Menu
in ,

Yanga wamechelewa kumfukuza Eymael?

Eymael


KLABU ya Yanga imemfukuza kazi kocha wao mkuu Luc Aymael kwa
madai ya kutoa lugha ya kibaguzi dhidi ya mashabiki wao pamoja na
kuvunja sheria za FIFA ibara ya 4 ya Katiba ambayo inakataza vitendo vya
kibaguzi vya aina yoyote ile.


Matamshi ya kocha huyo ni kuwaita mashabiki wa Yanga kuwa ni nyani na
mbwa kutokana na vitendo vyao vya kumpigia kelele amtoe mshambuliaji
Yikpe katika mchezo wao.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari imesema,
“Uongozi wa Yanga umesikitishwa na kauli zisio za kiungwana na za
kibaguzi zilizotolewa na kocha Luc Aymael na kusambaa katika mitandao
ya kijamii pamoja na vyombo vya habari mbalimbali. Kutokana na kauli
hizo zisizo za kiungwana na kiuanamichezo, uongozi wa klabu ya Yanga
umneamua kumfuta kazi kocha Luc Eymael kuanzia leo tarehe 27 julai
2020 na kuhakikisha anaondoka nchini haraka iwezekanavyo,” ilisema
taarifa ya klabu hiyo.


Aidha, imeongeza kuwa, “Uongozi unawaomba radhi viongozi wan chi,
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF),wanachama,wapenzi na
mashabiki wa Yanga, pamoja na wananchi kwa ujumla kutokana na kauli za
kuudhi na kudhalilisha zilizotolewa na kocha Luc Eymael,”

Wakati Yanga ikichukua hatua hiyo, Shirikisho la soka nchini nalo
limetangaza kumchukulia hatua za kinidhamu kocha huyo kutokana na
kauli za kibaguzi alizotoa.


MAKOSA YA LUC AYMAEL NA YANGA

Tanzania Sports
Kocha wa Yanga aliyefukuzwa


Ubaguzi; Hili ni kosa la kwanza kimatendo na maneno kutoka kwa kocha
Luc Aymael. Kosa hili lilionekana mwanzoni kabisa alipoajiriwa

kuifundisha klabu ya Yanga. Kocha huyo alilalamikia kitendo cha mwamuzi
mmoja wa mchezo kumlima kadi ya njano, lakini akataa kupokea mkono
wake. Kocha huyo alilaumu kuwa mwamuzi alibagua kutokana na rangi
yake, kwa kitendo cha kutopokea mkono aliompatia. Kitendo hiki pekee
kilitosha kutoa kengele ya hatari kwa viongozi wa Yanga na mashabiki wao
kuwa timu ipo mikononi mwa mtu mwenye kusababisha taharuki na
ubaguzi. Suala la ubaguzi alilianza mapema sana kwa kumtuhumu
mwamuzi. Ilibidi Yanga walione hili, wachukulie hatua ikiwemo kumpa
adhabu. Bahati mbaya likapita kimya kimya.


Kwa upande wa Yanga, walipaswa kuelewa wanamleta kocha wa aina gani.
Hivyo wangeweza kuepuka taharuki na migogoro isiyo na ulazima kama
inavyoendelea sasa.


Mipaka; moja ya mambo ambayo amekuwa akiyafanya ni kuvuka mipaka
ya kazi yake. mara kadhaa tumesikia kocha huyo kizungumzia mambo ya
ndani ya klabu ikiwemo migogoro ya wachezaji pamoja na fya zao bila
utaratibu maalumu.


Kwake yeye anapopigiwa simu na waandishi wa habari kuulizwa jambo
lolote la Yanga aliweza kutolea ufafanuzi ambao unaibua mgogoro wa
mipaka ya kazi. Hasara ya jambo hili ilikuwa kutokea taarifa tofauti zenye
mkanganyiko kutoka Yanga.


Uongozi ukisema hivi, Kocha anasema vile, msemaji wa timu analeta habari
nyingine. Mkorogo huu ulifanywa huku Yanga wakishuhudia na hili ni kosa
ya Luc Aymael mwenyewe lilipaswa kuonwa na Yanga.


Nakumbuka Barcelona waliacha kumpa kazi Jose Mourinho kutokana na
tabia yake ya kufyuka fyatuka maneno kwenye vyombo vya habari.


Kuropoka mambo ya ndani: Hivi karibuni alinukuliwa akisema, “Kwanza
nimechoka kukaa hii nchi, sina DSTV, sina gari, walinipangishia nyumba

mbaya. Bora hata mniache niondoke tu. Kwa mwendo huu Yanga haiwezi
kushinda chochote. Inakera.”


Mwajiri wako anapofanya makosa au kukiuka makubaliano hatua
inayofuata ni kukabiliana naye ndani kwa ndani. Hili ni jambo ambalo Luc
Aymael angeweza kuzungumza na viongozi, wakanyukana,kulumbana na
kukubaliana au kutokukubaliana ndani humo humo. Lakini kocha kutoka
nje na kuongelea masuala ya mkataba wake hadharani ilikuwa kengele
nyingine ambayo Yanga walitakiwa kuiona.


Kwa upande mwingine licha ya maneno hayo Yanga wanatakiwa kubadilika
na kuheshimu taratribu za mkataba yao na makocha. Kuheshimu vitendo
kazi vya makocha ni sehemu yenye mchango mkubwa wa mafanikio ya
klabu yoyote.


Ni lazima wafanye mambo yaliyo kwenye uwezo wao kuliko kujibebesha
mizigo mikubwa ambayo hawamudu. Siamini kuwa Yanga wanaweza
kukosa gari la kumpa Aymael alitumia katika kazi yake, lakini wanapaswa
kutambua ni sehemu ya vitendea kazi.


FAIDA
Yanga wamenufaika kumwondoa kocha mapema hali ambayo itawasaidia
kumpata mwingine mapema ili aandae timu kwaajili ya msimu ujao. Faida
ya kuwawahi kumfukuza Aymael inawapa nafasi na muda wa kuajiri kocha
wa kuingia na timu msimu ujao.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version