Klabu ya Yanga SC inarejea tena kwenye dimba la Benjami Mkapa, kusaka tiketi ya kuona kama wataweza kwenda hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Yanga SC wikiendi hii siku ya Jumamosi itakuwa na kibarua kizito mbele ya CR Belouizdad ya Algeria katika mchezo wa makundi ambao utakuwa ni kama vita kwani kila timu inamtazama wenzake kama mchezo pekee wa kufuzu kwenda robo fainali.
MSIMAMO WA KUNDI
Kundi ‘D’ linajumuisha timu ya Al Ahly ya Misri, CR Belouizdad ya Algeria, Yanga SC ya Tanzania, pamoja na Medeama FC ya Ghana. Katika kundi hili timu ya Al Ahly inaongoza ikiwa na alama 6, CR Belouizdad inafuata na alama 5, Yanga SC alama 5, Medeama FC alama 4, yenyewe ikiburuza mkia. Kinachoitofautisha Yanga SC na CR Belouizdad, ni ule mchezo wao wa kwanza ambao Yanga ilikubali kichapo cha mabao matatu ugenini nchini Algeria mbele ya Belouizdad na kuipa mlima mzito vijana wa Jangwani.
SAFARI YA YANGA
Ilikuwa Novemba 24 pale Yanga SC ilipoanza kuichanga karata zake kwenye michezo ya hatua ya makundi mchezo dhidi ya CR Belouizdad, hakuwa mchezo rahisi kwa Yanga kwani walipoteza kwa kipigo kizito cha mabao 3-0, na kupelekea viongozi kuanza kukuna vichwa. Mchezo ule Yanga ilionekana kutawala zaidi mchezo kuliko mwenyeji wake lakini kwenye mchezo wa mpira wa miguu kinachotazamwa zaidi ni matoke na siyo kitu kingine. Possession 58% kwa 42, haikuwafanya Yanga kuondoka na alama tatu. Mashuti ya kulenga goli 11 kwa 10 pia haikuwa kigezo kwa Yanga kutamba mbele ya waarabu hao. Dakika ya 10′ Benguit aliipa CR Belouizdad bao la utangulizi kisha dakika ya 45+2′ Meziane alifunga bao la pili na baadae Jallow, alifunga kalamu ya mabao kwa kuitandika Yanga SC bao la tatu mnamo dakika ya 90+4′ ya mchezo.
JUMAMOSI KIVUMBI
Wageni wa Yanga ambao ni CR Belouizdad, siku ya jana (Jumatano) aliwasili nchini salama tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi. Baadhi ya viongozi wa Belouizdad wameinguzungumzia hali ya hewa na kudai Dar es Salaam kuna joto Kali tofauti na ilivyo kwao lakini wamejipanga kupambana na hali yoyote dhidi ya mpinzani wao. Timu ya CR Belouizdad imeshusha nyota wake wote akiwemo Abdelraouf Benguit ambaye anatajwa sana kuwa mwiba mkali kwa Yanga SC. Kuhusu majeruhi, viongozi walishindwa kuweka wazi suala hilo na limebaki kama siri ya kambi.
HOMA YA MCHEZO
Hali inazidi kupamba moto na hata lile joto la mchezo ni kubwa na kwa hali ilivyo unaweza kudiliki kusema, huu mchezo hauna tofauti na mechi ya derby ya Kariakoo ambao hua inachukua shughuli zote za wakazi wa hapa Dar es Salaam na kusubiri mpaka mchezo huo kupita. Hamasa ni kubwa kwa viongozi wa Yanga chini ya Afisa habari wake Ali Shaban Kamwe, ambaye amejaribu kuhamasishi kila kona huku akiyatumia matawi mbalimbali ya klabu hiyo. Mfano mdogo siku ya jana (Jumatano) viongozi hao walikutana Mbagala Kwa ajili ya hamasa ya mchezo huo wa Jumamosi dhidi ya CR Belouizdad.
YANGA WANAJIAMINI
Kitendo cha kuifunga Polisi Tanzania mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam ‘ASFC’ imewapa hali ya kujiamini na kuona kama kila kitu kinawezakana, mchezo huo ambao ulipigwa kwenye uwanja wa Azam Complex, Yanga SC iliweza kuchomoza na ushandi wa mabao 5-0, mbele ya Maafande hao kutoka Mkoani Kilimanjaro huku mshambuliaji wao Joseph Guede aking’aa kwa kufunga mabao mawili na kuwapa matumaini mashabiki walioanza kumkatia tamaa kutokana na ukame wa yeye kutozifumania nyavu za wapinzani wake. Katika ushindi huo utamsifu sana winga Augustine Okrah the Magic ambaye alijua kuzitumia nafasi na uhodari wake wa kukimbia kwa kasi kisha kumtengea Guede na kumfanya afunge mabao hayo. Mashabiki wa Yanga kutoka Kona mbalimbali hususani mikoani tayari wameshaanza safari ya kuja Dar es Salaam tayari kwa kuipa nguvu timu yao siku hiyo ya Jumamosi kwenye dimba la Benjami Mkapa.
UWANJA WA MKAPA
Dimba la Benjami Mkapa lipo tayari kuupokea mchezo huo wa Yanga SC dhidi ya CR Belouizdad, awali uwanja huo ilitoka taarifa kutoka wizara ya michezo kwamba, ungefungiwa tena ili kupisha matengenezo kadhaa na timu zingetafuta viwanja vingine kwa michezo yao mbalimbali. Habari njema kutoka huko huko Wizarani ni ruksa kwa michezo ya Kimaitafa kwa vilabu vya Simba na Yanga kuutumia uwanja huo huku marekebisho yakiendelea.