*Je Yanga watagomea hafla ya zawadi?
Klabu mbili kubwa nchini, Yanga na Simba zimeanika program zao za kujifua, wakati mipango ya usajili ikiendelea bado kwa klabu nyingi.
Wakati Simba wameanza kuwajaribu wachezaji wapya na wengine wanaowaniwa kusajiliwa msimu huu, Yanga wanatarajia kuanza mazoezi rasmi wiki hii, baada ya kocha wa Ernie Brandts kutarajiwa kurejea kutoka kwao Ulaya.
Simba walio chini ya kocha Abdallah ‘King Mputa’ Kbaden wanafanya mazoezi yao kwenye Uwanja wa Kinesi, Barabara ya Shekilango wakati Yanga wanatarajiwa kujifua katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola.
Wachezaji wapya ambao Simba inawatazama bado kabla ya kufikia uamuzi wa kuwasajili au la, ni Issa Rashid wa Mtibwa; Zahoro Pazi wa JKT Ruvu; Sino Agustino wa Prisons na Adeyoon Salehe wa Miembeni.
YANGA NA MGOMO WA HAFLA YA ZAWADI
Wakati hayo yakijiri, Mabingwa wa Soka wa Tanzania, Yanga wameendelea na msimamo wao wa kugomea hafla ya kukabidhiwa zawadi iliyopangwa kufanyika wiki hii.
Yanga wameiandikia rasmi Kamati ya Ligi inayoongozwa na Wallace Karia, ikieleza kutoridhishwa kwao na zawadi kushikiliwa muda mrefu tangu kumalizika kwa ligi Mei mwaka huu.
Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto naye alisema ni fedheha kwa waandaaji na wadhamini kufanya hivyo, kwa sababu walistahili kulipwa chao mapema kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, na kwamba huo ni ubabaishaji.
Hata hivyo, Karia anasema kwamba kugomea zawadi ni utovu wa nidhamu na kwamba kama hawatakwenda, hawatawapelekea bali wenyewe Yanga watazifuata watakapojua.
Alionekana pia kubeza uamuzi huo wa Yanga, akisema si hafla maalumu kwa ajili ya Yanga tu, bali ni kwa wachezaji bora, wenye nidhamu, wafungaji bora na mabingwa wanajumuishwa hapo pia.