BAYERN MUNICH vs PSG
Wikiendi iliyopita imechezwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jijini Lisbon. Kwa mara ya kwanza Shirikisho la soka barani Ulaya limetumia ubunifu mzuri kukamilisha mechi za Ligi ya Mabingwa baada ya kusimama kwa muda kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
Mashindano ya mwaka huu yalizikutanisha timu zilizofuzu hatua ya robo fainali katika kituo kimoja nchini Ureno. Mchezo wa fainali uliochezwa wikiendi iliyopita umekuwa na mambo mambo yanayoshangaza kidogo. Makala haya ninaeleza yale yaliyoshangaza zaidi….
NGEKEWA YA KINGSLEY COMAN
Mfungaji wa bao pekee la Bayern Munich. Katika umri wake mdogo amechezea timu kubwa mno na ameshatwaa mataji mengi katika umri wa miaka 24 tu. Coman alicheza soka katika akademi ya PSG kabla ya kuhamia Juventus Turin ya nchini Italia kushiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo maarufu kama Serie.
Coman amecheza kwa mafanikio akiwa Juventus, kisha akachukuliwa na Bayern Munich ya Ujerumani ambako ametwaa mataji mbalimbali likiwemo la Ligi ya Mabingwa. Katika umri huo Zinedine Zidane hakuwa mchezaji tishio barani Ulaya.
Katika umri huo huo Eden Hazard hakuwa ametwaa mataji kama Coman. Katika umri huo Paul pogba hakuwa amefanikiwa kama Coman kwa sasa. Ni kama vile Coman ana ngekewa na vilabu vikubwa na mataji. Ni mchezaji mzuri, ana kipaji cha aina yake. kila anakoenda anaibuka na makombe.
MAJIBU YA PHILIPE COUTINHO
Naamini mashabiki wa Liverpool wamekasirika kweli kweli hahahahaha. Wanatamani Coutinho angeendelea kufulia zaidi katika mchezo wa soka kwa sababu aliondoka kwa matamanio ya kutwaa taji la Ulaya. Miezi michache baada ya Coutinho kuhama Anfield, Liverpool wakawa mabingwa wa soka Ulaya.
Coutinho alinangwa mno. Hata lilipofika suala la kurudi Liverpool angalau kucheza kwa mkopo, taarifa zinasema mabosi wa Liverpool hawakutaka. Coutinho akaenda Bayern Munich.
Barcelona ambao waliona Coutinho amefulia kisoka walishuhudia nyota huyo akiwa ndani ya jezi za Bayern Munich alipigilia misumari miwili ya mabao ya fedheha katika kipigo cha mabao 8-2. Bila shaka Barcelona waliumia mabao yale kwani yaliongeza aibu kwao, lakini mfungaji ni mchezaji waliyempuuza.
Coutinho tangu aondoke Liverpool amefanikiwa kutwaa mataji mawili ya La Liga, Cope Del Rey, Super Cup, Bundesliga, DFB Pokal,UEFA, Na zaidi ametwaa mataji matatu kwa mpigo msimu huu 2019/2020.
PSG BILA MCHANA NYAVU
Eneo la namba 9 kwa PSG bado ni dhaifu mbele ya wenye maarifa. Kylian Mbappe bado anahitaji kupevuka ili aweze angalau kuwa mchana nyavu mahiri anayeongoza mashambulizi.
Sisemi Mbappe si mchezaji mzuri isipokuwa anahitajika kupangwa winga wa kulia au kushoto akibadilishana na Nerymar. Nafasi nyingine ni mshambuliaji namba mbili (namba 10).
Kumpanga Mbappe kwenye mchezo ule kama nambari 9 hawezi kuwa tishio mbele mabeki wenye maarifa. Pia Mbappe katika eneo hilo licha ya kasi na kipaji chake bado si mchana nyavu mithiri ya akina Javie Chicharito, Zlatan Ibrahimovic, Ronald De Lima, Edinson Cavani, Philip Inzaghi, Karim Benzema, au Luis Suarez.
Mbappe anahitaji kucheza na washambuliaji wenye maarifa kama Benzema au Roberto Firmino ambao wana mtazamo wa mbali mno kiufundi. Kwenye timu taifa ya Ufaransa Mbappe alikuwa akipangwa na Olivier Giroud. Kazi ya Giroud ilikuwa kumaliza kazi anayofanya Mbappe.
Ni hivyo pia kwa Ronaldo De Lima alikuwa anamaliza kazi iliyokuwa inafanywa na Rivaldo au Ronaldinho. Lakini kocha wa PSG Thomas Tuchel naona alijilisha upepo kumpanga Mbappe kama nambari 9 wake. Hili ilishangaza. Wanahitaji kusajili mchana nyavu mpya sio kutegemea kilio cha Mbappe kupewa majukumu makubwa wakati nafasi alizopata hakufanya makubwa.
MAARIFA YA JOSHUA KIMMICH
Nimetazama fainali ya Ligi ya Mabingwa nikiwa nafurahishwa na maarifa ya beki wa kulia wa Bayern Munich, Joshua Kimmich. Ni mchezaji ambaye anaweza kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, lakini kutokana na eneo hilo kuwa na watu wenye maarifa kumzidi, Pep Guardiola alihusika kumpanga upande wa kulia.
Katika nafasi ya beki wa kulia kulikuwa na mkongwe aliyekuwa anamaliza muda wake Philip Lahm. Ni Lahm pia aliweza kucheza nafasi ya kiungo mkabaji kwa usahihi kabisa. Joshua Kimmmich ndiye silaha inayotisha zaidi ya Bayern Munich. Inanikumbusha namna Real Madrid wanavyotumia silaha ya Marcelo Da Silva. Ukitaka krosi zenye akili peleka mpira kwa Marcelo. Bayern wanamtumia vema Kimmich, na ndiye aliyepiga majalo ya kusisimua kabla Coman kupiga kupachika bao la ushindi la vijana hao wa Bavaria.
MKIMBIZI NA MAKAPI
Nimeyaona mabadiliko makubwa kwa kiungo mkabaji Thiago Alcantara. Nimetazama fainali ya Ligi ya Mabingwa nikiwa nashangaa ubora wa beki wa kushoto wa Bayern Munich, Alphonso Davies.
Thiago Alcantara alionekana kama makapi pale Barcelona. Akalazimisha kuondoka zake kumfuata Pep Guardiola wakati akiinoa Bayern Munich. Katika mchezo wa fainali hiyo Thiago Alcantara ameonesha ni mchezaji mahiri. Kwa sasa akiwa ancheza mpira wa nguvu-kazi, mapafu ya mbwa na shughuli yake inanikumbusha Mhispania mwingine Marco Senna.
Chini ya Luis Aragones na Vicente del Bosque eneo la kiungo mkabaji lilikuwa linalindwa Marco Senna. Kwa hakika mabadiliko makubwa ya ubora wa Thiago Alcantara.
Kwa beki wa kushoto Alhponso Davies hakika amesisimua msimu huu. Beki wa Real Madrid Marcelo amemwagia sifa nyota huyo. Bila shaka natamani siku moja acheze Real Madrid lakini kwa sasa haiwezekani kwa sababu yupo Marcelo, Ferland Mendy na Sergio Reguilon aliyeko kwa mkopo Sevilla. Alphonso ni mkimbizi kutoka Ghana aliyekimbilia nchini Canada mwanzoni mwa miaka 2000 kukwepa migogoro ya kisiasa nchini humo.
PSG BILA THIAGO SILVA
Fainali ya Ligi ya Mabingwa imenishangaza kwa mara nyingine kuona mkoba wa PSG, Thiago Silva anaondoka kwenye klabu huku akiwa na kiwango bora kabisa. Thiago Silva ni beki hodari wa Kibrazil.
Nahusudu uchezaji wake tangu nilipomwona akiwa AC Milan. Lakini sasa anatakiwa kuondoka. Ninachoshangaa zaidi ni kwamba nafasi ya Thiago Silva ni muhimu mno uwanjani, wala Kimpembe hatokuja kumudu majukumu ya Mbrazil huyo. Mfumo wa mabeki watatu wa PSG katika 3-5-2 hauwezi kumpanga Kimpembe bila Thiago Silva au beki yeyote wa kumlinda beki huyo.
Zipo tofauti kubwa baina yao. Kimpembe na Silva wanatofautiana katika uamuzi, ubora,kasi,kiwango na uongozi, ingaw awote wana vipaji vya kuwa mabeki. Silva ni kiongozi ambaye anahitajika mno kuongoza jahazi la PSG. Kimpembe anatakiwa kucheza chini ya kiongozi kuliko kumwacha yeye kuwa beki wa mwisho (mkoba) wa kulinda safu ya ulinzi ya PSG.
MBAPPE ANAPOTEZA MUDA PSG
Ronald De Lima ni mmiliki wa klabu ya Real Valladolid inayoshiriki La Liga nchini Hispania. Ronaldo kama mimi ttumeshachoka na blah blah zinazosemwa na kambi ya Kylian Mbappe.
Ronado amebainisha kuwa ni wakati mwafaka Real Madrid kumsajili Kylian Mbappe kuliko kumfikiria Mbrazil mwenzake Neymar. Mtazamo wa Ronaldo unafanana na namna ninavyuomwona Mbappe ni usajili sahihi kwa manufaa ya baadaye ya klabu hiyo.
Mbappe anahitaji kuboresha baadhi ya mambo ya kiufundi nje ya PSG. Sioni uwezekano wa nyota huyo kuboresha maarifa akiendelea kubaki Ligue 1. Si kwamba Ligue 1 ni mbaya lakini ili uwe na maarifa bora ni lazima ujiunge na ligi yenye kukuongezea uwezo zaidi.
Makosa ya kiufundi, kukosa umakini,kushindwa kutumia nafasi,makosa ya timu, makosa binafsi na kutozungukwa na wachezaji wenye ubora wa juu kunamnyima Mbappe kunakshi uwezo wake. Anatakiwa kufanya kazi na watu wenye kurahisisha kazi yake ili azidi kunoa maarifa yake. kubaki PSG na Ligue 1 ni kupoteza muda wake wa kuwa mchezaji bora duniani. Real Madrid ni nyumba ya mataji.