MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga leo (Jumamosi) wanaingia uwanjani kucheza na Villa Squad kwenye mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salam.
Mechi hiyo inakutanisha timu hizo zikiwa kwenye mazingira tofauti, Yanga ikiwania kutetea taji lake na Villa ikipambana kubaki kwenye Ligi Kuu msimu ujao, mazingira hayo ndiyo yanaufanya mchezo huo kutotabirika.
Kocha wa Villa Squad, Habib Kondo ambaye timu yake inashika nafasi ya pili kutoka chini ikiwa na pointi 16 kwa michezo 19 wana kila sababu ya kupambana kwa nguvu leo kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
Kondo alikaririwa wiki chache baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba akisema watapambana kuibakisha timu hiyo kwenye Ligi Kuu, hivyo ni wazi atataka kuendeleza rekodi hiyo kwa kuifunga na Yanga, ambayo pia ni moja ya vigogo vya soka hapa nchini.
Yanga inayoshika nafasi ya tatu baada ya michezo 19 ikiwa na pointi 40 nyuma kwa mchezo mmoja na hasimu wake Simba yenye pointi 44 inayoongoza ligi hiyo na nyuma kwa mchezo mmoja dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili ya Azam yenye pointi 41 ni wazi itataka kuendeleza ushindi wa bao 1-0 ilioupata dhidi ya African Lyon Jumatano ili kuisogelea Simba na kuwa mbele kwa pointi mbili dhidi ya Azam.
Kwenye mchezo dhidi ya Lyon, Yanga ilicheza bila ya nyota wake tisa wa kikosi cha kwanza kwa kufungiwa na Shirikisho la Soka nchini(TFF) na wengine wakitumikia adhabu ya kadi nyekundu ama kuwa majeruhi. Wachezaji hao ni Haruna Niyonzima, Athumani Idd, Hamisi Kiiza, Juma Seif, Nurdin Bakari, Omega Seme, Jerry Tegete, Nadir Haroub na Stephan Mwasika.
Lakini kwenye mchezo wa leo inatarajia kuwa na Athumani Idd, Hamisi Kiiza na Juma Seif ambao wamemaliza kutumikia adhabu ya kadi zao, huku ikiendelea kuwakosa Nurdin Bakari, Nadir Haroub na Omega Seme waliofungiwa kutocheza mechi tatu, huku Tegete na Mwasika wakifungiwa kwa kipindi cha miezi sita na mwaka mmoja kila mmoja.
Kurudi kwa baadhi ya nyota hao kunaweza kuwa faraja kwenye kikosi cha timu hiyo, kwani kilionekana kucheza vibaya kwenye mechi iliyopita dhidi ya African, aidha kuendelea kukosekana kwa baadhi ya nyota hao kwenye mchezo huo kunaweza kuwa faida kwa Villa Squad kwenye mchezo wa leo.
Kwenye mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Azam Chamazi, Yanga iliifunga Villa mabao 3-2, mabao ya Niyonzima, Asamoah na Kiiza.
Kutokana na hali hiyo mchezo wa leo ni wazi Villa yenye masikani yake Magomeni itataka kulipa kisasi na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao, huku Yanga nao wakitaka kushinda kuweza kutetea taji lao.
Villa itakuwa inamtegemea zaidi mshambuliaji Nsa Job ambaye amekuwa aking’ara kwa kufunga mabao karibu michezo yake karibu 7 iliyopita, huku safu ya kiungo ikiundwa na Sixbert Mohammed.