Menu
in , ,

YANGA NA MTIBWA, KONDOO ALIYETOKA USINGIZINI NA KONDOO ALIYE MALISHONI

Tanzania Sports

Hakujawahi kuwa na wepesi wa aina yoyote kipindi ambapo Mtibwa inapokuwa inacheza na Yanga au Simba.

Haijalishi uwanja utakaotumika kwa ajili ya mechi hiyo lakini ugumu wa mechi hiyo utaonekana wazi.

Mtibwa ametoka kucheza na Simba katika mchezo wa ngao ya jamii mchezo uliopita na Yanga wametoka kucheza dhidi ya USM Algers katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika.

Matokeo ya mechi zilizopita zitakuwa na nguvu ipi katika kuamua mechi ya Leo ?

Mechi iliyopita Mtibwa alifungwa na Simba (2-1) katika mchezo wa kuwania ngao ya jamii, wakati Yanga wakishinda goli 2-1 dhidi ya USM Alger’s.

Matokeo haya yanaweza kuwa na nguvu katika maamuzi ya mechi ya leo katika maeneo yafuatayo.

Kama Mtibwa watakuwa wanaendelea kukumbuka kipigo dhidi ya Simba jumamosi iliyopita kutawafanya wawe na mchezo mgumu kwao.

Ila kama watayachukulia matokeo yaliyopita katika mtazamo chanya, na kusahau kila kitu kuhusiana na matokeo hayo basi watakuwa na nafasi nzuri ya kupigana kwa ajili ya kupata alama katika mchezo wa Leo.

Yanga walishinda mechi iliyopita, matokeo ambayo wanatakiwa kuyachukulia kama ongezeko la nguvu kwao katika kupigania kwenye kila mechi. Kosa kubwa ambalo watalifanya ni wao kubweteka na ushindi wa jumapili iliyopita dhidi ya USM Alger’s kwa sababu wataingia uwanjani kwa kuwaangalia Mtibwa kama Underdogs.

Kuna faida gani kama Mtibwa wataonekana kama Underdogs katika mchezo wa Leo?

Kama Mtibwa watakubali kupokea hali ya wao kuwa underdogs itakuwa na faida kubwa sana kwao kwa sababu itawafanya wawe makini, umakini ambao utawapa utulivu katika kufanya maamuzi mbalimbali ndani ya mchezo.

Umakini huu utawafanya Yanga waonekane kama wamepania kwa sababu watataka kuonesha kuwa wao kwenye hii mechi ni wakubwà na wanataka kuonesha ukubwa wao kwa kuwafunga Mtibwa.Hivo kupania kwao kunaweza kuwaondolea utulivu na umakini katika kufanaya maamuzi uwanjani.

Yanga ni Kondoo aliyeamka ?

Amekuwa kwenye matatizo makubwa sana kuanzia msimu uliopita. Matatizo ambayo yamemfanya asiwe na matokeo mazuri ndani ya uwanja. Lakini katika mechi dhidi ya USM Alger’s alionekana kama ameamka kutoka usingizini.

Hali hii inaweza kuwa na faida na hasara kwao. Kwanini nasema hivi?

Yanga wakiingia uwanjani kwa minajili ya kuwaonesha mashabiki wao kuwa wameamka na wako tayari kwa ajili ya vita itakuwa na hasara kwao kwa sababu watapania mchezo, madhara ya kupania mchezo ni timu kukosa utulivu katika maamuzi uwanjani.

Lakini Yanga wakiingia kawaida na kwa utulivu katika mechi hii itawasaidia kuonesha kuwa wameamka kwa ajili ya ushindani.

Mtibwa ni kondoo aliyemalishoni tayari?

Tangu msimu jana wameonesha wana kikosi chenye ushindani na kikosi chao hakijabadilika sana. Kikosi chao kinaonesha kuwa wao tayari wameshaingia malishoni muda mrefu kwa sababu ya kutokuwa na mabadiliko makubwa katika kikosi chao ambacho kilifanya vizuri msimu uliopita.

Kuondoka kwa Hassan Dilunga kutakuwa na pengo kwa Mtibwa?

Hapana shaka alikuwa mchezaji muhimu sana msimu uliopita. Umuhimu ambao ulisababisha Mtibwa kubeba kombe la TFF.

Mtibwa wanatakiwa kutengeneza mfumo ambao utaiwezesha timu kucheza kwa pamoja ili kuondoa hali ya wao kufikiria kuwa Hassan Dilunga hayupo uwanjani tena upande wao.

Kutoka kuwa na Chirwa mpaka kuwa na Makambo….

Msimu uliopita Obrey Chirwa alikuwa mfungaji bora wa kikosi cha Yanga, alikuwa ameuzoea mpira wa Tanzania ndiyo maaana alikuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Yanga.

Leo hii wana Makambo, ambaye anaonekana ana uwezo mkubwa wa kufunga. Ongezeko lake pamoja na Deus Kaseke linaweza kuwa na tija katika kikosi cha Yanga.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version