Mabingwa watetezi wa England, Manchester City wamefikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji na mfungaji bora wa Swansea, Wilfried Bony kwa ada ya pauni milioni 28.
Bonny (26) ni mchezaji wa kimataifa wa Ivory Coast na alijiunga na Swansea mwaka 2013 kutoka Vitesse Arnhem kwa pauni milioni 12. Mwaka jana alifunga mabao 20 kwa klabu yake hiyo.
Inaelezwa kwamba dili hilo linatarajiwa kukamilishwa wiki inayoanza, ambapo Bonny atakwenda kujadili maslahi yake huko Manchester pamoja na kufanya vipimo juu ya utimamu wa mwili wake na afya kwa ujumla.
Hata hivyo, kwa sasa Bony yupo Afrika kwa ajili ya kuwakilisha nchi yake kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayofanyika Guinea ya Ikweta, hivyo huenda akakaa huko kwa wiki tatu.
Awali, Kocha wa Swansea, Garry Monk alisema kwamba mfungaji wake huyo bora angeuzwa kwa bei kubwa sana, vinginevyo abaki Dimba la Liberty. Msimu huu amefunga mabao tisa katika mechi 22, likiwamo la dakika ya mwisho la kusawazisha dhidi ya QPR siku ya mwaka mpya.
Man City walikuwa wakikabiliwa na matatizo kutokana na kuumia kwa washambuliaji wake, Sergio Aguero na Edin Dzeko, hivyo kocha Manuel Pellegrini anataka kuhakikisha anakuwa na wachezaji wa kutosha, maana Aguero amekuwa akijirudia rudia kwenye majeraha.
Klabu hiyo iliadhibiwa na Shirikisho la Soka la Ulaya kwa kukiuka kanuni za uungwana kwenye matumizi ya fedha, hasa kwenye usajili. Pellegrini alikuwa amedokeza awali kwamba hakutarajia kujishughulisha sana na dirisha dogo ambalo lipo wazi hadi mwisho wa mwezi.
Msimu wa kiangazi walitumia pauni milioni 48 kuwasajili beki Eliaquim Mangala, kiungo Fernando na kipa Willy Caballero, lakini waliwauza Jack Rodwell kwa Sunderland kwa pauni milioni 10, kiungo Javi Garcia aliyekwenda Zenit St Petersburg kwa pauni milioni 13.
Mbali na Man City, klabu za Arsenal, Liverpool na Tottenham Hotspur zilitaka kumsajili Bony.