Kuna habari ya kusisimua kwa wanamichezo nchini. Habari yenyewe inahusu serikali ya Manispaa ya Temeke iliyopo mkoani Dar es salaam. Manispaa hiyo imejenga uwanja wa kisasa wa michezo katika Kata ya Makangarawe umezinduuliwa rasmi Oktoba 17 huku viongozi wa Manispaa hiyo ukitoa wito kwa vijana kushiriki michezo ili kuibua vipaji walivyonavyo.
Ujenzi wa uwanja wa Temeke (Temeke Municipal Stadium) umenikumbusha malalamiko ya kubadilisha ratiba za Ligi Kuu hususani zile mechi zinazotakiwa kuchezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa. Malalamiko hayo dhidi ya TFF ni makubwa na yamekuwa yakifanyika mara kwa mara.
Mtu makini atajiuliza, TFF inalalamikiwa vipi kwa kubadilisha ratiba ya muda wa mchezo kati ya Yanga na Polisi Tanzania ambapo badala ya kuchezwa uwanja wa Mkapa umehamishiwa kwenye uwanja wa Uhuru. Tofauti ni kwamba awali mchezo huo ungefanyika saa moja usiku kwenye uwanja wa Mkapa, lakini uwnaja wa Uhuru hauna taa, hivyo mchezo huo utachezwa saa kumi jioni.
Hapo ndipo hoja ya kuunganisha ujenzi wa uwanja wa Temeke na klabu kongwe kama za Simba na Yanga ambazo zinaonekana kulalamikia kubadilishwa badilishwa viwanja. Pamoja na namna timu za Ligi Kuu zinavyoathiriwa na mabadiliko tajwa.
Aidha, kwenye mazungumzo yasiyo rasmi na kigogo wa zamani wa TFF wiki iliyopita jijini Dar es salaam aliniambia kuwa ili tufanikiwe kuwa na viwanja bora lazima tuvitunze vilivyopo bila kujali mmiliki ni nani. Alisema, “kwa mfano CCM ndio wamiliki wa viwanja vingi vya michezo, wamiliki hawa wanatakiwa kuanzisha kurugenzi ya viwanja vya michezo ambayo itakuwa inashughulikia maendeleo ya viwanja hivyo.
Akaongeza, “nimeona ilani yao CCM wakisesema wataendeleza viwanja vya michezo, iwe kweli waendeleze, tumechoka mambo ya kuona timu zetu zikihangaishwa kwa kufungiwa kwa sababu ya viwanja vibovu kwani makosa sio yao. Unapofungia uwanja wa Sokoine wa Mbeya au Jamhuri mkoani Morogoro zinazoathirika zaidi ni timu, kisha kuna mashabiki ambao wanakosa burudani na fursa za kiuchumi kwa wajasiriamali wadogo na wakubwa. Wageni wanakuja Morogoro,Mbeya,Mara,Moshi na kwingineko kuzitazama Simba au Yanga, halafu kuna mashabiki kununua bidhaa mbalimbali.
Aliongeza kuwa, “Unapovifunga unazuia shughuli za kiuchumi, sasa wamiliki wanatakiwa kuona fursa hii ili wawezeshe viwanja vyao viwe na hadhi. Jambo lingine tunaweza kuwalaumu kamati ya leseni ya TFF ila ukweli wanavumilia mengi lakini wacha sheria ichukue mkondo labda wenye mali watatambua namna nzuri ya kuhudumia viwanja. Nje ya hapo kuna suala la timu zenyewe zinatakiwa kumiliki viwanja vyao.”
Kimsingi hoja ya kigogo huyo ni sahihi, kwa sababu Gambwana ya mkoani Geita wana uwanja wao. Mwadui ya mkoani Shinyanga wana uwanja wao. Ifehu ya mkoani Mbeya wanao uwanja wao, Azam ya jijini Dar es salaam wanao uwanja wao. Yanga hakuna kama ilivyo kwa Simba hakuna uwanja wao.
Azam wanapanga wacheze muda gani, usiku,mchana au jioni, ndiyo raha ya kuwa na uwanja wao. Mara ya mwisho pale Chamazi sikumbuki ni lini wamecheza mchana wa jua kali. Hiyo ndiyo faida ya uwanja wao, kwani wanapanga muda gani wacheze mechi zao kadiri wanavyojisikia.
Baadhi ya watu watauliza, ikiwa Simba na Yanga itafanikiwa kuwa na viwanja vyao, je uwanja wa taifa utatumika kwa shughuli gani? Jibu ni rahisi sana mechi za Timu za Taifa, Taifa Stars, Twiga Stars, Judo, riadha, na matamasha mbalimbali yanaweza kufanyika uwanjani hapo. Vilevile zile mechi ambazo zitakuwa kubwa kuliko uwezo wa viwnaja vidogo zinaweza kuhamishiwa uwnaja wa Mkapa ama wa Uhuru.
Kwanini ninasema hayo kwa makala haya ya pili? Ni wazi kuwa Manispaa ya Temeke imeona fursa kwamba timu za Ligi Kuu zinaweza kutumia uwanja wao kufanya mazoezi, kucheza mechi za kirafiki pamoja na kukodisha kwa matamasha mbalimbali. timu zinapomiliki viwanja vyao ni rahisi kudhibiti ratiba ya mechi zao kwa uwanja wao kutumika kwa shughuli zingine kulingana na ratiba ya mechi. Kwahiyo inakuwa faida kwa tumu kuweza kupanga ni siku gani wakodishe uwanja kwaajili ya tamasha au michezo yoyote kama njia ya kuongeza mapato ya kuendesha viwanja vyao.
Upande mwingine Manispaa ya Temeke inazikumbusha zingine kuona fursa ya kujenga viwanja vyao badala ya kutegemea vile vya CCM kwa shughuli za kiserikali pamoja na kutotumia mwanya wa kumiliki uwanja hali ambayo inawakosesha mapato. Ni wakati wa kusema na kutenda.