*Timu 10 hazichekani, yoyote yaweza kushuka
*Mechi za Azam dhidi ya Simba, Yanga muhimu
Ligi Kuu Tanzania Bara inaelekea ukingoni, timu nyingi zikiwa zimebakiza mechi nne na chache zikiwa zimebakiza tano, huku Yanga wakiwa vinara kwa tofauti ya pointi saba.
Yanga wanafuatiwa na Azam wenye pointi 42 na Simba wenye pointi 35 na wote, pamoja na Mgambo Shooting wa Tanga wameshacheza mechi 22, wakati timu nyingine zote zimecheza mechi 23.
Mwelekeo wa matokeo ya mechi ya karibuni ya ushindi kwa Yanga yaliendelea pia Jumanne kwa Vijana wa Jangwani kuwafunga Stand United ya Shinyanga 3-2 na kuwaweka Yanga katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa.
Kadhalika kudorora kwa Azam ambao walipoteza mserereko wa ushindi na kuishia kufungwa na kisha kwenda sare kumewasaidia pia Yanga ambao ndio wawakilishi pekee wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.
Azam watakuwa wanawaombea Yanga wateleze kwenye mechi zilizobaki, lakini wanahitaji poi9nti sita tu kutangazwa mabingwa, kwa maana hiyo kuwapokonya Azam ubingwa walioutwaa msimu uliopita.
Yanga waliokwenda sare ya 1-1 na Etoile Du Sahel wa Tunisia Jumapili iliyopita, walicheza chini ya kiwango dhidi ya Stand United na nusura wapoteze mchezo kama si jitihada binagsi za baadhi ya wachezaji na pia makosa ya wachezaji wa Stand.
Ilivyokuwa ni kwamba kulikuwa na mabadiliko kwa wachezaji wa nyuma wa Yanga, ambapo baadhi waliocheza Jumapili walipumzishwa na wengine walikuwa majeruhi, namba tano aliyezoeleka, Nadir Haroub na pacha wake Kelvin Yondani.
Kadhalika kipa Ali Mustapha hakuwa golini na badala yake alikuwapo Deogratias Munishi ambaye alicheza na mabeki wasiozoeleka kama Saidi Makapu, Rajab Zahir na Mbuyu Twite aliyezoeakucheza kama kiungo mkabaji huku pembeni wakiwa wa kawaida Oscar Joshua na Juma Abdul.
Ni hali hiyo ya wachezaji ambao hawajakuwa pamoja karibuni walishindwa kuelewana na kuruhusu mabao mawili ambayo si kawaida kwa Yanga kuruhusu. Yanga wamefungwa mabao machache zaidi katika ligi hii (14) na wamefunga mengi zaidi (42), baadhi yakitokana na yaliyovunja rekodi dhidi ya Coastal Union waliobugizwa 8-0.
Simba walioanza ligi vibaya kwa sare kiasi cha kumfukuza kocha wao, Patrick Phiri walikuja kuzinduka lakini bado hawajajiweka pazuri, na watategemea kuanguka kwa Azam au Yanga kwenye mechi zao tano zilizobaki ili nao wapate nafasi kucheza mechi za Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Vinginevyo mabao ya Azam ya kufunga ni machache (29) na pia ya Simba (27) wakati wanaoshika nafasi ya nne wakiwa na pointi 31, Kagera Sugar wamefunga maba 22 ikilinganishwa nay ale 42 ya Yanga, wakiwa pia na mchezaji anayeongoza kwa kufunga mabao 14 – Simon Msuva.
Kwa kuangali katika jicho lingine ni kwamba hata ikitokea Azam au Simba wakafanikiwa kwenda sawa kwa pointi na Yanga hadi mechi za mwisho, Yanga watakuwa na faida kubwa katika hazina yake ya mabao kwa maana ya uwiano wa kufungwa na kufunga.
Hadi Jumatano hii Yanga wana uwiano wa mabao 28 mara mbili ya Azam wenye 14, Simba wenye 10 na Kagera Sugar wenye sifuri ikimaanisha mabao ya kufunga ni sawa na waliyofungwa, nayo ni 22 kila upande.
Kutoka hapo, timu nyingine zinazofuata hadi ile inayoshika mkia zina uwiano hasi wa mabao, ikianzia -1 hadi -8.
Pamekuwapo tetesi za kushangaza hivi karibuni pia kwamba baadhi ya klabu hufanya makusudi kutoshinda mechi zao, zikihofia gharama iwapo zitatwaa ubingwa au kushika nafasi ya pili.
Zipo timu zinazoelezwa kwamba zipo kwenye ligi kwa minajili ya kutangaza bidhaa za kampuni zinazozimiliki au zile zinazozidhamini lakini hazingependa kuona zikifanya vyema na kwenda mbele kwenye michuano ya Afrika.
Wakati Yanga wakipewa nafasi ya ubingwa sawa na Chelsea walivyo hapa London, Azam na Simba wanawaombea mabaya kama Arsenal na Manchester United wanavyowaombea Chelsea na kwa hakika kila mtu atavuna alichopanda.
Yanga na Chelsea wamejua kwamba biashara ni asubuhi na jioni ni hesabu ya mapato na matumizi na pia wanaepuka shinikizo baya la dakika za mwisho. Hata hivyo, Yanga bado wana mechi na Azam, ambapo rekodi yao kwao si nzuri na Simba wana mechi na Azam pia. Azam wakigangamala hapo, kisha waombe Yanga wateleze basi wanaweza kuutetea ubingwa wao.
Ama kwa upande wa kushuka daraja, kuna mlolongo wa timu zinazoweza kukumbwa na fagio hilo, hasa ikiwa zile za mkiani zitaamka, na inavyoonekana kuna dalili za kuamka. Tofauti iliyopo kati ya timu inayoshika nafasi ya tano – Ruvu Shooting na ile inayoshika mkia – Tanzania Prisons ni pointi saba tu, zinazoweza kupatikana katika mechi tatu zijazo.
Mtibwa Sugar wana pointi 29 wakifuatiwa na Mtibwa Sugar walioanza ligi kwa kasi ya ajabu, lakini sasa wapo nafasi ya sita wakiwa na pointi 28 sawa na Mbeya City, Mgambo Shooting na Stand United.
Nafasi ya 10 inashikwa na Coastal Union wenye pointi 27 wakifuatiwa na JKT Ruvu wenye pointi 25 sawa na Ndanda FC. Polisi Morogoro wanakuja nafasi ya 13 na pointi zao 24 wakati Tanzania Prisons mkiani wanazo pointi 22.
Kuna mtihani mkubwa katika timu zitakazoshuka daraja, kwani upo uwezekano wa timu inayoshika nafasi ya tano leo hii kushuka daraja iwapo itatetereka na kama zile za chini zitagangamala kwenye hatua hii ya lala salama