Ushindi mfululizo wanaoendelea kuupata mabingwa soka nchini, Yanga katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom, umeleta hisia tofauti kwa wapenzi na mashabiki wa Simba na hata baadhi ya viongozi.
Wakati Yanga ikiendelea kujaza kapu la pointi kwa kushinda mechi nne mfululizo, Simba imejikuta ikigawa pointi sita kufuatia kupoteza mechi mbili.
Alasiri imefanya mahojiano na mashabiki kadhaa wa Simba, ambao baadhi yao wamekiri kuwa Yanga inaweza tena kutwaa ubingwa msimu huu.
Mmoja wa mashabiki hao, Juma Hussein, amesema ingawa ligi bado ‘mbichi’ lakini spidi walioonyesha inaitisha.
“Unajua adui yako anapofanya vizuri kwenye vita na wewe unafanya vibaya, bila shaka ni lazima kuwa na wasiwasi,“ alisema.
“Tusingependa kuendelea kuona timu yetu (Simba) ikiendelea kupoteza mechi, na kama hilo litaendelea na Yanga kufanya vizuri, basi hatuna chetu msimu huu.“
Shabiki mwingine, aliyejitambulisha kwa jina la Josephine Mwainjokole, amekiri kuwa Yanga ni timu nzuri msimu huu.
“Timu nzuri ni ile inayocheza na kupata ushindi–unawezaje kusema Yanga ni mbovu wakati inacheza na kushinda? Alihoji na kuongeza, kwenye soka ushindi ni taswira ya kila mmoja.
Shabiki mwingine wa Simba aliyepiga simu mapema leo, John Thomas, amesema Yanga inaweza kutwaa ubingwa kama Simba hawatafanya marekebisho na kuendelea kugawa pointi.
“Wengine watasema hiyo ni nguvu ya soka, lakini kwenye ukweli lazima tusema. Yanga ni timu nzuri, ingawa Simba nayo bado ina nafasi.“
Aidha, kiongozi mmoja wa Simba ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini, mapema leo amesema naye amekiri kuwa Yanga ni kiboko safari hii.
“Kuna hatua ikifika ni lazima useme kweli. Mimi kama kiongozi Simba, nakiri kabisa kuwa wenzetu wana timu nzuri na wamejipanga vizuri kwa ushindi,“ alisema.
Bosi huyo alisema hayo wakati alipoulizwa na mwandishi kuhusu mwenendo mbaya wa Simba kwenye mechi za Ligi Kuu.
“Timu yetu (Simba) si mbaya, kufungwa ni jambo la kawaida ingawa linauma. Tumegundua makosa na sasa tunayafanyia kazi ili kurejea kwenye hali yetu,“ aliongeza.
“Wenzetu wamejipanga vizuri, na kikosi chao ni kizuri, sasa kwanini wasishinde mechi zao. Hii ni changamoto kwetu.“