Menu
in

Yanga waleta ‘kiarabu’, Simba yatandikwa mbele ya Rais Samia

Yanga FC

BAO la kiungo mkabaji wa Yanga, Zawadi Mauya limeibebesha kipigo cha 38 kwa mabingwa  watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara klabu Simba katika historia ya soka baina ya miamba hiyo tangu  mwaka 1965, na ukiwa mchezo wa kwanza kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Samia Suluhu Hassan. 

Ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Yanga walikianza kipindi cha kwanza kwa  utulivu na kutafuta namna ya kuipenya gome ngumu ya Simba na yenye uzoefu mkubwa katika  mechi zenye presha chini ya Pascal Wawa na Joash Onyango Achieng. 

Ushindi wa Yanga ulipatikana ndani ya dakika 13 za mchezo ambapo ilifanikiwa kuandika bao la  kuongoza kwa shuti kali la Zawadi Mauya ambaye alikuta mpira uliokuwa ukiambaa ambaa nje ya 18.  Tangu mwanzo wa mchezo huo Simba na Yanga zilionekana kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu,  huku zoyte zikifanya majaribio kadhaa. 

Takwimu zinaonesha kuwa Simba imepoteza mchezo wa 38 mbele ya Yanga tangu mwaka 1965,  ambapo Yanga imeshinda mchezo wa 38 katika mechi 106 walizokuitana miamba hiyo. 

Timu zote mbili zimekutana mara 106, Simba wameshinda mechi 31 na kufungwa 38, kutoka sare 37  na kuibuka na pointi 130. Watani wao Yanga wamecheza mechi 106, wameshinda michezo 38,  kutoka sare mechi 37,kupoteza mechi 31 na kuvuna pointi 151. 

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilionesha ufundi na ushindani wa makocha na nidhamu ya mchezo  wa timu zote mbili. Kocha wa Yanga alipanga viungo wawili wakabaji, Mukoko Tonombe na Zawadi  Mauya, huku kiungo mshambuliaji akiwa Feisal Salum maarufu kama Fei Toto. Upande wa kulia  alicheza Tusila Kisinda, wakati ule wa kushoto alisimama Deus Kaseke, na safu ya ushambuliaji  ikiongozwa na Yacouba Sogne. 

Simba ilianza na viungo wawili wakabaji, Taddeo Lwanga na Erasto Nyoni, kuhusu safu ya kiungo  washambuliaji wakipangwa Luis Miquissone,Cletous Chama ambao ubora wao huwapa uhuru  mabingwa hao. 

Tofauti za Simba na Yanga zilikuwa katika namna ya kucheza mbali ya nidhamu walizokuwa  nazo.kipindi cha kwanz akilionesha namna Yanga walivyotulia na kuonana vizuri, huku wakitegemea  upande wa Tuisila Kisinda kuichachafyua ngome ya Simba. Palikuwa na kosa kosa kadhaa ambazo  kama si umahiri wa kipa wa Simba Aishi Manula huenda nyavu zake zingetikiswa zaidi. kwa ujumla  kipindi cha kwanza kilikuwa kizuri kwa Yanga ambao walionesha nidhamu,ufundi na umahiri wa hali  ya juu uliowapatia bao la kuongoza.  

Kipindi cha pili kilikuwa cha kushambuliana kwa zamu, lakini Simba walikuwa na nafasi nzuri na  walionesha mabadiliko. Hata hivyo kama si umahiri wa mlinda mlango wa Yanga Farouk Shikalo huenda Simba wangesawazisha bao hilo.

Shauku ya kuibuka mshindi na ugumu wa ngome ya Yanga, ulisababisha kocha wa Simba Didier  Gomes aingize washambuliaji wawili Chris Mugalu na Meddie Kagere kama njia ya kutaka kuipenya  ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya Dickson Job na Bakari Mwanyeto.  

KIPIGO CHA KWANZA 

Simba kwa mara ya kwanza wamefungwa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan. Huo ulikuwa mchezo  wake wa kwanza kuhudhuria kwenye dimba la Benjamin Mkapa. Rekodi zinaonesha kuwa Yanga  hawajawahi kufungwa Kwa Mkapa kama mechi inahudhuriwa na Rais. Kwahiyo hiki ni kipigo cha  kwanza cha Simba katika utawala wa serikali ya awamu ya sita na ushindi wa kwanza wa Yanga katika  serikali hiyo. 

UBORA WA MCHEZO 

Mechi hii inabaki kwenye kumbukumbu za washabiki kuwa moja ya michezo maridhawa. Ni mchezo  uliowapatia burudani pande zote, kimbinu,uwezo na ufundi wa walimu wa timu zote mbili. Mabeki  wa timu zote mbili walionesha uhodari, viungo hali kadhalika, lakini sehemu pekee ambayo Simba  ilishindwa kupata jawabu ni pale Cletous Chama na Luis Miquissone walipodhibitiwa. Viungo  washambuliaji wawili hao ni silaha muhimu ya Simba katika mechi zao, lakini walishindwa kuipenya  ngome ya Yanga, huku mashuti yao yakitoka nje ya lango.  

YANGA WALETA STAILIYA KIARABU 

Yanga wanaonekana kuleta ladha ya soka ya kiarabu. Inafahamika soka la waarabu mara nyingi  wanapenda kucheza na mwamuzi pamoja na kuwazidi maarifa wapinzani wao. Mbinu yao huwa ni  kutafuta faulo kadiri wanavyoweza. Kwa dakika 45 Simba walionekana kutong’amua hilo na hivyo  walijikiuta wakifanya faulo nyingi.  

Nahodha wao John Bocco alionywa mara nne na mwamuzi wa mchezo huo, baada ya kufanya faulo  mara kwa mara dhidi ya Yanga. Kama ningepewa nafasi ya kuchagua neno la kiingereza kuelezea  mbinu hiyo ningesema ‘tricks’ zilizotu,iwa na Yanga ni kujiangusha na kutafuta faulo ambazo ziliishia  kuwachanga Simba na wengine kuadhibiwa kwa kadi za njano.  

Ndiyo maana walijikuta wakishaangaa aina ya faulo walizopata Yanga na ikawa inawapa nafasi ya  kupoteza umakini na kuhofia adhabu kutoka kwa mwamuzi. Kwa hili Yanga walicheza staili ya  kiarabu kujiangusha angusha na kuwachanganya Simba. Nabi alicheza mchezo kisaikolojia zaidi. 

Kipindi cha pili kilikuwa mali ya Simba lakini hawakufua dafu hivyo hadi dakika 90 za mchezo  wakijikuta wakibanduliwa na mabingwa wenzao wa zamani.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version