukiwavutia mashabiki wengi barani Afrika kutokana na Yanga kunyimwa bao la wazi kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa na kuwafanya Mamelodi wasonge mbele ilipofika kwenye mikwaju ya penati msimu uliopita.
Vita kali vya maneno vimekuwa vikitawalka mitandaoni kati ya mashabiki wa Yanga na Mamelodi Sundowns kiasi kwamba kila upande unatamani kuwe na mechi baina yao. Uhalisi wa mambo unaonesha kuwa Yanga ndiyo wanaitamani sana Mamelodi Sundwons. Ni kwamba Yanga wana kiu ya kulipiza kisasi na kuwaonesha Mamelodi Sundowns kuwa walibebwa na mwamuzi wa mchezo msimu uliopita.
Klab za Afrika kusini zimepangwa makundi tofauti, ambapo Yanga wenyewe wametupwa kundi A wakiwa na Al Hilal ya Sudan, TP Mazembe ya DRC. Mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika utachezwa mwezi ujao, ambapo makundi yatatupa karata zao za kwanza kuelekea ubingwa unaoshikiliwa na Al Ahly ya Misri.
Nini siri ya kiburi cha Yanga mbele ya Mamelodi?
Ushindani unaotolewa na klabu za Tanzania kwenye mashindano ya CAF ni siri mojawapao wanayojivunia mashabiki wa Yanga. Timu hiyo ilitoka kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho ambapo ililikosa dakika za majeruhi hivyo kuacha kilio kwa benchi la ufundi lililoongozwa na kocha Nasredine Nabi ambaye kwa sasa yupo Kaizer Chiefs pamoja na wachezaji wake ambao waliamini wangeichapa USM Alger nyumbani kwao.
Katika Ligi ya Mabingwa walikutana na miamba mingi lakini Yanga walisonga mbele hadi walipokwaa kisiki mbele ya Mamelodi. Tangu kuondoshwa mashindano msimu uliopita, si viuongozi wala mashabiki wa Yanga walioridhishwa na ushindi wa Wazulu hao, ndiyo sababu bado wanaamini kuna kazi haijakwisha kati ya Yanga na Mamelodi.
Sifa kubwa wanayojivunia Yanga sasa ni kuwa na kikosi imara na chenye machaguo mengi. Msimu uliopita walimpoteza Pacome Zouzoua aliyeumia goti pamoja na Khalid Aucho ambao hawakuweza kucheza mchezo wao dhidi ya Mamelodi. Kitendo hicho eneo la kiungo ushambuliaji kilipunguziwa nguvu ya ubunifu kwani kazi ilikuwa kwa Aziz Ki pekee huku nyuma yake akiwemo Mudathir Yahya.
Msimu huu Yanga imeongeza usajili katika safu ya ushambuliaji na kiungo mshambuliaji kwa kuwasajili Cletous Chama kutoka Simba na Prince Dube kutoka Azam FC. Usajili huo unawapa jeuri washabiki wa Yanga na kuamini kuwa kazi yao ilikuwa kunyukana na Mamelodi Sundowns. Bahati mbaya CAF wamekuja na ratiba tofauti kiasi kwamba yamebaki matumaini labda watakutana na Mamelodi Sundwons katika hatua zinazofuata. Kwa upande wao Mamelodi Sundowns hawaonekani kuvutiwa kukukutana na Yanga licha ya kubadilisha kocha kwa mpya aliyechukua mikoba ya Rulani Mokwena ambaye amejiunga na Waydad Casablanca.
Wakubwa wanaihofia Yanga?
Kwa ratiba ya CAF iliyotolewa wiki hii inaonesha kuwa Yanga wamenyimwa uhondo wao waliopania katika mashindano hayo kwa kusali sala zote ili wapangwe na Mamelodi Sundowns. Hata hivyo tamaa ya mashabiki wa Yanga kupambana na timu nzuri haiji hivi hivi bali kitu kinachooneshwa na uongozi na wachezaji wao ndani ya dimba. Usajili wao unawafanya watembee kifua mbele na kuamini wanaweza kupangwa na kisha kumshinda mpinzani wao yeyote. Na hapo walipofika Yanga wanafikiria ubingwa wa CAF.
Je, wataweza kunyakua kombe hilo msimu huu? Hilo ndilo linasubiriwa kwa hamu kujibiwa. Bila shaka yoyote timu kubwa barani Afrika hazitapenda kukutana na Yanga kwa kile walichokifanya kwa msimu miwili ya mashindano ya CAF. Jinsi wlaivyozitetemesha USM Alger kwenye fainali na Mamelodi ni dhahiri imekuwa timu ya kuogopeka na wageni hawawezi kuichukulia kama walivyozoea miaka ya nyuma kuwa timu za Tanzania kama dhaifu. Sasa timu zimekuwa miamba na Yanga wanaonesha hilo dhahiri.