*Ajeruhiwa mguu na Agger wa Liverpool
ARSENAL wamepata pigo kubwa, baada ya mchezaji wa Liverpool, Daniel Agger anayekipiga Timu ya Taifa ya Denmark kumuumiza Jack Wilshere kwenye mechi dhidi ya England.
Arsenal wamekasirishwa na kitendo cha beki huyo ambapo inasemekana Wilshere ameteguka mguu katika wayo wake katika mechi ambayo England waliwapiga Denmark 1-0 kwa tabu.
Inaelezwa kwamba kiungo huyo muhimu wa Arsenal atakuwa nje kwa walau wiki sita na klabu imethibitisha kwamba alepata maumivu makubwa kwenye mpupa wa wayo huo wa kushoto usiku wa Jumatano.
Licha ya kuumizwa katika dakika ya 12, Wilshere alibaki uwanjani akicheza hadi dakika ya 59 kocha Roy Hodgson alipombadili. Watu wa Arsenal tayari wameeleza mshangao na kuchukizwa kwao na kitendo cha Hodgson kuendelea kumchezesha Wilshere dakika zote hizo licha ya maumivu aliyokuwa nayo.
Hata hivyo, Wilshere anadaiwa kumwambia bosi wake Hodgson kwamba alikuwa fiti kuendelea kucheza na daktari wa timu, Gary Lewin naye akadai kwamba alikuwa fiti, lakini iwapo angetolewa nje muda alipoumia, matatizo yasingekuwa makubwa kama sasa.
Hasira ya wana Arsenal hata hivyo imehamishiwa kwa Agger ambaye anadai kwamba hakudhamiria na kuwa wote walipelekeana miguu na ilikuwa 50/50 wala si yeye aliyemkwatua.
Wilshere anadaiwa pia kudai alikuwa amekwaruzwa tu lakini waliporejea kwenye mazoezi London Colney, alilalamika kutojihisi vizuri na uchunguzi mpya wa kitabibu ukaonyesha kwamba amevunjika mfupa fulani.
Hata hivyo, atapata muda wa kuchezea Arsenal kwenye ligi kuu, japokuwa atavaa kitu cha kuulinda mguu huo usipate madhara. Kabla ya hapo atakuwa akifanya mazoezi gym hadi madaktari watakaporidhishwa na hali yake.
Arsenal inakabiliwa na majeruhi, mmoja wao akiwa kiungo mahiri aliyewasaidia sana mwanzoni hadi katikati ya ligi, Aaron Ramsey, winga Theo Walcott na Kim Källström aliyesajiliwa dirisha dogo kusaidia kiungo lakini akaumia kabla raundi ya pili haijaanza. Anadaiwa ataingia dimbani hivi karibuni.