Menu
in , ,

YANGA WALAZIMISHWA SARE

Yanga wakiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam jioni hii wamelazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Al-Ahly kwenye mchezo wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika.

Al-Ahly ndio waliokuwa wa kwanza kuandika bao kwenye dakika ya 11 kupitia kwa Amr Gamal aliyefunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa krosi iliyotokana na mpira wa adhabu baada ya Vincent Bossou kumchezea madhambi Ramadhan Sobhi nje kidogo ya eneo la hatari.

Bao hilo liliwaamsha vijana wa Jangwani ambapo walipeleka mashambulizi kadhaa langoni mwa Al-Ahly na kusababisha bao la kusawazisha alilojifunga Ahmed Said akijaribu kuokoa krosi kali ya Yousouf Boubacary mnamo dakika ya 18.

Yanga wakaendeleza mashambulizi kadhaa ya hatari baada ya kupata bao la kusawazisha huku Al-Ahly wakicheza kwa tahadhari zaidi na kutumia mbinu za kupoteza muda. Golikipa Sherif Ekramy wa Al-Ahly akaoneshwa kadi ya manjano ndani ya dakika ya 33 kwa kuchelewesha muda makusudi.
IMG_5047_1

Dakika 45 za kwanza za mchezo zikamalizika matokeo yakibaki kuwa sare ya bao moja kwa moja ndani ya dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam.

Al-Ahly wakazianza dakika 45 za kipindi cha pili kwa shambulizi kali kupitia kwa Momen Zakaria aliyemchambua Haji Mwinyi na kupiga shuti lililogonga mwamba.

Heka heka uwanjani

Yanga wakaonekana kupotea kwa takribani dakika 20 za mwanzo za kipindi cha pili kwa kuwa vijana wa mwalimu Martin Jol waliwadhibiti vyema na kuwanyang’anya mpira mara moja kila walipojaribu kuanzisha mashambulizi.

Jitihada za Yanga kujaribu kutafuta ushindi kwenye Uwanja wa nyumbani zikagonga ukuta pale mwamuzi Denis Dembele kutoka Ivory Coast alipopuliza kipenga cha kuashiria kumalizika kwa mchezo huo.

Mchezo wa marudiano utapigwa tarehe 18 mwezi huu kwenye dimba la ‘Cairo Stadium’ huko jijini Cairo. Ikumbukwe timu itakayoiondosha nyingine kwenye hatua hii itaingia kwenye hatua za makundi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version