KAMA ingekuwa kusema mkombozi amewasili kuokoa wahanga basi ujio wa kocha moya wa Barcelona ungefananishwa na hilo. Kama ingekuwa Xavi anafananishwa na mtu aliyekuja kukomboa jamii yake na wtau huenda angelifananishwa na safina la Nuhu kwenye masimulizi ya vitabu vya dini. Lakini hapa tunazungumzia mpira wa miguu ambao unavutia mamilioni ya watu na matrilioni ya fedha duniani.
Xavi Hernandrz ndilo jina linalopasua anga za michezo barani Ulaya. Ukizingatia ushindani uliopo katika Ligi za soka, ni kama vile Xavi amekuja kupandisha alama za umaarufu wa La Liga.
Zamani akiwa na nyota wenzake walifanikiwa kuifanya Barcelona iwe inatetemesha na kuogopesha kukutana nayo. Wakati huo Barcelona ilikuwa chini ya kocha Pep Guardiola, huku injini za timu yake zikiwa chini ya Xavi,Iniesta,Sergio Busquet wakati mbele kulikuwa na washambuliaji hatark Ronaldinho, Lionel Messi, Samwel Eto’o na Thiery Henry.
Ilikuwa Barcelona iliyotia fora barani Ulaya. Akiwa mchezaji wa Barcelona alicheza mechi 767, alitwaa makombe 25, UCL mara mbili na kumaliza nafasi ya pili katika tuzo za mchezaji bora wa dunia mwaka 1998 hadi 2015.
Lakini hivi karibuni Barcelona walilazimika kumfukuza kazi Ronald Koeman, nyota wao wa zamani katika kiti cha ukocha kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo.
Koeman anakuwa mhanga mwingine, kwa sababu tangu kuondoka kwa makocha wawili mahiri, Frank Rijkaard na Pep Guardiola hakuna mwingine aliyefanya kazi kwa ufanisi nje ya Luis Enrique. Wamepita akina Tata Maritino,Ernesto Valverde,Tito Vilanova hadi Ronald Koeman bado mambo yamekuwa magumu.
Sasa ni zamu ya Xavi Hernandez ambaye amekubali kujiunga na klabu hiyo. Xavi amejiunga mwezi huu na mjadala umekuwa mkubwa. Xavi hajafundisha soka barani Ulaya kwa mafanikio na hajawahi kuinoa klabu yoyote bara la Uropa, kwahiyo ukocha wake Barcelona ni wa kwanza.
Wapinzani wake kwa sasa watatakiwa kutazama video nyingi za mbinu za Xavi alipokuwa kocha wa klabu ya Al Sadd ya Qatar.
KANUNI NA SHERIA ZA XAVI
Kwanza, wachezaji wanatakiwa kuwasili uwanja wa mazoezi nusu saa kabla ya muda uliopangwa. Lengo ni kujianda na mazoezi kwa pamoja na kuwaweka karibu wacheaji.
Pili, wafanyakazi wanatakiwa kuwasili saa mbili kabla ya muda wa kuwasili wachezaji. Madhumuni ni kutayarisha kila kitu kwa wakati.
Tatu, wachezaji wote wanatakiwa kula chakula pamoja. Kocha huyo amesisitiza wachezaji wa kikosi cha kwanza wote wanatakiwa kula pamoja chakula cha mchana kinachotayarishwa klabuni hapo ili kuwa na mlo sahihi kuimarisha afya zao.
Nne, ametunga sheria maalumu ya kuwadhibiti wachezaji na kuwatoza faini ikiwa hawatafuata kati zile zilizotungwa kwa aajili yao. ukweli ni kwamba wachezaji wa kulipwa huwa wanachanganya maisha yao binafsi na kazi zao, hivyo kuomba muda wa kufanya mambo ya binafsi zaidi kuliko timu. Xavi ameamua kutumia mbinu waliyotumia makocha Luis Enrique na Pep Guardiola.
Tano, mchezaji yeyote atakayechelewa mazoezini watalipa faini ya euro 100, kosa la pili mchezaji atalipa euro 200, kosa la tatu atalipa euro 400 na kuendelea.
Sita, saa 48 kabla ya siku ya mechi mchezaji hatakiwi kuchelewa kurudi nyumbani (kurudi usiku). Lengo ni kuwapa wachezaji muda wa kutosha wa kupumzika.
Saba, kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii siku moja kabla ya mechi na siku ya mechi.
Nane, wachezaji ambao hawatakuwa kwenye kikosi cha mechi wanatakiwa kuhudhuria mechi wakiwa jukwaani bila kukosa na wanatakiwa kuwepo kwenye vyumba vya kubadilisha nguo uwanjani hapo.
XAVI ANALETA NINI?
Kupitia maelezo yake siku ya kutambulishwa Xavi haonekani kama ataunda timu nje ya misingi ya falsafa ya magwiji wa timu hiyo, wakiwemo Johan Cryff na Pep Guardiola.
Hata hivyo sidhani kuwa Xavi ataleta mafanikio makubwa kama Pep na Enrique, kwa sababu amechukua timu katikati ya msimu. Ni timu ambayo inaonekana imebomoka kupita kiasi lakini imani ya yeye kufanikiwa iko palepale kutokana na misingi aliyopitia na huenda akaunganisha uzoefu huo katika kikosi cha sasa.
Pongezi anazopewa ni nyingi, na wengi wanaamini ataleta mabadiliko. Lakini Barcelona ya sasa haina Lionel Messi badala yake imejaa wachezaji wengi chipukizi na baadhi ambao hawana viwango vya kutosha kuleta mafanikio klabuni hapo. Swali linalobakia sasa ni je Xavi ataleta tabasamu Barcelona?