Menu
in , , ,

YANGA MPYA INAHITAJIKA..

Klabu ya Dar es salaam Young Africans yenye maskani yake kwenye mitaa ya twiga na jangwani jijini Dar es salaam, tangu kumalizika kwa ligi kuu msimu huu imekuwa ikipitia mambo mengi.Kati ya hayo,yapo ya yanayoleta furaha na mengine ni yale yasimanzi hasa kwa mashabiki wa klabu hiyo kongwe nchini.Kubwa la simanzi kwa siku za hivi karibuni ni kuondokewa na wachezaji wake wawili mahiri,kiungo Franko Domayo na mshambuliaji Didier Kavumbagu ambao wote kwa pamoja wamejiunga na mabingwa wapya timu ya Azam.

Kuondoka kwa Domayo kumewatia simanzi mashabiki wengi wa wana jangwani hao kwa sababu,kiungo huyo amekuwa ni aina ya mchezaji ambaye anaongezeka kiwango kila iitwapo leo.Umri wake mdogo,uwezo wa kumiliki mpira,kupiga pasi zenye macho na nidhamu yake ndani na nje ya uwanja ni baadhi ya sifa zinazomfanya Frank aendelee kuwa bora Tanzania.Maisha ya mpira yana muda mfupi sana kwa hiyo,Domayo anahitaji kuundaa maisha yake ya baadae kuanzia leo na hivyo unaweza ukawa ni uwamuzi mgumu kwa shabiki lakini ukawa na maana kama mwanamichezo.

Kama hiyo haitoshi,kuondokewa na mshambuliaji wa aina ya Didier Kavumbagu wanayanga wanaweza wasisikitike sana kutokana na hazina ya watu wa kucheza nafasi hiyo walionao.Watu kama Mrisho Ngasa ambaye amefunga goli 13 msimu huu,Jerryson Tegete na washambuliaji wawili raia wa Uganda Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza lakini,ukweli utabaki pale pale,Kavumbagu ni aina ya mchezaji ambaye kwenye soka la kisasa kila timu ingependa kuwanaye.Uwezo wake wa kumiliki mpira,mbio,urefu wake na roho ya kikamanda uwanjani,ni sifa zinazomfanya awe mchezaji wa kipekee sana uwanjani.

Klabu ya Yanga pia,imeibuka na habari njema.Kuanzia tarehe 16 mei 2014 wanajangwani hao watazindua kadi mpya za wanachama ambazo zipo kwenye mfumo wa kidijitali baada ya kuingia makubaliano na benki ya posta Tanzania na kwa sasa,wanachama wa klabu hiyo watapata fursa ya kuichangia timu yao kupitia matawi yote ya benki ya posta nchini.Ada ya kujiunga na wababe hao wa jangwani ni shilingi 15,000 na ada ya mwaka ni shilingi 12,000 kama kawaida.Mpango huu utawasaidia Yanga kuweza kubaini idadi ya wanachama walionao hapa Tanzania lakini pia,itakuwa ni chanzo kizuri cha kujiongezea mapato na kuachana kabisa na taratibu za watu wanaojiita wafadhili ambao mwisho wa siku wamekuwa wakizirudisha timu zetu nyuma.

Klabu ya yanga ambayo imemalizi ligi kuu ikishika nafasi ya pili huku wakijikusanyia alama 56 na kuzidiwa na Azam waliotwaa ubingwa wakiwa na alama 62,hivi punde imetoka kutangaza kuachana na kocha wao mkuu Hans Van Der Pluijm ambaye mkataba wake wa miezi sita ulifikia tamati mwishoni mwa msimu uliomalizika hivi majuzi.Kocha huyo sasa atakwenda kuinoa timu ya ligi kuu ya Al-Shoalah nchini Saudi Arabia na kuiacha Yanga chini ya kocha msaidizi Charles Boniface Mkwasa.

Pamoja na kuwa Hans Van Der Pluijm ameshindwa kuwapatia taji lolote msimu huu,bado mashabiki,uongozi na wapenzi wa Yanga wameonyesha kusikitishwa sana na kuondoka kwa Mholanzi huyo.Hans alifanikiwa kujenga nidhamu ndani ya kikosi cha Yanga hasa pale walipokuwa wanapitia wakati mgumu,mbinu zake uwanjani na namna alivyokuwa anazungumza na vyombo vya habari ni wazi kuwa watu wengi watamkumbuka sana.

Ni mara chache sana kuona mashabiki na wanachama wa timu hasa hizi kubwa hapa Tanzania za Simba na Yanga,wakimpenda mtu ambaye hajawapatia taji lolote lakini kwa Hans Van Der Pluijm hali imekuwa ni tofauti.Mashabiki wataendelea kumkumbuka kwa ushindi wao mkubwa msimu huu wa mabao 7-0 dhidi ya timu ya Ruvu Shooting na ule wa bao 1-0 dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi wa klabu bingwa Afrika timu ya Al-Ahly walioupata jijini Dar es Salaam.

Baada ya kumaliza kwenye nafasi ya pili,timu ya Yanga ina nafasi tena ya kuipeperusha bendera ya taifa la Tanzania kwenye michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika na michuano mingine mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanza maandalizi ya ligi kuu msimu ujao.Ni vema timu hiyo ikaanza maandalizi yake mapema na sisi kama TanzaniaSports,tuna watakia kila la kheri kuelekea uchaguzi wao mkuu na jambo lolote lililoko mbele yao.

51.55671-0.117705

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version