Menu
in , ,

Yanga bila Mayele, Azam bila mipango, refa na kigugumizi

Tanzania Sports

MCHEZO wa kwanza wa Ngao ya Hisani ulichezwa jana Jumatano kwa kuzikutanisha mabingwa wa Soka nchini Yanga na mabwanyenye wa Chamazi, Azam FC. Katika pambano hilo la kusisimua lilishuhudia vita kali ya kutandaza kandanda huku kila timu ikijitahidi kutafuta ushindi. Hadi dakika ya 80 milango ya timu zote ilikuwa migumu, lakini Yanga walionesha kuwa wao ni wazoefu na walitoa ujumbe kwanini walikuwa mabingwa na wanataka ubingwa mwingine kwani kunako dakika ya 86 mambo yalibadilika baada ya kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki kupachika bao la kuongoza. Dakika chache baadaye mshambuliaji kinda Clement Mzize alipachika bao la pili kumaliza mchezo Yanga wakiwa kifua mbele.

TANZANIASPORTS ilikuwa makini kufuatilia mchezo huo wa kwanza na kuzichunguza timu zote mbili zilizokuwa zikikwaruzana katika dimba la CCM Mkwakwani jijini Tanga. Kwa kuzngatia dakika zote 90 Yanga na Azam wana mambo wanayotakiwa kurekebisha, huku wakiwa wameonesha ufanisi pia katika idara mbalimbali. kwanza, kuna ari kwa timu zote; pili kuna ujumbe umetumwa kwenye mbio za Ligi Kuu msimu ujao. 

YANGA BILA MAYELE

Dakika 85 zilionesha Yanga haikuwa na mshambuliaji mwenye maarifa zaidi kuibeba na kuipa bao la kuongoza. Safu ya ushambuliaji ya Yanga iliongozwa na Kennedy Musonda ambaye aina ya uchezaji wake hutokea pembeni kuingia katikati ya eneo la hatari na kupachika mabao. Mara kadhaa alitokea pembeni kulia na kuingia eneo la hatari lakini hakufanikiwa kuliona lango la Azam. 

Musonda ana kasi na uwezo mkubwa wa kupika mashuti pamoja na kufunga mabao katika mazingira magumu, lakini anahitaji nafasi nyingi zaidi ili kufunga mabao. Kwa Fiston Mayele enzi zake hakuhitaji nafasi nyingi ili afunge goli, ukimpa nafasi chache tu lazima wapinzani wao wangelia. 

Katika pambano la Yanga na Azam, kulikuwa na kasi nyingi, mashuti mengi na wachezaji walijaribu kuonesha shauku ya kumshawishi Mwalimu ili wapewe namba kwenye kikosi cha kwanza. Mashuti mengi yalielekezwa langoni mwa Azam, lakini hayakuwa yale ambayo yanakwenda kulitia msukosuko lango hilo au kutikisa nyavu. Yanga inaonekana kutaka kufunga kwa kila staili, kutokea pembeni kulia au kushoto, katikati na eneo la mshambuliaji wa kati. 

Mashuti yalipigwa kutokea upande wao wa kulia alikochezeshwa Yao. Kwa hakika Yanga wametia fora kwa kupiga mashuti langoni mwa adui lakini hayakulenga lango. Bila Mayele Yanga wamekosa nafasi nyingi za kufunga. Wangekuwa na Mayele au mshambuliaji wa aina yake bila shaka Yanga wangeweza kupata chini ya mabao matatu. 

AZAM BILA MIPANGO MBELE

Youssouph Dabo, ndiye kocha wa Azam FC. Mpango wa mechi alioingia nao ulikuwa kudhibiti eneo la ulinzi. Kocha huyu alikuwa na msitu wa wachezaji katika eneo la kiungo mkabaji kwa kutumia mfumo wa 3-5-2 ambao uliwanyima hata nafasi ya kupanga mipango ya maana kushambulia. Prince Dube alijikuta akirudi nyuma kusaka mipira au kusaidia ulinzi, kazi ambayo ingelifanywa na mawinga Aaron Lyanga au Idd Nado, lakini hawakuwapo kikosini. 

Azam walikamia mchezo huo, wamecheza kitemi mno, walikuwa imara kwenye eneo lao la ulinzi lakini wakasahau mipango ya kushambulia. Kocha Dabo atalazimika kurudi kwenye video ya mchezo huo kisha aangalie kwanini alibana uhuru wa Prince Dube kiasi cha kumfanya awe ‘mshambuliaji’beki’ badala ya mshambuliaji. Timu yake haikuwa na mpango thabiti wa kushmbuliaji badala yake ilikuwa na lengo la kutafuta sare. Ni kama vile aliingiza timu yake kinyonge kwani alijaza mfumo wa wachezaji watano katikati ya dimba huku nyuma akipanga mabeki wa tatu. Bahati mbaya hapakuwa na ujanja wa kupenya ngome ya Yanga kwa vile hapakuwa na mshambuliaji aliyeelekezwa kukabiliana na mabeki hao. Hapo ndipo Azam ikakosa mpango wa kushambulia.

KIGUGUMIZI CHA REFA

Refa wa mchezo alikuwa Abdallah Mwinyimkuu. Kati ya maamuzi mengi aliyotakiwa kuyafanya huenda yangeigharimu Azam. James Akamiko alikuwa yuleyule, mwamba wa eneo la kiungo aliyesababisha Skudu atolewe uwanjani ndani ya dakika 6 tu tangu kuanza kwa mchezo baada ya kumchezea vibaya. Lakini mwamuzi Mwinyimkuu alikuwa hajatoa maamuzi ya kumwadhibu James Akamiko, badi kipindi cha pili alipomlima kadi ya njano. 

Laiti angelifanya uamuzi sahihi, bila shaka Mwinyimkuu angeitoa kadi hiyo ya njano ya pili kwa James Akamiko. Maamuzi mengi ya refa yalijaa kigugumizi. Tangu mwanzo mchezo ulikuwa wa presha kubwa na alikuwa anayaona matumizi ya nguvu ambako rafu zilichezwa kama njugu lakini akashindwa kuwalinda wachezaji waliochezewa vibaya.

CLEMENT MZIZE NA LANGO

Kinda huyu anahitaji nafasi ngapi ili apachike bao moja? Kwa dakika chache alizoingia uwanjani kwenye mchezo huo, alipiga mashuti takriabani matano kuelekea langoni mwa Azam hadi pale alipopiga shuti la sita ndipo akapata bao. Mbali ya mashuti hayo, Clement Mzize anaonekana kutamani kupewa majukumu makubwa kikosini. 

Analazimisha magoli, anawasumbua mabeki, anajaribu kupokea na kutengeneza nafasi na zaidi anaipa uhai Yanga katika safu ya ushambuliaji kuwa yupo mchezaji benchi mwenye uwezo wa kubadili matokeo pale mambo yanapokuwa magumu. Mzize anaweza kuwa nyota wa Yanga msimu huu endapo kocha wake Miguel Gmaondi atataka hilo litokee, na hasa atalikumbuka shuti kali lililozaa bao la pili. Lile shuti ni kali sana.

MIGUU YENYE FUNGUO

“Bao la Stephane Aziz Ki ni la kideo”. Ni msemo maarufu sana kwenye viwanja vya soka pale bao zuri linapofungwa na mchezaji anayetegemewa kufanya mambo makubwa. Stephane Aziz Ki alipachika bao la kwanza la Yanga kwa mtindo wa aina yake. Kama nilivyosema hapo juu, Azam walikuwa na msitu mkubwa eneo la ulinzi. 

Aziz Ki alipokea pasi na kutulia, akaangalia kulia na kushoto akaona msitu mkubwa wa wachezaji wa Azam. Akaupeleka mpira kwenye mguu wake wa kushoto, kisha aurudisha kulia na kusogea mbele kidogo. Wakati msitu wa wachezaji wa Azam ukiwa unataka kuendelea kuthibiti asilete madhara, lakini akili ya Aziz Ki ilifanya uamuzi haraka kwa kurudisha mpira huo kwenye mguu wake wa kushoto na piga shuti maridadi lililokwenda moja kwa moja kimyani. Lilikuwa bao tamu sana kwa mwanamichezo.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version