Dhamira ya Yanga kusherehekea ubingwa wa Bara kwa kuwafunga Simba imetimia kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kuwanyoa mahasimu wao hao kwa mabao 2-0 katika mchezo wa kufunga msimu ulioacha matukio ya aina yake kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza walifunga kila kipindi kwa Yanga katika mechi ya wikiendi hii na kutimiza utabiri wa muda mrefu, kwamba kikosi hicho cha Jangwani kilikuwa bora kuliko kikosi cha Simba chenye mchanganyiko wa vijana na wakongwe.
Yanga waliotwaa ubingwa kabla hata ya kumalizika msimu, walipania kushinda mchezo huo ili kunogesha sherehe za ubingwa wao waliokabidhiwa Jumamosi hii na kitita cha Sh70 milioni kutoka kwa wadhamini, Kampuni ya Simu ya Vodacom.
Kipigo hicho kinawaacha Simba nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi na kutwaa zawadi ya Sh25 milioni, wakimaliza msimu kwa pointi 15 nyuma ya mahasimu wao Yanga waliofikisha pointi 60 baada ya ushindi wa jana.
Mchezo huo ulivunja rekodi kwa kujaza mashabiki wengi, Simba itabidi wajilaumu wenyewe kwani mabao waliyofungwa yalitokana na uzembe wa mabeki wao waliowaruhusu washambuliaji wa Yanga kuucheza mpira wakiwa huru ndani ya eneo la hatari.
Kiiza nusura awape uongozi Yanga dakika ya 21 baada ya kuunasa mpira uliochezwa vibaya na beki wa Simba, Shomari Kapombe lakini akajikuta akipiga shuti ‘cha mtoto’ na pia alikosa bao kwa shuti lake kutoka nje dakika ya 35.
Mrisho Ngassa nusuru afunge bao kwa Simba dakika ya 51 kama si shuti lililotoka nje ya uwanja baada ya kutengenezewa pande na Felix Sunzu, huku Simon Msuvu wa Yanga akikosa bao dakika ya 56 baada ya mpira wake wa kichwa kutoka nje kidogo ya lango la Simba.
Kiungo wa Simba, Amri Kiemba naye aliendeleza mlolongo wa kukosa mabao, kwani dakika ya 60 shuti lake ‘lililozaliwa’ na pasi Ngassa lilikosa shabaha langoni mwa Yanga na kuruka juu.
Dakika ya 85 lilitokea tukio la kushangaza na mpira kusimama kwa muda baada ya kiki kali ya adhabu ndogo ya Nizar kuchezwa na Kaseja kwa mpira na kugonga mwamba kabla ya kurudi na kumpiga kichwani kipa huyo wa Simba na kulazimika kulala chini kwa muda.
Aidha, dakika ya 90 mpira ulisimama kwa muda baada ya mwamuzi, Martin Saanya wa Morogoro kupigwa ngumi kwa bahati mbaya na kuchanika sehemu ya karibu na jicho na beki wa Simba, Cholo aliyekuwa kwenye mzozo na mshambuliaji wa Yanga, Kavumbagu.
Vilevile, mashabiki wa wiwili wa Yanga walipewa huduma ya kwanza baada ya kuzimia kutokana na kuzidiwa na furaha ya ushindi wa timu yao, huku Ngassa wa Simba anayeelezwa kurudi Yanga msimu ujao, akivalishwa jezi ya Wanajangwani hao na kuzungushwa uwanjani akiwa amebebwa na mashabiki.
Aidha, katika mechi hiyo, ulinzi ulikuwa mkali kwani hakuna magari yaliyoruhusiwa kuegeshwa eneo la maegesho ya magari ndani ya uwanja huo tofauti na inavyokuwa kwenye mechi zingine.
Sababu kubwa ya kuimarisha ulinzi imeelezwa kuwa ni hofu ya matukio ya kigaidi.
Iliwachukua Yanga, dakika nne tu kuandika bao la kwanza likiweka kimiani na Kavumbagu aliyeruka juu na kupiga kichwa mpira mbele ya msitu wa mabeki wa Simba na kumshinda kipa namba moja, Juma Kaseja.
Kiiza alifunga bao la pili dakika ya 64 kwa shuti la kugeuka ndani ya boksi la hatari baada ya mabeki wa Wekundu wa Msimbazi kuchelewa kuucheza mbali mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twite.
Musa Mudde angeweza kufanya matokeo kuwa 1-1 kipindi cha kwanza kama si kupiga penati ya ‘ajabu’ iliyokwenda moja kwa moja kumlenga kipa wa Yanga Ali Mustapha, baada ya Nadir Haroub kumkumbatia Ngassa ndani ya eneo la hatari dakika ya 27.
Hii hiyo ni mechi ya 101 kwa timu hizi kukutana katika michuano mbalimbali, na kati ya hizo, Yanga ilishinda mara 38, Simba mara 32, huku mara 31 zikitoka sare. Zaidi ya hapo, Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara 23 wakati Simba imefanikiwa kunyakua taji hilo mara 18.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig alikubali matokeo na kusema, Yanga walistahili ushindi kwa vile kikosi chao kilikuwa bora kulinganisha na kikosi chake ambacho, amesema kina miezi miwili tu tangu akitengeneza upya.
Kwa upande wake, Ernest Brandts wa Yanga alisema alikiandaa kikosi kwa ajili ya ushindi jambo ambalo limetimia na amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza kwa kujituma na kupata ushindi.
Yanga waliwakilishwa na Bartez, Mbuyu/Juma Abdul, David Luhende, Haroub, Yondan, Chuji, Msuva, Domayo, Kiiza/Nizar Khalfan, Kavumbagu, Niyonzima
Kikosi chaSimba kilikuwa na akina Kaseja, Cholo, Haruna Shamte, Kapombe, Mudde, William Lucas, Mwinyi, Abdallah Seseme/Sunzu, Ngassa, Kiemba/Jonas Mkude, Haruna Chanongo/Ramadhan Singano.