Menu
in , ,

YANGA  INATUMIA KICHWA KUTEMBEA NA MIGUU KUFIKIRIA

Tanzania Sports

Jua huchomoza ni mionzi, mionzi ambayo hupokelewa tofauti na wanadamu. Kuna watu ngozi zao hupokea mionzi ya jua kwa furaha na kuna wengine hupokea mionzi ya jua kwa huzuni.

Na hii ni kwa sababu jana yao ilikuwa haiwapi nafasi wao kutengeneza mazingira ya furaha ya leo yao.
Leo imara hutengenezwa na mawazo imara ya jana, udhaifu wa mawazo yako ya jana ndiyo matokeo ya kupata leo yenye maumivu.
Maumivu ambayo husababisha mtu kukosa tumaini, akili yake huwa inafikia ukomo wa kufikiria na mara nyingi akili yake hufikiria namna ya kupata mtu wa kumsaidia kwenye matatizo haya.

Ndipo hapo miguu huwa tunaipa nafasi ya kufikiria na kuamini kichwa ni kiungo sahihi cha kutembelea, ndiyo maana siyo jambo la kushangaza ukisikia kuna kikundi cha wanachama wa Yanga kipo getini kwa Yusuph Manji kikiwa kimepiga magoti na machozi yakifunika mashavu yao kwa minaji ya kumuomba arudi awe mwenyekiti wa Yanga!.

Kwao wao neno mwenyekiti wa klabu ni muhimu kuliko kitu kingine, unajua ni kwanini wanafikiria hivo?,  wanaamini Yusuph Manji akiwa mwenyekiti wa Yanga atatoa pesa zake kwa ajili ya klabu na timu kwa ujumla.

Bado wanaamini kupitia mfuko wa mtu mmoja, hakuna anayewaza namna ya kupata mfuko imara wa klabu ambao utakuwa na msaada kwao. Utaanzaje kuwaaminisha kupitia taasisi imara na waache kufikiria kupitia mtu imara?

Kwao wao mtu imara ni muhimu zaidi kuliko taasisi imara ndiyo maana mtu atakayekuja na wazo la kutengeneza mazingira ya kupata taasisi imara hadhamiki kama mtu ambaye atakuja na pesa zake ambazo atazitoa bila utaratibu wa kibiashara.

Hapa ndipo mwisho wa kufikiria ulipo, hatuwazi nje ya hapa kwenye dunia hii ya kibiashara, dunia ambayo kila kitu ni biashara mpaka ndoa.

Na hii ni kwa sababu tunaamini miguu yetu ina ubongo mzuri wa kufikiria kuliko miguu yetu. Ndiyo maana ni rahisi kusikia viongozi wa Yanga wakirumbana hadharani, hawaoni madhara hasi. Kwao wao wanaona ni kawaida.

Hakuna anayefikiria namna ya kuiokoa Yanga. Yanga inatembea kwa kurudi nyuma ndiyo maana hata matokeo yake ni mabaya.
Huwezi kushangaa mtu akikuambia kuwa mara ya mwisho kwa Yanga kushinda mechi ilikuwa mwezi wa nne. Hili ni jambo la kawaida sana kwa sababu hakuna mazingira dhabiti ya kuifanya Yanga ishinde mechi yoyote.

Kuna wakati unaona kitu kinachoitofautisha Yanga na Lipuli ni jina lakini vitu vingine wanafanana.
Yanga ni taasisi kubwa, taasisi ambayo ina watu ambao wanaweza kutumika kama mtaji wa kutengeneza taasisi imara.
Taasisi ambayo itakuwa haina wanachama au viongozi ambao watakuwa wanamlilia mtu.

Imefikia sehemu Yanga yenye wanachama wengi hapa Tanzania inaamini bila Yusuph Manji hakuna Yanga imara.
Hakuna anayekataa umuhimu wa Yusuph Manji, ila kunatakiwa kutengenezwe mazingira bora ambayo hata mtu fulani akiondoka Yanga inabaki kuwa imara ndani na nje ya uwanja.

Leo hii tunaiongelea Juventus kama timu ambayo inatengeneza pesa nyingi kupitia jezi za Cristiano Ronaldo, wao wamefanikiwa kwa sababu jana  walikuwa na mawazo imara yaliyotengeneza leo ya imara.

Leo ambayo ina viongozi imara wenye maono, viongozi ambao wanajua kipi wanachotakiwa kufanya kwa ajili ya maendeleo ya timu.
Viongozi ambao hawatakuwa tayari kupeleka timu katika mechi imara bila kuwa mkuu kwenye benchi. Kocha ana muda mrefu akiwa nchini lakini viongozi wanaona ni jambo la kawaida kwao kucheza mashindano ya CAF bila kuwa na kocha mkuu kwenye benchi.
Hivi wanajua umuhimu wa kuwa na kocha mkuu kwenye benchi la ufundi? Wanajua kuwa kocha mkuu ndiye kiranja?, ndiye mtu ambaye anatakiwa kubadilisha mbinu kwa uharaka kutokana na mwenendo wa mechi husika?

Ndiye mtu ambaye anasimama kama baba wa familia?, kwao wao wanaona ni kawaida , hakuna anayeshtuka kwa sababu tumezoea kufanya mambo ya kawaida katika ukawaida usio wa kawaida.

Hatuumii na matokeo jana kwa sababu tuliyaandaa. Ligi yetu inamechi chache sana, mechi ambazo hazina faida kubwa kwa wachezaji wetu. Viongozi hawakuona umuhimu wa mechi za Kagame kwa faida ya kuwapa mechi nyingi wachezaji wao.

Waliamini kuwapa mechi za Kagame Cup itakuwa kuwachosha wachezaji, lakini mwisho wa siku jana Yanga walionekana ndiyo wamechoka kuzidi Gor Mahia ambao walishiriki Kagame Cup.

Yanga haikuwa timu ambayo inamaelewanao mazuri ndani ya uwanja kwa sababu hawakuwa na mechi nyingi hivi karibuni za kuwafanya wawe na maelewano mazuri ndani ya timu.

Timu ilionekana imejikusanya siku moja na kwenda kucheza mechi hiyo, hawakuwa na sababu kubwa ya kushinda kwa sababu hawakuandaliwa kushinda mechi hiyo.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version