KAULI mbiu ya ‘The Return of Champions’ inaweza kutafsiriwa kuwa mabingwa wa kihistoria Yanga wamerejea katika mashindano ya kimataifa wakiwa katikati ya nuru na giza. Hiyo ni baada ya kupata kipigo cha bao 1-0 nyumbani dhidi ya Rivers United ya Nigeria. Pambano la marudiano kati ya Yanga na Rivers United inatarajiwa kuchezwa Septemba 19 mwaka huu nchini Nigeria.
TANZANIASPORTS inakuletea makala haya ya tathimini baada ya kutazama kwa marudio mara 4 mchezo huo uliojaa mshangao,makosa,uzembe,umahiri na namna makocha wa timu zote mbili walivyosomana kuelekea mchezo wa marudiano.
GOLIKIPA
Kama kuna usajili ambao Yanga wanapaswa kujivunia ni eneo la golikipa Diarra Djigui. Nyanda huyo alionesha uhai kucheza kwa mfumo wa soka la kisasa, mithiri ya Manurl Neuer
Uwezo wa golikipa wao unasisimua mno. Namna anavyofanya uamuzi kuokoa hatari, uwezo mzuri wa kucheza mpira kwa miguu. Kucheza kisasa nafasi ya golikipa kama beki namba tano, yaani golikipa mwenye uwezo wa kupanda hadi nusu ya eneo lao.
Unaweza kumlaumu Djigui kwa kuruhusu bao langoni mwake lakini hadi dakika 90 za mchezo zilipomalizika unaona kabisa ni mchezaji anayeonesha kituambacho hakipatikani kwa makipa wetu.
Kwa mbali Juma Kaseja anaonesha hatua hiyo, huku Aishi Manula akiwa anajiamini na ubora wake hauna shaka. Ninaamini Manula amemwangalia Djigui na bila shaka atamtumia kama mfano.
UHAI WA WASHAMBULIAJI
Uwezo wa kupachika mabao huenda wanao lakini dhidi ya Rivers United walikosa nafasi nyingi. Endapo safu ya ushambuliaji ingetumia nafasi zao kwa usahihi Yanga wangeweza kuibuka na ushindi wa mabao 3 hadi manne.
Rivers wanafanya makosa mengi langoni mwao lakini angalau wanajua namna ya kuopunguza presha ya mchezo. Uhai wa Yanga upo mikononi mwa safu ya ushambuliaji ambayo ilikosa nafasi nyingi za kufunga katika mchezo huo licha ya kuwa katika giza nene lakini eneo hili linaweza kuwapa nuru.
NANI KIONGOZI?
Kikosi cha Yanga kinakosa mchezaji anayetoa amri uwanjani. Mchezaji wa kuelekeza na kuwaamsha nyota wake. Katika nafasi hiyo Lamine Moro alikuwa mahiri, alihamasisha,kuwatuliza wachezaji wenzake hata akiwa benchi.
Katika mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho mkoani Kigoma, Lamine Moro alionesha hali hiyo akiwa benchi. kamera za Televisheni zilimuonesha akionesha ishara ‘tulieni’ hali ambayo ndiyo inatakiwa uwanjani.
Kiongozi mchezaji ndani ya uwanja anatakiwa kuwa na sauti inayosikika na kueleweka. Sina uhakika kama sauti ya Bakari Mwanyeto Nondo inasikika,inakemea na kuamrisha. Lakini hili swali lingalipo.
NI BAHATI AU KUKOSA UMAKINI?
Herieter Makambo na Feisal Salum walikosa nafasi za wazi. Kama Yanga wangekuwa makini basi wangepachika mabao matatu kutoka kwa nyota hao.
Lakini vipi Yanga kukosa nafasi nyingine kwa Athuman Yusuf na Yacouba Sogne kwa nyakati tofauti ni bahati mbaya au kukosa umakini? Nadhani Nasredine Nabi anatakiwa kufanyia kazi eneo hilo la umaliziaji, ambalo lilishindwa kuwapa hamasa Yanga.
AANZE YUSUF, YACOUBA,KASEKE AU MAKAMBO?
Safu ya ushambuliaji angalau inao watu ambao wanaweza kukaa na mpira mguuni kisha wakawa wanakimbia kwa kasi. Eneo hili msimu huu Yanga wanaweza kujivuna kumsajili chipukizi Athuman Yusuf ambaye ameonesha tofauti katika mchezo wao na Rivers United.
Nabi anao mtihani hapa, katikati kuna nuru na giza kuwachagua Makambo,Yacouba,Yusuf au Deus Kaseke. Makambo ana kasi na mashuti ya kufunga. Yacouba ana kasi na uwezo wa kukaa na mpira hivyo kuwa tishio kwa wapinzani.
Deus Kaseke anaweza kusaidia ulinzi kuliko Yacouba na Makambo. Hii ina maana Makambo na Dues ni rahisi kucheza pamoja lakini timu itakosa mshambuliaji wa pili wa kuichachafya ngome ya wapinzani.
Kama Nabi ataamua kushambuliaji Makambo,Kaseke na Yacouba ndio wanaomfaa, huku Muloko akianzia benchi kwa sababu ya washambuliaji hao atacheza Feisal Salum.
AKILI YA NASREDINE NABI
Bila wasiwasi wowote mwalimu huyu alifanya makosa ya kupanga kikosi chake, lakini huwezi kuwapuuza Rivers United kwa uwezo walioonesha na utimamu wa mwili.
Pia huwezi kupuuza kuwa Nabi hakuwa na muda mwingi wa kukaa na kikosi chake. Wachezaji wake walikuwa kwenye vikosi vya mataifa yao hivyo kujikuta akifanya maandalizi kwa mafungu.
Uamuzi wa kumwingiza Ditram Nchimbi mbele ya Deus Kaseke unaweza kuwa mbovu. Lakini kama angetaka kubadili safu ya ushambuliaji basi mpango wa pili angewaingiza washambuliaji wapya watatu; Athuman Yusuf,Deus Kaseke na Ditram Nchimbi kwa maana ya kasi na kujilinda. Mfungaji angekuwa Yusuf na wasaidizi wake ni Kaseke na Nchimbi, kwa maana ya kuingiza akili mpya ya kusaka ushindi.
KILA MTU ANATAKA KUFUNGA
Udhaifu mwingine wa Yanga ni pale timu inakosa mpango madhubuti kwa mchezaji wa kufunga. Kocha Nabi anatakiwa kuja na jawabu juu ya hili.
Yanga walipiga mashuti kuelekea lango la Rivers United lakini ndani ya dakika 45 za kwanza hakuna lililolenga langoni. Ilikuwa kila mchezaji anapigia kujaribu bahati yake jambo ambalo lilikuwa linaigharimu timu.
Mpango madhubuti kwa mfungaji inasaidia kuifanya timu iende kwenye mtiririko mmoja. Amsha amsha yao inahitaji mtu wa kumalizia tu, yaani kutupia wavuni.
UZEMBE WA KUSHANGAZA
Hakuna jambo linalokera katika mechi hii kama Yanga kupoteza pasi katika mazingira ya ajabu. Katika mchezo wa kwanza Yanga walijikuta wakishambuliwa zaidi pale wanapopteza pasi kizembe.
Pasi inapigwa lakini haioneshi kuwa imekusudiwa kumfikia mlengwa. Pasi zinapigwa ilmradi, na makosa ya namna hiyo ndiyo yalichangiwa kuonesha udhaifu wao kuwa hawana uwezo wa kupiga pasi hata 20 mfululizo bila kupoteza. Rivers United walichoiweza Yanga ni uwezo wa kuonana,kucheza kitimu na kutumia makosa yao kuwaadhibu.
ULINZI TAFRANI
Safu ya ulinzi imeendeleza makosa yaleyale yanayofanyika hata kwenye timu ya taifa Taifa Stars. Makosa ya bao walilofungwa Yanga ni yaleyale ambayo Bakari Mwamnyeto aliyoshuhudia Taifa Stars kwenye mashindano ya CHAN nchini Cameroon katika mchezo wao dhidi ya Zambia.
Nahodha huyo wa Yanga angweza kutumika vizuri na kuimarishwa uwezo wake wa kutumia mwili kuwavuruga wapinzani wao, lakini naye alisindikiza kwa macho kama haoni vile.
Ni makosa hayo hayo kwenye mchezo wa Rivers United. Dickson Job ana kasi kuliko Bakari, lakini anahitajika kucheza kwa staili ya Abdala Ninja yaani kuwa na uwezo wa kuona hatari kabla haijatokea.
Ninja anao uwezo wa kuwakabili washambuliaji wapinzani kabla hawajapata pasi huwa ameshatibua. Hofu pekee iliyopo kwake ni kulimwa kadi kutokana na ubabe huo. Lakini walimu wa Yanga wanaweza kuimarisha uwezo wake katika mchezo wa marudiano kisha akawa mchezaji imara kikosini.