Menu
in , , ,

YANGA FANYENI HIVI KWANZA…..

Yanga ndiyo bingwa mtetezi wa ligi kuu Tanzania bara.

Usisahau kuwa ndiyo atakuwa mwakilishi wetu katika michuano ya klabu
bingwa barani Afrika mwezi ujao wa pili.

Michuano ambayo ni migumu kwa sababu inakutanisha mabingwa wa Afrika.

Hapa unatakiwa uwe na kikosi kipana na imara ili kuweza kushindana
katika michuano hii, na ikizingatia kuwa ana kazi ya kutetea ubingwa.

Kutetea ubingwa kunaweza kukaonekana kama kitu kigumu kwake kwa sababu
kazidiwa alama saba (7) na anayeongoza ligi Simba.

Lakini mpira unampa nafasi ya yeye kutetea ubingwa, tukumbuke msimu
jana Yanga ilitoka nyuma ya alama nane (8) na ikachukua ubingwa.

Huwezi tegemea bahati ya aina moja kila mwaka kwa sababu hata mpinzani
huwa anajifunza kutokana na makosa.

Simba walikosea msimu jana, ni ngumu kusubiri Yanga kusubiri Simba
ifanye makosa yale yale ya msimu cha jana.

Cha muhimu ni kwa Yanga kukaa chini na kuja na mpango mahususi wa muda
mfupi wa kuiwezesha timu yao kufanya vizuri kwenye michuano ya klabu
bingwa Afrika, ligi kuu , Kagame na kombe la shirikisho Tanzania.

Vitu gani ambavyo Yanga wanatakiwa kuvifanya kwa haraka kama mpango wa
muda mfupi ??

Kupunguza ukata, mimi bado naamini Yanga haijachelewa katika suala hili.

Wiki hii tumeshuhudia wakiingia mkataba na Macron, ni jambo jema na
lenye tija sana. Wamefikisha idadi ya wadhamini wawili kwa sasa (
sportpesa na macron).

Yanga ni timu ambayo inamtaji mkubwa wa mashabiki, bado wana nafasi ya
kuongeza wadhamini wengine ili kuondokana na ukata unaoikabili timu
kwa sasa.

Ongezeko la wadhamini wengine liwe lengo la muda mrefu , ila kwa
sababu mwezi wa pili ligi ƴya mabingwa inaanza kunahitajika mpango wa
haraka na wa muda mfupi kuinusuru timu.

Yanga ina wapenzi wengi sana, wapenzi wenye uwezo mkubwa wa kifedha.

Muda huu timu imeachwa kwa kina Mkwasa, mzigo unaonekana kuwaelemea
kina Mkwasa ila wanajitahidi sana kuubeba ili wafike.

Itachukua muda mrefu kwao kuwahi kufika kama wataendelea kutengwa.

Ni muda sahihi kwa Wana Yanga kwa pamoja kurudi na kushikamana kwa
pamoja kipindi hiki kigumu kwenye timu.

Watu wenye uwezo wa kifedha Yanga ni wengi, wajitokeze kipindi hiki
waisaidie timu wakati huo uongozi uwe na harakati za kuongeza
wadhamini wengi kwenye timu ambapo ndiyo itakuwa tiba sahihi ya
ugongwa huu wa ukata.

Ukata unaondoka Morali ndani ya wachezaji hivo hata kujituma kwao kunapungua.

Pesa pekee inaweza kuongeza ƘMorali ?. Jibu la hapa ni hapana, kama ni
hapana basi Yanga wanatakiwa wafanye kitu hiki cha pili.

Kitu chenyewe ni kutafuta watu wa Saikolojia ambao watakaa na
kuzungumza na wachezaji.

Kuna nguvu kubwa sana pale wanasaikolojia wanapokuwa wanazungumza na
wachezaji. Kwa sababu mchezaji huzaliwa kwa mara ya pili.

Pia, Yanga inawachezaji wengi ambao wamepita pale ambao waliwahi kutamba.

Waliweka historia katika timu ya Yanga na historia inawabeba.

Wachezaji hawa wana nafasi kubwa ya kuwafanya wachezaji kuwa na Morali
kama wakipewa muda wa kuzungumza na wachezaji hata mara moja kwa wiki
ili kuwapa moyo na kuwatia kupigana sana.

Aina ya uchezaji wa Yanga inawasumbua sana, timu inashambulia pole
pole. Unapokuwa na timu ambayo inayoshambulia polepole haimpi nafasi
mpinzani wako kufanya makosa binafsi.

Mpinzani wako hufanya makosa binafsi kipindi ambacho timu yako
inapokuwa inashambulia kwa kasi, presha inakuwa kubwa kwa mpinzani.

Hiki kitu hakipo ndani ya kikosi cha Yanga. Na hii inatokana na aina
ya kushambulia ambayo Yanga walizoea kuitumia.

Yanga walikuwa wamezoea kutumia wachezaji wa pembeni kushambulia , na
magoli mengi ya Yanga kwa kipindi cha nyuma yalikuwa yanatokea
pembeni.

Kwa sasa hicho kitu hakipo kwa sababu hawana wachezaji wa hivo, sasa
kinachotakiwa kufanywa ni kutumia wachezaji waliopo katika mfumo ambao
utawaruhusu wachezaji waliopo kufurahi na kuwapa matokeo.

Mfano, idadi kubwa ya wachezaji waliopo Yanga wana asili ya viungo wa kati.

Hivyo Yanga wangebadili utamaduni kwa kutumia viungo wa katikati kama
chanzo cha kwao kupata magoli mengi.

Wakimaliza hapo wanatakiwa waweze kuchagua kati ya Kombe la shirikisho
(kombe la TFF), ligi kuu au Kagame.

Kwa muda huu waliopo wanatakiwa kuchagua ni wapi watumie nguvu nyingi.

Hawatakiwi kutumia nguvu nyingi kwenye mashindano yote kwa sababu
kikosi chao ni finyu na wana idadi kubwa ya wachezaji ambao hupatwa
majeraha ya mara kwa mara.

Hapana shaka kombe la klabu bingwa barani Afrika ni muhimu kwao na
wanatakiwa kuwekeza nguvu kubwa huko.

Ila kwa huku nyumbani kuna muhimu wa kwao kuchagua kombe moja kati la
Kombe la TFF, Kagame au Ligi kuu.

Wakiwa na idadi chache ya mashindano ambayo wataamua kuwekeza nguvu
nyingi kulingana na aina ya kikosi walicho nacho naamini itawapa
nafasi kubwa kwao kufanya vizuri.

Ushauri wangu, katika mashindano ambayo hawatayapa nguvu kubwa
wanatakiwa kuwatumia vijana wadogo kama kina Nkomola, Said Musa,
Makka, na wengine ili kuwapa uzoefu na kuwajenga kwa faida ya kizazi
cha kesho.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version